Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba imechelewa kupata mbadala wa Chama

Chama Alamba Dili La Ubalozi Clatous Chama

Sun, 26 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kuna nyimbo nyingi nzuri zimeimbwa katika zama hizi. Nyimbo kali za Amapiano na Bongo Fleva. Nani asiyeifahamu Honey ya Zuchu? Mke wa Mtu Sumu ya Alikiba ama Umeyatimba ya Whozu? Ni nyimbo kali kweli kweli.

Lakini pamoja na nyimbo hizi tamu, hakuna inayowasisimua Wanasimba wengi kama jina la Chama. Huyu ndiye Mfalme wa Simba ya sasa. Ndio kipenzi chao. Ndiye anayewapa burudani.

Kwa Wanasimba, chenga na pasi za Chama zinawafurahisha kuliko shoo kali ya Wasafi Festival pale Masaki. Ni kheri washindwe kumuona Diamond Platinumz lakini watalipa tiketi za gharama kwenda kumuona Chama pale kwa Mkapa. Mfalme wa Simba.

Chama ndiye roho ya Simba. Anaamua timu icheze kwa kasi kubwa kiasi gani. Ndiye anaanzisha mashambulizi. Ndiye anaamua presha ya mchezo. Huyu ndiye injini ya timu kwa sasa.

Ni kama ilivyowahi kuwa kwa Emmanuel Okwi kipindi cha nyuma. Alikuwa kipenzi cha Wanasimba kweli kweli. Viongozi wa Simba wangeweza kwenda Uganda kumfuata Okwi ili aje kucheza mechi ya watani wa jadi. Alikuwa roho yao.

Katika zama zake, Okwi alifanya alichojisikia. Angeweza kwenda kwao Uganda na kuzima simu kwa wiki nzima bila taarifa. Wangemfanya nini? Hakuna. Ndiye alikuwa mfalme wao.

Na ukweli ulionekana uwanjani. Okwi aliwapa burudani kubwa Wanasimba kuliko hata ambavyo Professor Jay ama Ommy Dimpoz angeweza kuwakosha. Ndiyo sababu hadi wakati Okwi amechoka, walitamani bado aendelee kusalia Msimbazi. Nyakati zinakuja, nyakati zinapita.

Baada ya nyakati nyingi za Okwi, akaja Shiza Kichuya. Huyu aliimbwa hadi kwenye Nyimbo za Bongo Fleva. Alijua kuwapa furaha wanasimba. Haijalishi Kichuya angefanya nini, kwa Wanasimba alikuwa dhahabu kwao.

Mtu angeweza kushindia mihogo kwa wiki nzima ili tu akamuone Kichuya akiwatesa mabeki wa Yanga pale kwa Mkapa. Zilikuwa nyakati bora sana kwake.

Akauzwa kwenda Misri, na aliporejea akakuta ufalme wake umechukuliwa na Luis Miquissone ‘Konde Boy’. Nyota kutoka Msumbiji aliyekiwasha kweli kweli pale Msimbazi. Kila Kichuya alipomtazama Miquissone, alikubali nyakati zake pale Simba zimekwisha.

Miquissone angeweza kuwafanya mabeki wa timu pinzani kile alichojisikia. Alifunga magoli kwenye mechi ngumu na nyepesi. Alipiga chenga. Alitoa pasi za magoli. Huyu ni Miquissone yule aliyeuzwa kwenda Al Ahly, siyo huyu aliyerudi. Pengine walibadilishiwa uwanja wa ndege.

Hivi ndivyo ufalme wa mtu humalizwa. Kama nyakati za Okwi na Kichuya zilivyomalizwa na Chama na Miquissone, vipi kuhusu nyakati hizi za sasa. Kuna namna Simba imechelewa kutafuta mbadala wa Chama.

Wakati Okwi anaelekea kuchoka, Simba ilimleta Chama. Wakati Chama anaelekea kuchoka sasa, Simba imemleta nani? Hakuna. Tangu msimu ulipita Simba inapambana kusajili wachezaji wengi, lakini hakuna aliyekuja mwenye angalau robo tatu ya sifa za Chama.

Matokeo yake inawaumiza Simba. Kasi ya Chama imepungua uwanjani. Kuna namna kupungua kwa kasi ya Chama kumeipunguza kasi Simba msimu huu.

Huu ni ukweli. Ndiyo sababu kwa sasa Kibu Denis anaonekana kuwa mchezaji mahiri zaidi pale Simba kwa sasa.

Kwa nini Kibu anaonekana mahiri? Ni kwa sababu anajituma. Siyo mchezaji fundi sana, lakini anacheza kwa kujitoa kwa dakika zote.

Lakini je timu imara inahitaji mchezaji anayejituma tu? Hapana. Timu lazima iwe na mchezaji anayejituma na mafundi wa kumtuma kazi. Ndiyo sababu pale Yanga kuna kina Khalid Aucho, Mudathir Yahya, Sure Boy, Zawadi Mauya na wengineo wanajituma kwaajili ya kina Pacome na Aziz Ki.

Ukweli ni kwamba Simba lazima itafute mbadala wa Chama mapema. Ni vyema waka mtafuta wakati huu bado yupo, vinginevyo itawagharimu zaidi hapo baadaye.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live