Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba kufuta uteja kwa Mlandege?

Simba Mapinduzi Znz.jpeg Kikosi cha Simba

Fri, 12 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Achana na kelele za namna Mlandege na Simba zilivyofika fainali za Kombe la Mapinduzi 2024, lakini ukweli ni kwamba kesho Jumamosi mashabiki wa soka hususan wale wa visiwani Zanzibar watatapa burudani ya aina yake katika kusindikiza maadhimisho ya Miaka 60 ya Siku ya Mapinduzi ya Zanzibar yaliyofanyika Januari 12, 1964.

Timu za Mlandege ya Zanzibar na Simba zitavaana katika mchezo wa fainali ya Mapinduzi 2024 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, kuanzia saa 2:15 usiku, ikitarajiwa Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi atakuwa mgeni rasmi.

Pambano hilo la fainali ya msimu wa 18 wa michuano hiyo iliyoasisiwa mwaka 2007, linazikutanisha timu ambazo zimepenya hatua hiyo kwa mbinde kwelikweli kwa kupitia mikwaju ya penalti, huku Mlandege ikiwa na kazi ya kutetea taji kwa msimu wa pili na Simba ikisaka taji lake tano kuifikia Azam.

Mlandege ilipenya hatua hiyo baada ya kuiondosha APR ya Rwanda kwenye mechi ya nusu fainali kwa penalti 4-2, baada ya dakika 90 za pambano lao kumalizika kwa suluhu, huku Simba ikiing’oa Singida Fountain Gate kwa penalti 3-2 baada ya dakika 90 kuisha kwa sare ya 1-1.

Timu hizo zote zimetinga hatua hiyo, huku ushindi wao ukiacha gumzo kutokana na maamuzi ya marefa waliochezesha mechi hizo za nusu fainali, ikiwamo APR kunyimwa bao lililoonekana halali lililofungwa na kiungo Shiboub El Sharif na kitendo cha Mwamuzi wa Simba na Singida kuipa Simba kona wakati mpira uliopigwa na Saido Ntibazonkiza kudakwa ukiwa nje na kipa wa Singida.

Kona hiyo ndiyo iliyozaa bao la kusawazisha la Simba lililofanya mchezo huo kuamuriwa kwa penalti na Simba kuvuka ikiifuata Mlandege inayocheza fainali ya pili mfululizo ikiwa ni rekodi kwao na timu za Zanzibar katika michuano ya Mapinduzi.

Mwanaspoti linakuletea dondoo fupi ya rekodi chache za mechi za fainali zilizopigwa ndani ya miaka 17 iliyopita na fainali ya msimu huu inavyoweza kuwa kutokana na viwango vya timu hizo zilizotinga hatua hiyo hiyo baada ya kuzizidi ujanja klabu nyingine 10 zilizoshiriki michuano hiyo.

REKODI ZINAIBEBA SIMBA

Pambano la fainali ya kesho litakuwa la 18 tangu michuano hiyo ilipoasisiwa mwaka 2007, huku Simba ikiwa ni ya tisa na inakutana na Mlandege kwa mara ya kwanza kwenye hatua kama hiyo.

Katika fainali nane za awali ambazo Simba imecheza, mara nne ilibeba ubingwa na nyingine kama hizo ilizipoteza na kuifanya iwe timu iliyocheza fainali nyingi zaidi kuliko timu nyingine, lakini ikishika nafasi ya pili ya kubeba mataji ya Mapinduzi nyuma ya Azam yenye mataji matano.

Ushindi katika mechi ya kesho itaifanya Simba kufikia idadi ya mataji iliyotwaa Azam kwenye michuano hiyo na kuzidi kuboresha rekodi ilizonazo visiwani humo.

Rekodi zinaonyesha Simba ilicheza fainali za kwanza mwaka 2008 ikiwa ni msimu wa pili wa michuano hiyo ilipokutana na Mtibwa Sugar na kuifunga bao 1-0 na kulitwaa taji lililoachwa wazi na watani wao Yanga waliokuwa wamelitwaa msimu wa kwanza nyuma, pia kwa kuifunga Mtibwa mabao 2-1, yaliyowekwa kimiani na Salum Swedi ‘Kussi’ dakika 18 na Gulla Joshua aliyefunga dakika ya 60, huku Abubakar Mkangwa alifunga bao la kufutia machozi la dakika ya 72.

Fainali ya pili kwa Simba 2011 ilikutana na watani wao wa jadi, Yanga na kushinda kwa mabao 2-1 kisha ikatinga nyingine sita zilizofuata ikipoteza 1-0 mbele ya KCCA ya Uganda mwaka 2014 kabla ya kuitambia Mtibwa kwa penalti 4-3 mwaka 2015 na kupoteza 1-0 mbele ya Azam 2017.

Mwaka 2019 hadi 2021 ilipoteza fainali tatu ilizoingia kwa kufungwa tena na Azam kwa mabao 2-1, kisha Mtibwa (2020) kwa bao 1-0 na kulala kwa penalti mwaka 2021 ilipovaana na Yanga.

Mwaka juzi ilizinduka kwa kuifunga Azam kwa bao 1-0 lililopatikana kwa mkwaju wa penalti lililowekwa kimiani na Meddie Kagere na kesho inakutana kwa mara ya kwanza na Mlandege katika mechi ya aina yake kutokana na rekodi baina ya timu hizo zinapokutana kwenye michuano ya Mapinduzi.

Kama hujui, hiyo ni mechi ya nne kwa timu hizo kukutana kwenye Kombe la Mapinduzi kwani tayari zilishakutana mara tatu tofauti katika hatua ya makundi ikiwamo ya msimu uliopita ambapo Mlandege ilishinda kwa bao 1-0.

Lakini awali zilishakutana kwa mara ya kwanza Mapinduzi Cup 2019, mechi iliyopigwa Jan 08, 2019 na timu hizo kukosa mbabe baada ya kutoka sare ya 1-1 sawa na mwaka 2022 ziliposhindwa kufungana, Simba ikiwa na kazi ya kutaka kulipa kisasi kwa watetezi hao waliowakatilia msimu uliopita na kuiondosha mapema.

MLANDEGE HAITABIRIKI

Ukiacha rekodi ya kutowahi kupoteza mbele ya Simba katika michuano hiyo ya Mapinduzi, lakini Mlandege imekuwa ni timu isiyotabirika kirahisi kwani hata msimu uliopita ilifika fainali na kubeba ubingwa bila hata kutarajiwa.

Kwa msimu huu timu hiyo iliyokuwa Kundi A sambamba na Azam, ilivuka robo fainali bila kupata ushindi wala kupoteza, kwani mechi zore tatu iliambulia sare na kukusanya pointi tatu na kukutana na KVZ na kuing’oa kwa penalti baada ya dakika 90 kumalizika bila timu hizo kufungana.

Katika nusu fainali pia timu hiyo ilitoa suluhu na APR ya Rwanda na kuitoa kwa penalti 3-2 na sasa inakutana na Simba katika pambano hilo litakalopigwa kuanzia saa 2:15 usiku. Katika michuano ya msimu huu, Mlandege ni moja kati ya timu iliyokuwa ngumu kufungika kwani katika mechi tano ilizocheza hadi kufika fainali, iliruhusu mabao mawili tu na kufunga mawili ndani ya dakika 450. Mechi mbili ilizoruhusu bao ni zile dhidi ya Vital’O na Chipukizi zilizoisha kwa sare ya 1-1 kila mechi, huku nyingine tatu zikiisha kwa suluhu zikiwamo mbili za mtoani walizovuka kwa penalti.

VITA YA MASTAA

Ukiacha vita ya Simba na Mlandege, lakini fainali inayopigwa kesho ina vita nyingine ya mastaa wanaowania tuzo ya Mfungaji Bora, Kipa Bora na Mchezaji Bora wa michuano ya msimu huu.

Elvis Rupia wa Singida Fountain Gate labda itokee miujiza na kumnyima nafasi ya kubeba tuzo ya Mfungaji Bora, kwani mabao matano aliyofunga kabla ya timu yake kutolewa yanambeba kabisa.

Mbali na Mfungaji Bora, lakini kuna vita ua Mchezaji Bora wa michuano hiyo baada ya awali kila mechi kutoa Nyota wa mchezaji huyo wachezaji watatu pekee kuchaguliwa mara mbili mbili, akiwamo Diao wa Azam, Fabrice Ngoma wa Simba na kipa wa KVZ, Salum Abdallah Salum.

Mbali na wachezaji hao, lakini fainali za safari hii zimeshuhudia wachezaji wengi wakifunika kwa kuupiga mwingi, hivyo kesho haitakuwa ajabu kusikia miongoni mwa wachezaji waliokuwa wakitangazwa kama nyota wa mchezo wa mechi 24 zilizopita wa michuano hiyo akitwaa tuzo hiyo itakayoenda sambamba na mkwanja wa maana kutoka kwa wadhamini.

TATIZO HILI TU

Fainali inapigwa, lakini michuano ya msimu hii imeingia dosari kidogo kutokana na maamuzi tata ya waamuzi, japo baadhi yao wameshaadhibiwa na Kamati ya Waamuzi ya Zanzibar, lakini tayari imeshaaza doa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live