Kwenye msimamo wa Kundi B wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Asec Mimosas imekusanya pointi 11. Imeshafuzu robo fainali na imejihakikishia kumaliza kinara wa kundi hilo bila ya kujali matokeo ya mechi ya mwisho.
Chini yao wapo Simba wenye pointi sita, kisha inafuatia Wydad Casablanca yenye pointi sita pia na mkiani ipo Jwaneng Galaxy yenye pointi nne. Timu hizi zote tatu zinawania nafasi moja iliyobaki na kuungana na Asec kwenye robo fainali.
KWANINI ZOTE ZINA NAFASI?
Moja, Simba itafuzu bila ya mjadala ikipata ushindi wa aina yoyote dhidi ya Jwaneng Galaxy. Yaani hata 1-0 ni fresh tu. Haitajali matokeo ya mechi nyingine ya kundi hilo kati ya Wydad itakayokuwa nyumbani dhidi ya Asec ambayo imeshafuzu na itamaliza kileleni.
Lakini pia Simba inaweza kufuzu bila ya ushindi na pengine hata bila ya kufunga bao lolote dhidi ya Jwaneng, endapo itatoka sare ya mabao yoyote au hata ikitoka 0-0, itatinga robo fainali kama tu Wydad hawatoshinda (yaani wafungwe au watoke sare).
JWANENG WANAPENYAJE
Kuna njia ya kwanza hawa jamaa kutinga robo fainali ni kushinda mechi ya Dar es Salaam dhidi ya Simba huku ikiomba Wydad ipoteze kwa Asec. Njia ya pili Jwaneng washinde halafu Wydad asipate matokeo ya ushindi dhidi ya Asec, lakini hiyo pia itategemea idadi ya mabao watakayoifunga Simba. Ni lazima yaanzie 3-0 kwenda juu. Je, Jwaneng ataweza kuifunga Simba 3-0 Kwa Mkapa?
MTOKO WA WYDAD
Faida ya kwanza ya Wydad wanacheza nyumbani. Faida ya pili wanacheza na timu ambayo imeshafuzu na imejihakikishia kuongoza kundi. Mechi hii inaweza kuwa haina presha kwao. Kitu wanachotakiwa kufanya ni kushinda kwanza, huku wakiomba Simba itoke sare na Jwaneng Kwa Mkapa. Wydad watapoteza nafasi ya kufuzu endapo Simba itashinda.
SIMBA WAFANYEJE?
Kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Simba inahitaji ushindi wa aina yoyote ili kuungana na Asec Mimosas, Yanga, Mamelodi Sundowns, Al Ahly, Petro de Luanda na TP Mazembe katika hatua ya robo fainali.
Simba inalingana alama na Wydad Casalanca zote zikiwa na pointi sita, lakini kigezo cha kwanza cha Shirikisho la Soka Afrika (CAF) linachoangaliwa endapo timu mbili zinalingana alama ni matokeo baina yao (head to head).
Hapo Simba ndipo inapata jeuri ya kutaka ushindi bila kuangalia matokeo mengine kwani katika mechi mbili dhidi ya Wydad ilianza kwa kupoteza ikifungwa 1-0 ugenini, lakini ikashinda mchezo wa marudiano nyumbani kwa mabao 2-0, hivyo matokeo ya jumla ni Simba 2-1 Wydad.
Hivyo, Simba na Wydad zikishinda mechi zake za mwisho ambapo zote zitakuwa nyumbani Wydad ikiialika Asec ambayo tayari imefuzu na alama 11, huku Simba ikiisubiri Jwaneng yenye alama nne, basi Simba itatinga robo fainali ya tano ya michuano ya CAF ndani ya misimu sita ya hivi karibuni.
WADAU WAIPA MAUJANJA
Ili Simba ifuzu, makocha, wachambuzi na wadau mbalimbali wa soka nchini wanaipa Simba nafasi ya kushinda mechi hiyo itakayopigwa Jumamosi, lakini wameweka wazi maoni ya namna timu hiyo inapaswa kucheza ili kushinda na kuungana na Yanga katika robo fainali zikiweka rekodi ya Tanzania kuingiza timu mbili katika hatua hiyo.
Beki wa zamani wa Simba ambaye kwa sasa ni kocha wa timu ya taifa ya soka la ufukweni, Boniface Pawasa alisema Simba inahitaji kuiheshimu Jwaneng na kucheza huku akili zote zikiwaza ushindi pekee.
“Lengo la kwanza ni ushindi, benchi la ufundi na wachezaji wote wa Simba wanatakiwa kuhakikisha hilo linatimia. Simba icheze ikijua ikipoteza au kutoka sare tu, itakuwa imewaachia nafasi Wydad watakaokuwa wakicheza na Asec ambao hawana cha kupoteza kwani tayari wamefuzu,” alisema.
“Pili wawe na nidhamu ya mchezo. Wasiende na matokeo bali waiheshimu Jwaneng na kucheza kwa tahadhari zaidi. Simba imekuwa na makosa mengi kwenye eneo lake la ulinzi ambayo muda mwingi yanawasumbua. Wajitahidi kuyapunguza hayo.
“Nashauri benchi la ufundi litumie zaidi mifumo inayotoa nafasi kushambulia ili ipate mabao na ikiwezekana ifunge hesabu kipindi cha kwanza kisha ianze kulinda ushindi. Nadhani hapo Simba itakuwa salama zaidi na mwisho wachezaji wa Simba wajiulize wanaifanyia nini timu?”
Mkongwe wa uchambuzi wa soka nchini, Edo Kumwembe alisema Simba haipaswi kukubali aibu ya kushindwa kufika robo fainali, na inapaswa kucheza kibabe ili kutinga hatua hiyo.
‘’Simba inatakiwa kupambana zaidi. Ikipoteza ni aibu kwao na kwa taifa, lakini pia watataniwa sana na watani zao wa jadi Yanga, ambao wamefuzu robo fainali tayari,” alisema Kumwembe anayechambua pia soka katika gazeti hili.
“Kwa ninavyoijua Simba haitakubali aibu. Itafanya iwezalo kufuzu kwani imekuwa na rekodi nzuri katika Uwanja wa Mkapa. Kikubwa icheze kwa kujua inahitaji kushinda ili isonge mbele na hilo naamini linawezekana.”
Kaimu kocha mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Hemed Suleiman ‘Morocco’ alisema Simba ina wachezaji wengi wenye ubora hivyo wanapaswa kutumia ukubwa kuamua mechi kwa ushindi.
“Wachezaji wengi wa Simba ni wa madaraja ya juu. Wengi wao wanacheza timu za taifa. Hilo linaonyesha ni namna gani ni wakubwa. Wanachotakiwa kufanya ni kuonyesha ukubwa wao katika klabu yao. Wapambane hadi dakika ya mwisho kwani wao ndio wenye dhamana ya kuiheshimisha timu hiyo na taifa kwa ujumla,” alisema Morocco.
MIFUMO, MBINU KUBADILIKA
Akizungumzia kikosi chake, kocha mkuu wa Simba, Abdelhack Benchikha alisema atakuwa na mabadiliko ya kimfumo na wachezaji katika mechi hiyo na wadau wengi wameshauri hivyo.
Benchikha ni muumini wa mfumo wa 4-2-3-1, ambao amekuwa akiutumia pia Simba ambapo hujaza viungo watano na kuweka mshambuliaji wa kati mmoja huku mabeki wakiwa wanne.
“Tunatarajia kuwa na mabadiliko chanya kikosini. Tutawashangaza wengi na naamini yatatulipa na kushinda,” alisema Benchikha.
Awali, Pawasa alisema ishu ya mfumo siyo shida, lakini inabidi wabadilishe aina ya wachezaji anaowatumia kwenye mfumo huo.
“Katika mechi iliyopita aliwatumia viungo watatu wenye sifa sawa (Babacar Sarr, Fabrice Ngoma na Sadio Kanoute). Wote hao ni wazuiaji kwa asili, hivyo pasi zao nyingi zilikuwa za pembeni na siyo mbele. Kunatakiwa kuwa na mtu walau mmoja atakayekuwa anachukua mpira nyuma na kusogea eneo la juu. Kwa aina ya wachezaji waliopo Simba, Mzamiru Yassin, Kibu Denis, na Luis Miquissone wanaweza kufanya kazi hiyo,” alisema Pawasa.
Kwa upande wa Jwaneng, inayonolewa na kocha Morena Ramoreboli raia wa Afrika Kusini, imekuwa ikitumia zaidi mfumo wa 4-3-3, lakini katika mechi ya mwisho iliyopoteza kwa kuchapwa 1-0 na Wydad nyumbani ilitumia 4-2-3-1 sawa na ule inaoutumia Simba.
Jwaneng imekuwa ikitumia zaidi mfumo wa 4-3-3 kwenye mechi za kimataifa hivyo na katika mchezo na Simba kama zote zitaingia hivyo zitakuwa zikifanana na kitakachoamua ni ubora wa mchezaji mmoja mmoja.
VITA YA KISASI
Vita ya kisasi ndiyo kauli mbiu ya Simba kwenye mechi hiyo ambayo imetokana na kufanyiwa unyama na haohao Jwaneng mwaka 2021, kwa kuiondosha kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika katika hatua ya awali jambo ambalo Simba haikutegemea.
Wakati huo, Simba ilianzia ugenini Botswana ambako ilishinda kwa mabao 2-0, na kuhisi imemaliza kazi, lakini katika mechi ya marudiano iliyopigwa kwa Mkapa, Jwaneng ikaamka na kuichapa Simba mabao 3-1 nyumbani yaliyoifanya kuiondosha katika michuano hiyo.
WASIKIE WENYEWE
Kocha Benchikha alisema njia pekee ya kuivusha Simba kwenda robo fainali ni ushindi na wako tayari kufanya hivyo.
“Tuna njia moja tu ya kufanya ambayo ni kupata ushindi. Tutacheza kwa ajili ya kushinda na tunatuma ujumbe kwa mashabiki wetu waje uwanjani kutupa sapoti.
“Tumecheza mechi nzuri Ivory Coast (dhidi ya Asec Mimosas). Tulipoteza nafasi moja nzuri ya kufunga hatukuitumia. Kwa sasa akili yetu tunaielekeza katika mechi inayofuata ambayo naamini tutapata ushindi,” alisema Benchikha aliyeshinda Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita na CAF Super Cup akiwa na USM Alger ya Algeria.
Nahodha msaidizi wa Simba, Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’ alisema: “Itakuwa ni mechi ngumu na itakuwa ni ya kuamua hatima yetu katika michuano hii, lakini uzuri ni kwamba katika hizi mechi za kuamua kwenda robo fainali mara nyingi tumekuwa tukifanya vizuri.
“Tutaendelea kuwasikiliza walimu wetu nini wanahitaji kuhakikisha kwamba mchezo huo tunashinda. Hiyo ni mechi yetu muhimu. Hiyo ni mechi yetu sote. Naamini mashabiki watajitokeza kwa wingi kuhakikisha kwamba tunafanya vizuri.
“Tunaingia katika mechi hiyo kwa tahadhari ili kuhakikisha tunafanya vizuri. Timu yoyote ikiwa ipo katika mechi hizi za Ligi ya Mabingwa ni nzuri na sisi tunawafahamu hivyo tutajipanga.”
Zimbwe ambaye kwa muda mrefu ndiye mchezaji aliyepo Simba aliyedumu zaidi kwenye kikosi hicho ikiwa ni mwaka wake wa 10 sasa, alisema wataipambania jezi ya timu na mashabiki wake.
KWA MKAPA HAWATOKI
Rekodi zinaibeba Simba inapocheza Uwanja wa Mkapa katika mechi za CAF kwani tangu msimu wa 2018/2019, kwenye mashindano yote imecheza mechi 24 na kupoteza mbili ambazo ni ile ilipochapwa 3-1 na Jwaneng na kuondoshwa katika duru la kwanza la Ligi ya Mabingwa mwaka 2021 kwa bao la ugenini baada ya mechi ya kwanza kushinda 2-0 ugenini na matokeo ya jumla kuwa (3-3), na ile ya msimu uliopita dhidi ya Raja Casablanca ilipofungwa 3-0.