Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba kuendeleza msako nafasi ya pili

Balua Simba Sz Simba kuendeleza msako nafasi ya pili

Fri, 17 May 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kikosi cha Simba leo kitaendeleza kampeni yake ya kujaribu kusaka tiketi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika itakapocheza na Dodoma Jiji FC kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaochezwa Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.

Simba inapambana kumaliza ligi kwenye nafasi ya Pili ili kupata tiketi ya kushiriki michuano hiyo mikubwa Afrika kwa ngazi ya vilabu.

Leo itaumana na Dodoma FC  kwenye mchezo wa 28 wa Ligi Kuu ambayo inaelekea ukingoni huku wakishuhudia watani zao Yanga wakitangaza ubingwa huku wakiwa na michezo mitatu mkononi.

Akizungumza na gazeti hili, Kaimu Kocha Mkuu wa Simba, Juma Mgunda, alisema mchezo huo ni muhimu kwao katika kusaka kumaliza kwenye nafasi ya pili ya ligi hiyo.

“Tumejiandaa vizuri, utakuwa mchezo mzuri na sisi lengo letu ni ushindi, kama nilivyosema huko nyuma ligi haijaisha, tunaweza tukafanya vizuri kwenye michezo iliyobakia na kumaliza katika nafasi ya pili," alisema Mgunda.

Aidha, alisema anafahamu Dodoma FC ni timu nzuri na wenyewe watapambana kuhakikisha wanapata ushindi kwenye mchezo huo hivyo lazima wawe makini nao.

"Tulipofika sasa kwenye Ligi hakuna mchezo mwepesi, kila timu inapambana kupata ushindi kwenye michezo iliyobakia, sitarajii mchezo mwepesi na ndio maana nasema tumejiandaa vizuri na tutapambana kupata alama tatu," alisema Mgunda.

Simba inachuana na Azam kwenye kusaka nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi ambapo mpaka sasa kwenye msimamo, Azam yupo nafasi ya pili akiwa na pointi 60 akifuatiwa na Simba wenye pointi 57.

Kwa upande wake, Kocha Msaidizi wa Dodoma Jiji, Kassim Liogope alisema wanaiheshimu Simba kwa kuwa wana wachezaji wenye uzoefu mkubwa lakini wamejipanga kupambana nao uwanjani kwa lengo la kuondoka na pointi tatu.

Alisema hawatawadharau wapinzani wao na watakazania kwenye mbinu na maandalizi yao kwa ajili ya mchezo huo muhimu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live