Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

'Simba inaenda mbele, ikirudi hadi mwaka 47'

Simba Kikaoooooooo Simba

Wed, 27 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Simba ni kati ya timu kongwe Tanzania na Afrika, lakini ikiwa ni moja kati ya zile zilizofanikiwa.

Ukiitoa Yanga, kwa mafanikio ya ndani timu inayofuata ni Simba halafu zitafuata nyingine, kwenye kimataifa inatajwa ndio klabu bora zaidi  ndio maana haishangazi juzi ikitajwa kama klabu ya saba kwa ubora Afrika inayoweza kushiriki michuano ya Klabu Bingwa wa Dunia 2025 itakayoshirikisha timu nyingi zaidi.

Upande wa makombe ya Ligi Kuu Bara, Simba imeshatwaa mara 22 ikiwa ni ya pili nyuma ya vinara, Yanga yenye mataji 29. Simba ilifika fainali ya Kombe la Caf mara moja mwaka 1993, nusu fainali Klabu Bingwa Afrika (sasa Ligi ya Mabingwa Afrika) mara moja mwaka 1974 pamoja na robo mara nne, na mara moja kwenye Kombe la Shirikisho.

Kwenye upande wa mashabiki ni hivyo hivyo, zinakimbizana pia kwa kuwa na mashabiki wengi, hakuna uchunguzi sahihi ambao unaonyesha timu gani inaongoza, lakini zina wafuasi wengi zaidi kwenye soka la Tanzania.

Kumekuwa na fukuto kubwa kwenye klabu hii kwa sasa huku kila mmoja akizungumza lake, lakini matatizo mengi yakionekana yameanza baada ya Simba kulala mabao 5-1 dhidi ya Yanga pamoja na kushindwa kufanya vizuri kwenye michezo ya mwanzoni ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Pamoja na ubora wa uongozi wa Simba, pamoja na baadhi ya mambo ambayo wamekuwa wakiyafanya kwa usasa wa hali ya juu, bado kuna sehemu Simba inataka kurudi enzi za ujima kipindi ambacho soka letu lilikuwa nyuma sana.

ISHU IPO HIVI

Hivi karibuni Rais wa Heshima wa Simba, Mohammed Dewji ‘Mo’ alishauriana na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi na Mwenyekiti wa Klabu kuunda Baraza la Ushauri la Bodi ya Klabu hiyo chini ya Mwenyekiti Jaji Thomas Mihayo na wajumbe wengine 20.

Wajumbe hao ni Hassan Dalali, Ismail Aden Rage, Evans Aveva, Faroukh Baghoza, Swedi Nkwabi, Azim Dewji, Kassim Dewji, Musleh Al-Ruweh, Mohamed Nassor, Mulamu Nghambi, Octavian Mshiu, Prof  Mohammed Janabi, Hassan Kipusi, Geofrey Nyange ‘Kaburu’, Gerald Yambi, Moses Kaluwa, Crescentius Magori, Juma Pinto, Mwina Kaduguda na Idd Kajuna.

Baadhi ya watu ambao walitangazwa ni wengi ambao waliwahi kuwa kwenye kundi maarufu zaidi la soka Tanzania, ‘Friends of Simba’ pamoja na wengine wengi wenye ushawishi mkubwa kwenye soka.

Baada ya uchaguzi uliopita ambao ulimweka Murtaza Mangungu madarakani, yalizuka maneno mengi kuhusu mgawanyiko uliotokea na baadhi ya watu akiwemo Kassim Dewji kutangaza kuachana na soka.

Sio jambo baya kuwa na watu hawa kwenye timu au kuchukua ushauri kutoka kwa viongozi wa zamani au wanachama wa Simba, lakini hawa wanaishauri nini bodi?

Naamini bodi iliyopo Simba imeteuliwa kwa kufuata misingi na inajitosheleza kama kuna sehemu imepwaya basi ingeweza kuwekwa sawa kwa kutafuata watu wengi wakaongezwa, lakini sio kupewa watu wa kuwashauri, wale wanaotakiwa kushauri.

ENZI HIZO

Simba kama ilivyo, ina mabaraza ya wazee, nyuma lilikuwa chini ya Hamis Kilomoni sijui kuhusu sasa na sijui kama linafanya kazi yake ileile, lakini ina wadhamini wa mali za klabu hawa wamekuwa wakiibuka mara moja moja sana likishatokea jambo linalowahusu.

Lakini kwa hawa kina Kaburu, kina Aveva ambao walishafanya kazi yao kwa mafanikio makubwa huko nyuma, sasa ulikuwa muda wao wa kupumzika na kumuachia Abdallah Salim ‘Try Again’ kuendelea na gurudumu la kuiongoza Simba na kama watataka washauri kwa  ujumla pale ambapo wataona panafaa, lakini sio kwa upande wa bodi tu ambayo nayo inashauri.

Simba ilivyo ina viongozi waliochaguliwa wakiwemo hawa wa bodi ambao wapo pale kikatiba kazi yao ni kushauri ili timu  ipate mafanikio na tayari walipomaliza uchaguzi waliweka malengo yao mezani kuwa wanataka kufanya nini kwa kipindi gani, je, watakubali kuchukua ushauri waachane na yale waliyokuwa wamepanga kufanya?

Lakini bodi inafanya kazi na viongozi walioajiriwa kutokana na taaluma zao, nafikiri ilikuwa vizuri kuwaacha watu wafuate taaluma katika  kuiendesha klabu, ili kila mmoja afanye kwa wakati wake na malengo aliyojiwekea.

TATIZO LIPO HAPA

Mfano inawezekana washauri wakawa wanafikiri kitu kifanyike kama ambavyo walifanya wakati wakiwa viongozi lakini sasa zama zimebadilika, au wakati mwingine wakawa na mawazo mazuri ya sasa, lakini bodi ikawa inafikiri tofauti, mawazo yao yasipofanyiwa kazi, utaanza mgongano.

Kwenye hali ya kawaida, bodi pamoja na kuwa na watu wenye taaluma, kazi yake kubwa ni kuwashauri viongozi akiwemo mwenyekiti wa Simba, jinsi ya kuendesha baadhi ya mambo ndani ya timu, wanamshauri pia Mtendaji Mkuu wa Klabu baadhi ya mambo ili timu ipate mafanikio.

Mfano Rais wa nchi akiiteua Bodi ya Korosho, hii haiwezi kuwa na washauri tena nyuma yake, bali ndiyo itawashauri viongozi wa juu akiwemo rais mwenyewe, ndio maana nasema Mo ameteua washauri, wakawashauri washauri.

Hivi nitakuwa sahihi kuamini kuwa uongozi wa Simba akiwemo Rais wa Heshima Mo amekuwa hapati ushauri nzuri kutoka kwenye bodi ndiyo maana akatafuta watu wa kuishauri ili nayo imshauri yeye?

Kuna mambo ambayo naona Simba inataka kurudi nyuma kwenye yale tuliyowahi kuachana nayo kama kamati ya usajili, kwa kuwa usajili ni taaluma kuliko nani anataka nani asajiliwe kwenye timu kwa sasa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live