Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba hii iliwahi kupewa kipigo cha mabao 6

Simba Dms Simba hii iliwahi kupewa kipigo cha mabao 6

Tue, 1 Aug 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Historia ipo kwa ajili ya kukumbushwa kila kilichotokea miaka ya nyuma.

Lakini watu wengi hawataki kukumbushwa historia mbaya walizokutana nazo katika maisha yao.

Zipo historia nyingi za timu moja kubwa kufungwa maboa mengi zaidi na kuwashangaza mashabiki wa soka.

Simba imekuwa ikijivunia historia ya takribani miaka 46 ya kuwafunga watani zao Yanga mabao 6-0 mwaka 1977 katika Uwanja wa Taifa (sasa Uwanja wa Uhuru).

Hiki kilikuwa kichapo cha kulipa kisasi baada ya mwaka 1968, Yanga kuifunga Simba 5-0 katika Uwanja wa Karume jijini Dar es salaam.

Lakini kuna historia ambazo watu wengi hawazikumbuki na wala habari zake huwezi kuzipata kwenye vijiwe vya soka, labda kwa wachezaji husika walishiriki kucheza mchezo huu au kwenye ukurasa huu.

Bahati mbaya zaidi wachezaji wachache tu walioshiriki michezo kama hii ndio waliokuwa na bahati ya kuwa hai hadi leo.

KWANINI HAIZUNGUZWI?

Tukio hili ni kama vile halipo au halijawahi kutokea katika historia za soka ya Ligi ya Tanzania.

Au labda kwasababu Klabu ya CDA ya Dodoma haipo tena katika ushindani wa Ligi Kuu Tanzania, labda ndio maana historia haikumbushwi.

Au labda kwasababu CDA sio klabu kubwa kama zilivyo Simba na Yanga.

Acha tujikumbushe, miaka 41 iliyopita Simba iliwahi kuchezea kichapo cha nguvu cha mabao 6-1 na timu ya CDA ‘Watoto wa Nyumbani’ katika Ligi Daraja la Kwanza.

Ilikuwa ni Machi 31, 1982 Simba ilipokea kichapo cha aibu katika mchezo wa Kituo cha Mwanza. Mchezo huo ulichezwa wiki moja baada ya mchezo wa awali Simba kuifunga CDA mabao 3-2.

Katika ushindi huo mnono uliisaidia CDA kukusanya pointi tisa, mabao 16 na kufungwa matano na kushika nafasi ya kwanza katika kituo hicho.

Simba ilitoka katika kituo hicho ikiwa ya pili ikiwa na pointi tisa, mabao 21 na kufungwa mabao 10 na kuzifanya timu hiyo kuingia hatua ya pili.

KALAMU YA MABAO

Mashabiki wa Mji wa Mwanza (sasa jiji) walishudia mabao hayo wakiwa hawaamini macho yao baada ya Omari Mgeni kufunga bao la kwanza katika dakika ya tatu ya mchezo.

Mgeni alipokea pasi kutoka kwa winga wa kushoto, Justine Simfukwe ( sasa anatumia jina la Nelson Mawazo) na kuandika bao hilo.

Abbas Mtuli alifunga bao la pili katika dakika ya nane baada ya kupokea pasi kutoka kwa George Mutafungwa.

Kama haitoshi, Adolf Kondo alifunga bao kwa kichwa kufuatia kona ya Simfukwe iliyopanguliwa na kipa Peter Paul na kumkuta Omari Mgeni aliyetoa asisti kwa mfungaji.

SIMBA YABADILI KIPA

Baada ya mabao hayo ya haraka haraka, Simba ilimtoa kipa Paul na kumwingiza James Kisaka kuchukua nafasi yake.

Hata hivyo, hiyo haikuwa dawa, kwani katika dakika 23, Mtuli alipachika bao la nne.

Kipindi cha pili Mtuli tena alifunga bao la tano na kuwafanya mabeki ya Simba kuanza kulaumiana.

Simba ilijitutumua na kupata bao lililofungwa na George Kulagwa ‘George Best’ dakika ya 71

Winga mfupi aliyekuwa na machachari, Eric Sagala alihitimisha kalamu ya mabao baada ya kufunga bao la sita dakika ya 77.

SIMBA YACHOTA WACHEZAJI CDA

Mchezo huu kwa njia moja ama nyingine uliwafanya baadhi ya wachezaji kutakiwa na Simba.

Simba ilifanya juu chini na kuwachukua, Eric Sagala, Adolph Kondo na Lilla Shomari.

VIKOSI VILIVYOCHEZA

CDA DODOMA:

Enzi hizo, kikosi cha Watoto wa Nyumbani kiliundwa na kipa Peter Poka, Yussuf Ambwene, Suleimani Abeid, Charles Suleiman (Eric Sagala) na Kakimu Byemba.

Wengine ni Charles Mgodo, Omari Mgeni, Adolf Kondo, Abbas Mtuli, George Mutafungwa na Justine Simfukwe/ Lilla Shomari.

SIMBA:

Kipa Peter Paul/ James Kisaka, Kihwelo Mussa, Mohammed Kajole, Filbert Lubibira, Mwinyi Kidekeo, Nico Njohole, George Kulagwa, Amri Ibrahim, Robert Masanja, Abdallah Mwinyimkuu na Mrage Kabange.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live