Baada ya droo ya Ligi ya Mabingwa Afrika kufanyika na Simba kupangwa na Al Ahly kwenye mchezo wa robo fainali, mjumbe wa bodi ya wakurugenzi ya Simba, Issa Masoud amesema kukutana na Ahly mara nyingi katika misimu kadhaa kutasababisha kwenye mechi hiyo Waarabu hao waingie kwa woga.
Katika droo hiyo iliyofanyika leo nchini Misri kuanzia saa 10:00 jioni, Simba imepangwa na Ahly ambayo itakutana nayo kati ya Machi 29 na 30, mwaka huu na mchezo wa mkondo wa pili utapigwa kati ya Aprili 5 na 6.
"Sisi kama Simba tulisema mwanzoni kwamba tupo tayari kukutana na yeyote, lakini tulipendelea sana kukutana na Petro de Luanda. Haikuwa hivyo tumedondokea kwa Ahly, ni timu ambayo tumeshacheza nayo mara nyingi, hususan katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita," amesema Masoud na kuongeza:
"Kwa hivyo kadri tunavyozidi kukutana nao zile mbinu na mipango yake tunakuwa tunaijua."
Msimu huu Simba ilikutana na Ahly kwenye mechi ya ufunguzi ya African League ambapo mchezo wa Dar es salaam ulimalizika kwa sare ya mabao 2-2 kisha ule wa Misri ukamalizika kwa sare ya bao 1-1.
Ikiwa itapita kwenye mchezo huu, Simba itakwenda kukutana na mshindi kati ya TP Mazembe na Petro de Luanda.