Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba ina kitu

Simba Squad Warm Up.jpeg Simba ina kitu

Thu, 26 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Hii ni wiki ya heshima kwa Simba baada ya kufanikiwa kupambana na Al Ahly ya Misri kwenye michezo miwili mikubwa Afrika.

Simba ilikuwa haipewi nafasi ya kufanya vizuri kwenye michezo hiyo ya michuano mipya ya African Football League, lakini imeishangaza dunia baada ya kuibana Al Ahly kwenye Uwanja wa Mkapa na kufanya hivyo tena kwenye Uwanja wa Cairo International jijini Misri.

Simba imefanikiwa kuonyesha kiwango cha juu na kuwashtua wapinzani wake wengine kutokana na ubora ambao imeuonyesha pamoja na kwamba imetolewa kwa kanuni ya mabao ya ugenini.

Katika mchezo wa kwanza Simba iliweka rekodi kadhaa kubwa, lakini ufundi wa kocha wake, Robert Oliviera ‘Robertinho’ unaonekana kuwabeba mastaa hao wa Msimbazi kutokana na jinsi ambavyo timu hiyo imekuwa ikicheza.

Huo ulikuwa mchezo wa nane kwa timu hizo kukutana kwenye michuano mbalimbali ya kimataifa na ulikuwa na rekodi kadhaa kali ambazo hazikuwahi kuwekwa huko nyuma, kuonyesha kuwa Simba hii ni tofauti na zile zilizopita.

BAO LA KWANZA CAIRO

Huo ulikuwa mchezo wa kwanza kwa Simba kuambulia sare ikiwa inavaana na Al Ahly kwenye michuano ya kimataifa nchini Misri.

Katika michezo mitatu ambayo ilikuwa imecheza huko nyuma Simba ilipoteza mechi zote ikipoteza kwa vichapo vya 1-0, 5-0, 2-0.

Lakini pamoja na kutoka sare ndiyo kwa mara ya kwanza Simba inafanikiwa kufunga bao kwenye michezo ambayo imekutana na wapinzani wake hao ambao wanashika nafasi ya kwanza kwenye ubora wa soka Afrika.

Lakini kumbuka kuwa hata kwenye mchezo wa kwanza hapa nchini ulikuwa wa kwanza kwa Al Ahly kupata sare na wa kwanza kufunga mabao mawili dhidi ya Wekundu hao, kwani mingine yote ya nyuma ilikuwa imepoteza. Simba ilikuwa imeshinda bao 1-0, 1-0 na 2-1.

Kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa (zamani Uwanja wa Taifa), mabao kwenye sare ya 2-2 yalikuwa ya kwanza kwa Ahly kuifunga Simba, kwani mchezo ambao Simba ilishinda 2-1 ulipigwa katika Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.

ROBERTINHO MTU KWELIKWELI

Moja ya heshima ambayo Simba wanayo kwa sasa ni kuhakikisha wanamtumia vyema kocha Robertinho ambaye amekuwa wa kwanza kutofungwa na Al Ahly kwenye michezo miwili ambayo wamekutana.

Makocha wengine waliopita walifanikiwa kupata ushindi kwenye michezo ya Tanzania, lakini walipokwenda ugenini waliambulia kichapo.

Mbrazili huyu anakuwa wa kwanza kupata sare kwenye mchezo dhidi ya Ahly nchini Misri, lakini akiwa anaendelea kuweka rekodi ya kutofungwa kwenye mchezo wowote kuanzia msimu huu umeanza akiwa ndiye kocha anayeshikilia rekodi hiyo hapa nchini.

KANOUTE REKODI

Kiungo Sadio Kanoute anakuwa mchezaji wa kwanza wa Simba kuifunga Al Ahly nyumbani na ugenini baada ya mastaa wengine kushindwa kufanya hivyo katika michezo nyuma.

Kanoute aliifunga Al Ahly kwenye Uwanja wa Mkapa kwa bao la kichwa wakati Simba ikipata sare ya mabao 2-2, lakini kiungo huyohuyo ambaye juzi alipambana vizuri na staa mwenzake raia wa Mali, Alou Dieng wa Ahly alifanikiwa kufunga bao la kuongoza kwa Simba kwa kichwa.

Huyu ndiye mchezaji pekee wa Simba mwenye mabao mawili kwenye michuano hiyo na anaonekana kuamka baada ya msimu huu kuanza kwa kusuasua na kukosa nafasi kwenye kikosi cha kwanza, lakini kwenye michezo mwili na Ahly ameonyesha umwamba.

KALI KIPINDI CHA PILI

Katika mchezo wa kwanza kwenye Uwanja wa Mkapa, Simba ilifanikiwa kufunga mabao yake kipindi cha pili kupitia kwa Kibu Denis na Kanoute - kipindi ambacho msimu huu Simba ndicho imekuwa ikifunga mabao zaidi.

Katika mchezo wa pili, Simba ilifanya vivyo hivyo baada ya kupata bao katika dakika ya 68 kwenye sare ya 1-1. Katika sare ya bao 1-1 dhidi ya Power Dynamos kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba ilifanikiwa kufunga bao kupitia kwa John Bocco dakika ya 69 katika sare ya 2-2 nchini Zambia Simba ilifunga mabao yake kipindi cha pili dakika 59 na 90 kupitia kwa Clatous Chama na Bocco.

YAWAKUMBUSHA MAMELODI

Simba imekuwa ikitajwa na baadhi ya mitandao ya Misri kuwa imeonyesha jambo ambalo ni adimu kutokea kwenye Uwanja wa Cairo, ikikumbushia matokeo ya sare ya 2-2 kati ya Ahly dhidi ya Mamelodi Sundowns kwenye Ligi ya Mabingwa, Februari, mwaka huu ambapo Ahly ililazimishwa sare. Baada ya mchezo huo sare nyingine inayofuata ni hii ya Simba ya bao 1-1 kwenye michuano ya kimataifa.

Chanzo: Mwanaspoti