Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba ilifungwa kabla ya kukutana na Azam.FC

Azam Vs Simba FT Simba ilifungwa kabla ya kukutana na Azam.FC

Sat, 29 Oct 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Pamoja na kwamba mpira una matokeo matatu, ushindi, sare na kupoteza, kwenye mechi ya Ligi Kuu iliyochezwa juzi kati ya Azam FC na Simba, soka lingekuwa halitendi haki kama Wekundu wa Msimbazi wangeibuka na ushindi kwenye mechi hiyo.

Simba iliyokuwa na wachezaji waliochezea Azam FC tangu mwaka 2008, leo hii iwaje kucheza dhidi ya timu yao ya zamani miaka 14 baadaye wapate ushindi?

Ukweli ni kwamba makocha wa Simba, Juma Mgunda na Selemani Matola walitengeneza wenyewe mazingira ya kufungwa na hili hawawezi kupwepa lawama kwa wanachama na mashabiki wa timu yao ambao wameonekana kulalamika sana baada ya mechi hiyo.

Haikuingia akilini makocha kumpanga Erasto Nyoni kucheza kama beki wa pembeni dhidi ya mawinga wa Azam wenye kasi na wajanja.

Kama makocha wa Simba wangeangalia mechi ya Azam dhidi ya Yanga jinsi mawinga wa Azam walivyowachachafya mabeki wa pembeni wa timu hiyo, sidhani kama wangethubutu kufanya hivyo.

Kama mabeki wa pembeni wa Yanga kina Kibwana Shomari, Farid Mussa, na Djuma Shaaban ambao kwa sasa ni bora sana kwenye Ligi Kuu ya Tanzania walipata taabu na 'kulala na viatu' dhidi ya kina Kipre Junior, Ayoub Lyanga, unawezaje kumweka Nyoni kukabiliana na mawinga hao? Hapa ndipo nasema kuwa Simba ilifungwa kabla hata mechi hiyo kuanza.

Kwanza kabisa, picha inaanza. Haikuwa  na viungo wao ambao wamekuwa tegemeo kwa sasa, Mzamiru Yassin na Sadio Kanoute na hilo likawa pengo kubwa kwenye mechi hiyo. Inakuwaje  tena kuwapa mzigo mwingine wachezaji kuwaongezea mtu ambaye kwa sasa umri umekwenda na hawafai tena kwenye mechi ya ushindani kama ile?

Ilikuwa kama kuchezea shilingi kwenye choo. Kwa timu yoyote ambayo inasaka ubingwa, sifa ya kwanza ni kupata pointi tatu au moja kwa timu ambazo inagombania nazo ubingwa.

Kwa maana hiyo, Simba ilihitaji zaidi pointi tatu au moja dhidi ya Azam ambayo ndiyo timu pekee ambayo kwa maneno na vitendo inaonekana kuusaka ubingwa, na hasa baada ya kuichukua moja kutoka kwa watani zao wa jadi, Yanga.

Makocha wanaojua hivyo, sidhani kama wangecheza mchezo wa hatari kama huo kumuweka Nyoni ambaye pamoja na umri, amekuwa hana tena kasi, wala uamuzi  sahihi mbele ya winga hatari kama Kipre. Kama amekuwa haaminiki hata kwenye mechi dhidi ya Ihefu, inakuwaje kwenye mechi dhidi ya Azam?

Watetezi wanaweza kusema mabeki wa kulia wote ni majeruhi ambao ni Shomari Kapombe ambaye ingawa maerejea bado hana utimamu wa mwili na mwingine ni Israel Mwenda. Lakini  kama makocha wangekuwa makini, wangeweza kumchezesha Keneddy Juma kati na Henock Inonga angeachwa kucheza namba mbili.

Ukiangalia kwenye mechi ya juzi ni kwamba Inonga alikuwa akicheza zaidi kulia akimsaidia Nyoni kuliko kwenye namba yake ya asili. Sasa unajiuliza kwa nini kati pale asingekaa Kennedy kwa sababu hata huyo Nyoni mwenyewe hakuonekana kama anacheza beki wa kulia licha ya kuonekana yupo. Hakuweza kuzuia, wala kupandisha mashambulizi mbele. Na cha ajabu alicheza dakika zote 90.

Ni umakini mdogo wa Azam FC lakini kama wachezaji wake wangechachamaa wangeweza kushinda hata mabao 4-0 dhidi ya Simba ambayo kati kwenye kiungo wa kukaba walikuwa dhaifu na beki wa kulia pia.

Licha ya wachezaji wa Azam kujua tatizo hilo na kupeleka mipira yote upande huo,  makocha wa Simba ni kama waliamua liwalo na liwe, lakini Nyoni hatoki, hivyo kuwapa wakati mgumu baadhi ya wachezaji hasa Inonga na Clatous Chama.

Nilichogundua kwenye mechi hiyo pia kuwa Simba inatakiwa kusajili kiungo mkabaji mwenye kiwango cha juu cha kimataifa kama kweli inataka kupambana kwenye Ligi Mabingwa Afrika.

Hata hawa kina Mzamiru na Kanoute ni msimu huu tu ambao wamekuwa kwenye kiwango kizuri, lakini msimu uliopita nao pia walikuwa wanapigiwa kelele.

Kwa viongozi wa Simba itoshe tu kusema wafanye uamuzi mgumu kwani wakiendelea kuwa na kina Nyoni, Bocco na viungo wakabaji ambao hawafanyi kazi ipasavyo wanakuwa wanajipiga kisu mgongoni.

Wachezaji hawa wameifanyia makubwa kwa kuipa ubingwa mara nne mfululizo, lakini kwa walipofikia inatosha na viongozi wasitake kuwafanya mpaka wachezaji hao wanazomewa ndiyo wawaondoe.

Kwa timu kubwa kama Simba inayotaka mafanikio kwenye michuano ya kimataifa, haina kikosi kipana kwenye viwango vya kimataifa, badala yake wachezaji wawili tu wakiwa majeruhi basi wanaoingia ni wale waliocheza Ligi Kuu tangu katikati ya miaka ya 2000.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live