Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba inavyotisha kutoa vipigo Mabingwa wa CAF

SIMBA SALIM Simba inavyotisha kutoa vipigo Mabingwa wa CAF

Mon, 24 Apr 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Jumamosi iliyopita ilikuwa ni mwendelezo wa Klabu ya Simba kuwabwaga Mabingwa wa Afrika, ikiwa kwenye ardhi yake ya nyumbani wa Benjamin Mkapa, ikiweka rekodi nyingine ya kushinda mechi zake dhidi ya Mabingwa Watetezi na safari hii ikiwa zamu ya Wydad Athletic Club kutoka Casablanca nchini Morocco kuangukia pua kwa bao 1-0.

Katika mchezo huo wa mkondo wa kwanza wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, straika raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Jean Balele aliingia kwenye orodha ya wachezaji waliofunga mabao dhidi ya mabingwa wanaokufa wakija nchini Tanzania, alitupia bao pekee dakika ya 30 ya mchezo.

Kama nilivyoeleza kuwa hii imekuwa ni kama utamaduni sasa kwa Simba kushinda dhidi ya timu ambazo zinatetea kombe hilo, kwani imeshawahi kufanya mara kadhaa bila kuangalia matokeo ya mechi zake za ugenini, ambapo mara moja imeshawahi kufuzu.

Si kwa Mabingwa wa Afrika tu, hata Mabingwa wa Kombe la Washindi kwani mwaka 1985 katika hali iliyowashangaza wengi iliwachapa Al Ahly ya Misri ambao walikuwa ndiyo watetezi wa kombe hilo.

Ikiwa inalitetea kombe lake la Washindi Afrika ililolichukua mwaka 1884, mechi za 16-bora, Al Ahly ilishuka nchini na ikacheza na Simba kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, ikaangukia pua kwa kuchapwa mabao 2-1.

Mechi hiyo ilichezwa Agosti 22, 1985, Al Ahly ikianza kupata bao dakika ya tano lililofungwa na Mohamed El Khatib 'Bibo', ambaye ndiye alikuwa anatoka kuchukua tuzo la mchezaji bora wa Afrika wakati huo na kwa sasa ndiye Mwenyekiti wa Klabu hiyo, lakini 'Golden Boy', Zamoyoni Mogella, straika hatari kipindi hicho, alisawazisha dakika ya 44 na katikati ya kipindi cha pili, kiungo Mtemi Ramadhani alifunga bao la pili.

Hata hivyo, Simba ilitolewa kwenye michuano hiyo kwa jumla ya mabao 3-2 ilipokwenda kufungwa 2-0 nchini Misri.

Katika makala haya, tunaziangalia mechi ambazo Simba ilipata ushindi nyumbani ikicheza na Mabingwa wa Afrika...

Simba 1-0 Zamalek

Ilikuwa ni Mei 18, 2003 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam (sasa Uhuru), Simba ilipocheza na bingwa mtetezi wa Afrika.

Simba ilishinda bao 1-0 lililowekwa wavuni na straika Emmanuel Gabriel, ambapo pamoja na ushindi huo hakuna aliyeweza kuamini kuwa ingeweza kusonga mbele hasa ikijulikana kuwa inakwenda kucheza kwenye nchi ya Misri iliyokuwa ikisifika si kwa soka tu kwa timu zake, lakini hata mashabiki wenye vituko na vurugu, pamoja na mambo mengi ya nje ya uwanja.

Kwa sababu mechi hiyo ndiyo pekee ambayo Simba iliweza kuwatoa mabingwa watetezi, tuiangalie upande wa pili ilipokwenda kucheza ugenini Juni Mosi mwaka huo huo jijini Cairo dhidi ya mabingwa hao watetezi.

Yeyote aliyetegemea Simba ingefungwa mabao mengi haikuwa hivyo. Ilifungwa bao 1-0 lililowekwa wavuni na nahodha wao wakati huo, Hazem Emam.

Timu hizo zikalazimika kwenda kupigiana mikwaju ya penalti ambapo Simba iliivua ubingwa Zamalek kwa kushinda penalti 3-2. Kipa Juma Kaseja aliibuka kuwa shujaa, akiokoa penalti za Wael El Qabbani, Beshir el Tabei na Mahmoud Abdelrazek Hassan, maarufu kama Shikabala.

Simba iliivua Zamalek ubingwa na kutinga hatua ya makundi, kwani wakati huo ilikuwa ni hatua ya raundi ya pili, baada ya kwanza kuitoa Santos ya Afrika Kusini kwa mikwaju ya penalti pia, kutokana na suluhu mechi zote mbili.

Simba 1-0 Al Ahly

Simba ilipangwa Kundi A na Mabingwa Watetezi Afrika, Al Ahly, ilipofanikiwa kuingia hatua ya makundi mwaka 2021.

Mabingwa hao wa Afrika walikuwa wanatoka kucheza Ligi ya Mabingwa wa Dunia dhidi ya Bayern Munich ya Ujerumani.

Wakiwa wa moto, Al Ahly ilikumbana na kipigo cha bao 1-0 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, lililowekwa wavuni na winga raia wa Msumbiji, Luis Miquissone. Mechi hiyo ilichezwa Februari 23 mwaka 2021.

Ushindi huo ulikuwa ni moja kati ya rekodi ya Simba kuwafunga mabingwa wa Afrika. Inawezekana ilikuwa rahisi kwao kwa sababu msimu uliopita 2019/20 walikuwa wote kwenye kundi moja.

Na pia msimu huo Simba ilishinda bao 1-0 Februari 12 kwa bao lililofungwa na Meddie Kagere, ingawa wakati wanacheza mechi hiyo Al Ahly haikuwa bingwa. Timu hizo zilikuwa Kundi D.

Simba 1-0 Wydad Casablanca

Kwa mara nyingine tena, Simba juzi ilifanya ilichokifanya huko nyuma, baada ya kuichapa Wydad bao 1-0 kupitia kwa Mkongomani Baleke.

Imerudia kama ilivyofanya miaka miwili nyuma. Kinachosubiriwa sasa ni mechi ya marudiano itakayopigwa Aprili 28, mwaka huu kwenye Uwanja wa Mfalme wa Tano nchini Morocco.

Wanachama na mashabiki wa Simba hawahitaji kile kilichofanywa miaka miwili iliyopita kwa sababu tayari kimeshafanyika. Wanachohitaji ni kile kilichofanyika miaka 20 iliyopita jijini Cairo kwa kuwavua ubingwa Zamalek.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: