Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba kufunga usajili na Awesu Awesu

Awsu Awesuu Simba kufunga usajili na Awesu Awesu

Fri, 12 Jul 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wachezaji Awesu Awesu kutoka KMC na Kelvin Kijili wa Singida Blach Stars, wametajwa kuwa ndiyo watakaofunga usajili msimu huu kuunda kikosi cha Simba.

Baada ya Kijili kutangazwa kuwa ni mchezaji wa Simba, Habari kutoka ndani ya klabu hiyo zinasema kuwa taratibu zinamaliziwa kuweza kumtangaza Awesu ambapo ataungana na Kijili kukwea pipa kwenda kuungana na wachezaji wenzao nchini Misri ambako imeweka kambi kwa ajili ya msimu ujao wa michuano ya kitaifa na kimataifa.

"Ni kweli, tunaendelea na mazungumzo ya mwisho, dirisha la usajili bado lipo wazi, na hawa ndiyo watatufungia dirisha, hapo tutakuwa tumeshakamilisha kazi," kilisema chanzo ndani ya klabu hiyo.

Awesu anakwenda kuongeza nguvu kwenye eneo la kiungo mshambuliaji, huku Kijili akienda kupeleka changamoto kwa beki wa kulia, Shomari Kapombe pamoja na Israel Mwenda, huku David Kameta akiondoka kwa mkopo.

"Tumesajili beki wa kushoto Valentin Nouma kwenda kumpa changamoto Tshabalala (Mohamed Hussein), sasa ule upande wa Kapombe ulikuwa bado, tulikaa na kuona Kijili anafaa, na Awesu ametuonyesha kuwa ni mmoja wa wachezaji wa Kitanzania ambao ana uwezo mkubwa, anajitambua na mwenye nidhamu, tumeamua kumsajili," kiliongezea kusema chanzo hicho.

Ingawa hakutaja majina ya wachezaji, Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu hiyo, Ahmed Ally alikiri kuna maingizo mengine ya wachezaji wachache ndani ya kikosi.

"Tumefanya usajili kwa asilimia 98, kuna wachezaji wachache kama wawili watatu ambao watakuja kukamilisha kikosi, na kuna 'thank you' kama nne zinakuja, na niwaambie kuwa kwa sasa wanachama na mashabiki wa Simba wasiwe na wasiwasi, kikosi kinaandaliwa Misri," alisema Ahmed.

Mpaka sasa Simba imesajili wachezaji sita wapya wazawa kuelekea msimu ujao.

Tayari imeshawatia mikononi, Lameck Lawi kutoka Coastal Union, Abdulrazack Hamza wa Super Sports ya Afrika Kusini, Valentino Mashaka, akitokea Geita Gold,  Omari Omari aliyekuwa akikipiga Mashujaa FC na Yusuph Kagoma kutoka Singida Black Stars.

Pia imesajiliwa wachezaji saba wa kigeni ambao ni Nouma, kutoka FC Saint Eloi Lupopo ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Jushua Mutale kutoka Power Dynamos ya Zambia, Steven Mukwala kutoka Asante Kotoko ya Ghana, Jean Charles Ahoa kutoka, Stella Adjame ya Ivory Coast, Debora Fernandes Mavambo kutoka Mutondo Stars ya Zambia, Augustine Okajepha, kutoka Rivers United ya Nigeria na Karaboue Chamou, akitokea klabu ya Racing Club d'Abidjan ya Ivory Coast.

Wakati huo huo, klabu hiyo imekanusha kuwa itamtoa kwa mkopo mchezaji wake Hussein Kazi, ambaye awali ilidaiwa hajasafiri na kikosi.

"Kazi yupo kikosini, kumekuwa na maneno maneno mengi kuwa amerudishwa, hayana ukweli, yeye yupo Ismailia akiendelea na mazoezi na wenzake," alisema Ahmed.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live