Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba hii ya Gomes balaa tupu

Simba Gomes Pic Data Simba hii ya Gomes balaa tupu

Mon, 12 Apr 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

KIKOSI cha Simba kimerejea jijini Dar es Salaam, kikitokea Cairo Misri ilipoenda kuvaana na Al Ahly na kuupiga mpira mwingi uliowakosha wadau wa soka nchini waliodai soka hilo linaasharia benchi la timu hiyo chini ya Didier Gomes limeshapata dawa ya kufanya vyema katika robo fainali.

Simba ilipoteza bao 1-0, lakini soka ililolipiga limewakuna wengi, huku Kocha Gomes mara baada ya kutua jana mchana aluisema hesabu zake zilienda sivyo ndivyo na kuumizwa na matokeo hayo, lakini anajipanga ili kumaliza mambo mechi za robo fainali.

Simba imemaliza kama vinara wa Kundi A katika Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa na pointi 13, mbili zaidi na ilizonazo Al Ahly ambao ni watetezi

“Nashukuru kwa kuongoza kundi, ila lengo lilikuwa kushinda Cairo, lakini kwa vile tuna kazi kubwa mbele yetu, hatupaswi kuendelea kuumia badala yake tunajiweka sawa kwa mapambano yajayo,” alisema Gomes na kuongeza

“Pamoja na ugumu wa michuano ya CAF, tutapambana tupate matokeo mazuri katika robo fainali, kila kitu kinawezekana muhimu ni kufanya maandalizi mapema.”

Gomes alisema hana wasiwasi na kikosi chake katika kutimizia malengo yao CAF.

Wakati Gomes akiyasema hayo jana, baadhi ya wadau wa soka wamesema licha ya kupoteza bao 1-0 katika mechi hiyo ya mwisho ya makundi, Simba ilicheza kwa nidhamu kubwa na kimbinu na safu yake ya ulinzi ilionyesha uimara wa kukabiliana na mastraika hatari, pia walitengeneza nafasi kadhaa za mabao ambazo kama zingetumiwa huenda ingepata ushindi ugenini.

Wakizungumza na Mwanaspoti jana baadhi ya wadau wakiwamo makocha walisema mechi ya juzi ilikuwa ni kipimo tosha kuwa Gomes na benchi lake la ufundi na Simba kiujumla ina uwezo wa kupenya robo fainali na kufika mbali katika mashindano hayo ya Afrika.

“Kwa jinsi nilivyoona ikicheza dhidi ya Al Ahly, niwapongeze Simba kwani walikuwa wazuri ila walikosa tu bahati na utulivu walipolisogelea lango la wenyeji. Inawezekana kasi yao ilipungua kwa vile imeshafuzu, kama wangekuwa kuna kitu wanakihitaji ingekuwa moto zaidi,” alisema Mrage Kabange, nyota wa zamani wa klabu hiyo ambaye kwasasa ni kocha, aliyeongeza;

“Naiona Simba ikifika mbali, kwani ukiondoa Mamelodi Sundowns na Wydad Casablanca zinazoonekana bora zaidi, ila zilizobaki zinalingana au kuzidiwa uwezo na Simba na kuna uwezekano wa kushinda dhidi yao kufuzu nusu fainali.”

Naye kocha wa Simba Queens, Mussa Mgosi alisema Simba ya msimu huu ni tofauti na miaka ya nyuma na inaonekana ipo tayari kushindana na timu kubwa Afrika. “Timu inaendelea kuimarika na inaelekea kutimiza malengo iliyojiwekea kwani mwanzoni ilikuwa ni robo fainali, ila kwa sasa inaonekana wazi inataka kusogea zaidi ya hapo,” alisema nahodha huyo wa zamani wa Simba.

Mchambuzi wa michezo, Geoffrey Lea alisema jambo kubwa linaloleta matumaini kwa Simba kufanya vyema ni nidhamu ya kimbinu ambazo wamekuwa wakionyesha chini ya Gomes hasa katika mchezo wa juzi.

“Mimi ni muoga sana wa mechi za mtoano, sijajua Simba wataingia na mpango gani ila lazima wabadilike. Nawapa 50 kwa 50 kutinga nusu fainali,” alisema.

Simba imemaliza mechi za Kundi A ikiwa kinara ikikusanya pointi 13, mbili zaidi na ilizonazo Al Ahly na sasa inasubiria droo ya robo fainali itakayofanyika Aprili 30 kujua itacheza nani.

Timu hiyo sasa inarudi kwenye Ligi Kuu Bara kwa kuvaana na Mtibwa Sugar katika mechi ya kiporo itakayochezwa Jumatano jijini Dar es Salaam, wapinzani wao wakiwa na kazi kubwa mbele ya jeshi hilo la Gomes. Mtibwa ipo ovyo msimu huu na juzi usiku ilinyooshwa na Azam FC jijini Dar es Salaam kwa mabao 2-0 na kuwapa nafasi Wauza Lambalamba kuiengua Simba katika nafasi ya pili kwa kufikisha pointi 47, moja zaidi na ilizonazo Simba.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz