Simba inapitia katika nyakati ngumu kweli kweli. Ni ngumu kuliko nyama ya tembo ambayo haikupikwa vizuri. Ni ngumu kama mawe ya pale Mwanza. Inaumiza sana.
Ndani ya siku tano tu Simba imeondoshwa katika Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho la ndani. Ni huzuni. Ni simanzi kwa wapenzi wa Simba.
Msimu huu walianza na malengo makubwa sana. Waliweka wazi nia ya kufika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Waliweka wazi nia ya kurejesha nyumbani Kombe la FA pamoja na Ligi Kuu Bara. Hesabu zimekwendaje?
Hadi sasa hakuna uwezekano wowote wa kufikia malengo hayo. Katika Ligi ya Mabingwa wameishia robo fainali kama mwaka jana. Sio hatua mbaya sana, ila bado ni nje ya malengo yao.
Kwenye FA wameishia hatua ya 16 Bora. Yaani wameshuka zaidi ya mwaka jana ambapo walitolewa katika nusu fainali na Azam FC. Nini kimewakuta Simba? Ni ngumu sana kueleza. Katika Ligi Kuu tumwachie Mungu.
Simba wamekwama sehemu. Kuna vitu haviendi sawa. Kama ni viongozi, ni walewale waliokuwepo wakati ule wakitwaa mataji. Hawa kina Salim Abdallah ‘Try Again’ na wenzake ndio waliokuwa wakiunda Bodi ya Wakurugenzi wakati ule wanatamba.
Aliyekosekana ni Mohamed ‘MO’ Dewji ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Bodi, lakini bado ameendelea kusalia kama mwekezaji na Rais wa Heshima wa klabu. Ni kweli hatoi fedha? Ni swali ambayo linahitaji majibu ya haraka.
Kama Mo Dewji hatoi fedha ni tatizo moja, lakini ndani ya uwanja Simba ina matatizo mengi zaidi.
Kwa upande wa makocha wana benchi zuri la ufundi. Abdelhak Benchikha ni miongoni mwa makocha wenye wasifu mkubwa sana Afrika. Mwaka jana alikuwa ndiye kocha bora kwa ngazi ya klabu Afrika. Aliteuliwa kuwania tuzo ya Kocha Bora Afrika. Alitwaa Kombe la Shirikisho Afrika na CAF Super Cup kwa kuzifunga Yanga na Al Ahly.
Tuna wasiwasi na uwezo wake? Hapana. Tunaona namna Simba inacheza. Kuna vitu vingi vimebadilika kiuchezaji, lakini kinachokwamisha kufika kwenye kilele cha mafanikio ni ubora mdogo wa wachezaji.
Nilikuwa nikimtazama Shomari Kapombe akimkaba Reda Slim pale Cairo. Bahati mbaya upande ule walicheza Reda Slim na Mohamed Abdelmonem. Kapombe alikuwa hoi. Alitia huruma muda wote. Hakuweza kuendana na kasi ya nyota hao wa Ahly hata kidogo.
Kapombe amechoka. Ubaya ni kwamba Israel Mwenda na David Kameta ‘Duchu’ ambao walitazamiwa kuvaa viatu vyake wameshindwa kabisa. Yaani Kapombe aliyechoka bado ni bora kuliko Duchu na Mwenda walioko vizuri. Inashangaza sana.
Sio kweli Simba inatakiwa kuachana na Kapombe, ila inatakiwa kuleta beki mahiri zaidi yake. Kabla ya Kapombe nadhani wanapaswa kuachana na Duchu na Mwenda kwanza.
Henock Inonga ni beki mahiri. Ana uwezo mkubwa sana. Hata hivyo, Inonga ndiye beki anayeongoza kufanya makosa katika mechi kubwa za Simba. Inafikirisha sana. Kwanini beki mahiri wa timu anacheza ovyo katika mechi kubwa?
Simba inapaswa kulitazama vizuri suala la Inonga. Kama kuna uwezekano wa kupata beki mahiri zaidi ni vyema wakaachana naye. Yawezekana hachezi kwa moyo mmoja. Inonga wa kwenye AFCON na huyu wa Simba ni watu wawili tofauti kabisa. Bahati nzuri inatajwa anajiandaa kuondoka mwenyewe.
Kwenye kiungo Mzamiru Yassin amechoka, umri umekwenda. Babacar Sarr, Fabrice Ngoma na Sadio Kanoute wote wanacheza mpira unaofanana.
Ipo haja ya Simba kupunguza kiungo mmoja hapa na kutafuta mwingine mwenye uwezo wa kushambulia. Vinginevyo ni matumizi mabaya ya nafasi kuwa na viungo watatu wanaocheza soka linalofanana.
Saido Ntibazonkiza amechoka. Akili inataka mwili hautaki. Siku hizi anasubiri kufunga mabao ya penalti tu. Ndani ya uwanja, hana maajabu tena. Sikushangaa alivyokosa nafasi ya wazi dhidi ya Al Ahly. Enzi zake pale Saido angekosaje?
Luis Miquissone ni fedha iliyopotea gizani. Natamani kuamini huenda akarudi katika ubora wake, lakini akili inagoma. Ni ngumu sana kuendelea kuamini. Ila kwa namna Leandre Onana anavyocheza kama vile hataki, ni bora kubaki na Miquissone na kuachana na Onana.
Sijawahi kumwelewa Onana. Tangu ametua Simba ni mechi mbili tu amecheza vizuri. Alicheza vizuri siku ya Simba Day, kisha akaja kucheza vizuri tena dhidi ya Wydad Casablanca. Baada ya hapo amekuwa tu kama mtumishi hewa. Hakuna cha maana anachofanya.
Muda mwingi anazurura uwanjani. Hakabi. Hatengenezi nafasi kwa wenzake. Hana kasi na anapoteza mipira mingi kirahisi sana. Kwa kifupi hana maajabu.
Kuhusu Pa Omary Jobe na Fred Koublan sitaki kusema sana. Pengine waendelee kupewa muda. Huenda msimu ujao wakawa bora zaidi. Pengine wanashindwa kuwa bora kwa kuwa wanacheza katika timu ambayo inakosa ubora katika maeneo mengi.
Simba ikiachana na nyota hawa inapaswa kutazama aina ya nyota wapya inaowataka. Wawatazame Yao Kouassi na Pacome Zouzoua wa Yanga. Hiki ndio kipimo kipya cha wachezaji bora katika Ligi yetu. Simba inatakiwa kusajili wachezaji wenye uwezo kama Yao au Pacome na zaidi. Tofauti na hapo watakwenda kupoteza muda tena msimu ujao.