Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba inamhitaji Anthony Barry wake

Simba Sporyts Tr Simba inamuhitaji Barry wake

Sat, 30 Oct 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Unanjua au umeshawahi kumsikia mtu mmoja anaitwa Anthony Barry?

Huyu ni kocha miongoni mwa wasaidizi wa meneja wa Chelsea, Thomas Tuchel ambaye alijiunga na timu hiyo mwaka jana akitokea Wigan Athletic.

Barry (35), jukumu lake kubwa ndani ya Chelsea na hata timu ya taifa ya Ireland ambayo pia anaitumikia, ni kuimarisha safu ya ulinzi.

Ingawa alipokuwa mchezaji kabla hajastaafu alikuwa akicheza safu ya kiungo, Barry amegeuka kuwa mbobezi wa kuisuka safu ya ulinzi na haishangazi kuona akiwa miongoni mwa wasaidizi wanaotegemewa na Tuchel pale Chelsea.

Tofauti na ilivyozoeleka kwa makocha wengi kutokuwa na utamaduni wa kufanya kazi na wasaidizi wa wenzao waliotangulia, hali ilikuwa tofauti kwa Tuchel ambaye mara baada ya kujiunga na Chelsea aliamua kuendelea kubakia na Barry katika benchi lake la ufundi na bila shaka hilo linadhihirisha aliridhishwa na utendaji kazi wake

Hapana shaka uamuzi huo wa Tuchel kubaki na Barry unaleta matokeo chanya kwa timu hiyo hivi sasa kwani ametoa mchango mkubwa kuifanya Chelsea kuwa na safu imara ya ulinzi Ligi ya England hadi sasa kutokana na idadi ndogo ya mabao iliyoruhusu katika mechi tisa ilizocheza mwanzoni.

Chelsea imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara tatu tu ikifuatiwa na Manchester City ambayo yenyewe safu yake ya ulinzi imeruhusu mabao manne.

Lakini sio tu Chelsea ambayo ina mtaalamu aliyejikita katika majukumu ya kuisuka safu ya ulinzi tu bali karibia timu zote barani Ulaya zimekuwa na mtu kama huyo anayeifanya kazi ya meneja au kocha mkuu kuwa rahisi.

Hata timu chache barani Afrika zimekuwa na makocha wa aina hii na hilo limesaidia kwa kiasi kikubwa kuziwezesha kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali zinakoshiriki.

Baada ya Simba kutolewa kizembeLigi ya Mabingwa Afrika msimu huu, pengine huu sasa ni wakati sahihi kwao na hata timu nyingine za Tanzania kuajiri watu kama Barry na kuwapa jukumu la kuimarisha safu zao za ulinzi.

Kwa nini tunasema Simba wametolewa kizembe?

Ni kwa sababu walifanya makosa ya kuruhusu mabao ambayo yamekuwa yakiwagharimu kila msimu, mabao yatokanayo na mipira ya juu.

Bao la pili lilitokana na mpira uliorushwa uliopita juu ya kichwa cha beki kiongozi Pascal Wawa ambaye kwa mshangao wa wengi alisimama tu bila kujishughulisha kuuokoa mpira huo kama ilivyokuwa kwa kipa wake Aishi Manula na kuwapa mwanya Jwaneng Galaxy kufunga bao.

Bao la tatu lilitokana na mpira mrefu uliotokea upande wa kulia na kupita juu ya vichwa vya mabeki wa Simba na kutua kwa mchezaji wa Jwaneng Galax kuunganisha kwa kichwa bila hata kubughudhiwa na beki yeyote wa wawakilishi hao wa Tanzania.

Aina hii ya mabao Simba ilifungwa wakati wa Patrick Aussems, ikarudia kufungwa pindi ilipokuwa ikinolewa na Sven Vandenbroeck na tumeshuhudia tena ikifungwa nyakati hizi ilipokuwa chini ya Didier Gomes aliyeachana na timu hiyo.

Wakati Aussems alipokuwa akiinoa Simba, ushahidi wa uwepo wa tatizo hilo ni mechi dhidi ya AS Vita waliyopoteza kwa mabao 5-0 ugenini na walifungwa mabao matatu ya aina hiyo.

Ikiwa chini ya Vandenbroeck tuliona ikifungwa mabao kama hayo na Samson Mbangula kule Uwanja wa Nelson Mandela walipofungwa bao 1-0 na Prisons, pia Boban Zirintusa wa Mtibwa aliwanyima pointi tatu pale Uwanja wa Jamhuri Morogoro walipotoka sare ya bao 1-1 msimu uliopita.

Inaonekana ni tatizo sugu ambalo makocha watatu tofauti wameshindwa kulitatua na kila msimu limekuwa likiwanyima Simba ushindi kwenye baadhi ya michezo iwe ile ya mashindano ya kimataifa ama ya ndani.

Kama timu zenye hadhi na uwekezaji mkubwa zaidi ya Simba zinaajiri makocha maalumu wa kushughulikia safu ya ulinzi licha ya uwepo wa makocha wakuu wa daraja la juu katika madawati yao ya ufundi, Simba na timu nyingine za Tanzania zinajiamini nini hadi zinashindwa kuwa na watu wa namna hiyo katika vikosi vyao?

Kama Simba na timu nyingine yoyote hapa nchini inataka kufanya vyema kimataifa na kujiweka katika daraja la timu kubwa barani Afrika, hazipaswi kuhofia kutumia hela kupata wataalam kama Barry watakaozifanya ziwe na ngome imara katika timu zao.

Lakini kama wataendelea kuwa na mikono mifupi, basi wasitegemee kutibu tatizo sugu la kushindwa kudhibiti mipira ya juu na mwishowe kila mara watakuwa wanatafuta wasaliti baada ya kufanya vibaya.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz