Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba kibaruani tena leo

Simba Kufanya Mazoezi Usiku Kisa Al Ahly.jpeg Simba kibaruani tena leo

Sat, 13 Apr 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Baada ya kupoteza mechi tatu mfululizo, Simba itakuwa na nafasi ya kujiuliza katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Ihefu (sasa Singida Black Stars) itakayochezwa leo kwenye Uwanja wa CCM Liti, mkoani Singida.

Simba itashuka dimbani na kumbukumbu ya kufungwa nyumbani na ugenini na Al Ahly ya Misri, katika mechi za robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika huku Jumanne iliyopita ikiondolewa kwenye mashindano ya Kombe la FA na Mashujaa FC ya Kigoma kwa kufungwa penalti 6- 5 baada ya sare ya bao 1-1 kwenye dakika 90 za kawaida.

Wachezaji wa Simba, benchi la ufundi na viongozi wa timu hiyo wamewaangukia na kuwaomba mashabiki 'wajazane' kwa wingi uwanjani ili kuishangilia na kamwe wasisuse.

Kocha Msaidizi wa Simba, Selemani Matola, alisema mechi hiyo haitakuwa rahisi, lakini ameahidi kutowaangusha tena mashabiki kwa sababu wanajua wameumia kutokana na timu yao kutofanya vyema.

"Haitakuwa mechi rahisi, ni ngumu, Ihefu (Singida Black Stars), imesajili vizuri, ina kikosi kizuri, wamekuwa na matokeo mazuri katika mechi zao ilizocheza, sisi tunalielewa hilo, tumefanya maandalizi mazuri, tutahakikisha ni lazima tupate matokeo mazuri katika mechi hii.

"Kikubwa niwape pole matokeo yaliyopita, hakuna asiyejua mmeumia katika mechi iliyopita, lakini tuna hakika hatutawaangusha katika mchezo wetu huu, wasituache waje kutupa sapoti,' alisema Matola.

Nahodha Msaidizi wa timu hiyo, Mohamed Hussein Zimbwe Jr alisema wamejipanga kupambana zaidi na kuhakikisha wanashinda mechi hiyo ili kupunguza pengo la pointi kati yao na timu zilizoko juu yao kwenye msimamo wa ligi hiyo.

"Tunahitaji kushinda ili kuhakikisha haturuhusu pengo la pointi baina yetu na wanaoongoza, lakini haliwezi kufanyika kama mashabiki hawawezi kujitokeza kuja kutushangilia, sisi kama wachezaji tunawahitaji wao, tayari kuna vitu tumevizungumza wachezaji wenyewe ambavyo siwezi kuviongea hadharani, kurekebisha hapa na pale.

Kwa maana hiyo, tunawaahidi matokeo mazuri, kwa sababu mechi tatu za nyuma hatujafanya vizuri, tutapambana, alisema beki huyo wa kushoto.

Kocha wa Ihefu, Mecky Maxime, amesema pamoja na uzuri wa Simba, hata wao hawapo katika nafasi nzuri sana, hivyo wanazihitaji sana pointi tatu.

"Tunajua tuna mchezo mgumu dhidi ya Simba, kikubwa sisi kwenye Ligi Kuu bado hatuna matokeo ya kuridhisha, kwa hiyo pointi tatu tunazitaka. Mashabiki waje kwa wingi, mechi itakuwa nzuri kwa sababu Simba ni moja kati ya timu kongwe nchini, wana kikosi bora, ila bahati mbaya wametolewa katika mechi za kimataifa na wanajipanga tena ya kutaka kushiriki msimu ujao," Maxime alisema.

Simba iliyoshuka dimbani michezo 19 ipo katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na pointi 45 huku lhefu ikiwa katika nafasi ya 11 na pointi zake 23 kibindoni lakini imecheza mechi 21.

Mechi nyingine za ligi hiyo zitakazochezwa leo ni kati ya Geita Gold dhidi ya Mtibwa Sugar huku JKT Tanzania itawafuata Tabora United na Kagera Sugar watakuvwa wenyeji wa Dodoma Jiji FC kwenye Uwanja wa Kaitaba ulioko Bukoba mkoani, Kagera.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live