Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba ikishinda ni Mo Dewji, ikifungwa ni Mangungu

Mangungu Mo Dewji Simba ikishinda ni Mo Dewji, ikifungwa ni Mangungu

Thu, 9 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Simba SC tangu baada ya kubondwa 5-1 na Yanga wameendelea kuweweseka, wamefukuza makocha wawili lakini bado kuna shinikizo kutoka nje kwamba viongozi waondoke pia.

Katika viongozi wanaotajwa na wengi kutaka waondoke ni Mwenyekiti wa Simba SC Murtaza Mangungu wala sio Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Salim Abdallah Muhene ‘Tryagain’ au Mo Dewji.

Nimetafakari kidogo tu kwanini kwenye hili jambo baya anatakiwa Mangungu kuondoka na sio MO Dewji na kwenye mambo mazuri kote anaonekana MO Dewji au mwakilishi wake Tryagain na sio Mangungu?

Ukimuona Tryagain ndio umemuona Mo Dewji kwakuwa SALIM anatokana na upande wake na ukimuona Salim ndio umemuona MO Dewji kwakuwa ndiye aliyemteua.

Wakati wa usajili MO yeye mwenyewe au kupitia Salim atasema ametoa kiasi gani kusajili msimu huu na watu watafurahi sana na kumsifia, timu ikifanya vibaya au usajili kubuma anatajwa Mwenyekiti wa Simba Mangungu kwanini amemsajili Onana kwa mfano.

Simba Day waliokuwa karibu na Rais na pengine hata kuongea ni Salim na MO Dewji, Mangungu hakuonekana sana na hakuna aliyejali.

Ikaja African Football League, Rais wa CAF Dr Patrice Motsepe akamtambulisha MO Dewji kama Mwenyekiti wa Simba na watu wote wakafurahi ilihali Mwenyekiti yupo na hakutambulishwa na hakuna aliyejali.

Leo timu imekula mbao 5 watu wanamtaka Mangungu apishe na sio aliyetambulishwa pale kwenye steji ya AFL.

Labda Simba watuambie kuanzia leo ni wakati gani Mangungu anakuwa Mwenyekiti wao na wakati gani au kwenye matukio yapi anakuwa sio Mwenyekiti? Kinyume chake ni kumuangushia jumba bovu tu.

Kama huko nyuma walikosea kutolisema hili kikatiba au kwa kulitolea maelezo sio vibaya wakasema hata sasa kwakuwa muda wanao, vinginevyo watakuwa wanachanganya watu wenye uwezo wa kuchanganua mambo.

Ukimuona Mangungu vyovyote alivyo leo ni kutokana na katiba yao wakati wanafanya marekebisho kumuingiza muwekezaji, walipoambiwa wanapokosea majibu yalikuwa rahisi tu “tunataka furaha na timu inashinda ndiyo furaha yetu” leo wanapigwa wanataka nguvu za Mwenyekiti wao ambazo hazipo kikatiba, huwezi kula keki ukaimaliza yote kisha ukabaki nayo mkononi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live