Bao la dakika ya 34 la kiungo Clatous Chama limetosha kuipa Simba ushindi muhimu wa bao 1-0 ugenini dhidi ya JKT Tanzania mchezo uliomalizika muda mfupi pale kwenye Uwanja wa Isamuhyo, Dar es Salaam.
Chama alifunga bao hilo kwa shuti kali akipokea pasi safi ya mwenzake Said Ntibazonkiza 'Saido' likitosha kuamua mchezo huo na kuifanya Simba kufikisha pointi 36 ikibakiza pointi nne tu kuifikia Yanga iliyo kileleni na alama zao 40.
Hata hivyo, mashabiki wa Simba watafurahia matokeo hayo ya ushindi lakini wakijua wazi kwamba timu yao haikucheza vizuri baada ya JKT kuwabana hasa kipindi cha pili ikiwaandama kwa mashambulizi mengi.
Simba ilipotea kipindi cha pili hasa eneo la kiungo ikionekana kushikwa na JKT lakini wanajeshi hao wakashindwa kusawazisha bao hilo kutokana na kukosa umakini wa washambuliaji wao.
Kipa wa Simba Ayoub Lakreb anaweza kuwa nyota wa mchezo huo baada ya kuwa imara langoni akiibeba timu yake kugomea nafasi za wazi ambazo JKT ilitengeneza za kufunga.
Ushindi huo unaifanya Simba kumaliza mechi zake za mzunguko wa kwanza kwa ubabe ambapo sasa itaanza mzunguko wa pili Jumapili Februari 18 itakaporudi nyumbani kucheza dhidi ya Mtibwa Sugar.