Wakati taarifa zikieleza kuwa Mchezaji ‘KIRAKA’ wa Simba SC, Nassoro Kapama akiwa katika hatua za mwisho kutemwa na uongozi wa klabu hiyo, kesho Jumatano (Januari 03) kutafanyika kikao cha kuwajadili pamoja na mwenzake Clatous Chama.
Wawili hao walisimamishwa na uongozi kutokana na kile kinachodaiwa walifanya vitendo vya utovu wa nidhamu, hivyo kesho ndiyo hatima rasmi itafahamika kama wanarudi kikosini au wanaondolewa jumla
Hata hivyo, kutokana na Chama kuwa nchini kwao Zambia na timu ya Taifa ya nchi hiyo inayoshiriki michuano ya Kombe la Mataifa Afrika ‘AFCON 2023’ kikao hicho kitafayika kwa kutumia teknolojia ya video ya Zoom.
Chanzo cha uhakika kutoka ndani ya Simba SC, kinasema: “Simba kwa sasa inahitaji nidhamu kwa kila mfanyakazi, ili kurejea kwenye ushindani na uwanjani kuonyesha kiwango cha juu, kitakachowapa mashabiki furaha na siyo vidonda vya tumbo.
Angalau ujio wa kocha unaanza kuwarejesha kwenye mstari, sasa hatutaki ndani ya timu kusikike mara mchezaji huyu kafanya hivi, mara yule kile, hayo kwa sasa yanakwenda kufikia mwisho.”
Kuhusu Chama, kesho Jumatano kikao kitaamua kama msimu huu uwe wa mwisho kwake baada ya kutumikia timu hiyo tangu alipojiunga nayo msimu 2018, akitokea klabu ya Power Dynamos na baadae kutimkia RS Berkane na hakuchukua muda akarudi tena Tanzania, sijafahamu nini kitatokea, tusubiri tuone.
Wakati huo huo, baada ya kumaliza kikao cha kuwajadili Chama na Kapama ambaye chanzo kinasema tayari kwa asilimia kubwa hana maisha ndani ya timu hiyo na kesho ni kama kumalizia tu, kamati ya usajili itakutana kujadili ni wachezaji gani wanapaswa kuwaongeza na kuwaondoa ndani ya timu.
“Kabla ya dirisha kufungwa kila kitu kitakuwa sawa, pia watakaondoka tunatoa nafasi ya wao kusaka timu za kuzichezea mapema,” amesema.