Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba hawajui tatizo ni nini

FDNKk2BWEAAr8TB Mabingwa watetezi, Wekundu wa Msimbazi Simba SC

Wed, 3 Nov 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Sare tasa na Coastal Union nyumbani kwenye Uwanja wa Mkapa juzi, imeifanya Simba ijikute nyuma ya vinara wa Ligi Kuu, Yanga kwa pointi nne.

Ni matokeo magumu kuyapokea kwa mashabiki wa Simba ambao timu yao inatetea ubingwa kwani sio tu yanawapa faida kubwa washindani wao katika mbio za ubingwa, Yanga, bali pia yaliendana na kiwango kisichoridhisha hasa katika kipindi cha kwanza.

Pamoja na kutengeneza nafasi nyingi, Simba waliokosa utulivu eneo la timu pinzani na hilo liliwafanya wapoteze idadi kubwa ya nafasi za mabao hasa dakika 45 za pili pia benchi la ufundi lilionekana kukosa usimamizi mzuri kiasi cha kufanya nyakati kadhaa hadi wachezaji kunyanyuka na kutoa maelekezo kwa timu jambo ambalo ni kinyume na majukumu.

Namna ambavyo Simba walicheza imedhihirisha timu hiyo kwa sasa inahitaji kupata mapema kocha mkuu ambaye atafanyia kazi matatizo yaliyopo hasa ubutu wa ushambuliaji, staili ya uchezaji na nidhamu ya timu ili irejee mstarini ukizingatia ina ratiba ngumu ya mashindano ya ndani na yale ya kimataifa

COASTAL WALIVUJA JASHO

Haikuwa kazi rahisi kwa Coastal kupata matokeo ya sare na walilazimika kufanya kazi ya ziada katika dakika zote 90 za mchezo.

Timu hiyo ilicheza kwa nidhamu kubwa ikionekana kuwapa heshima Simba, walicheza kwa kujituma na kukimbia umbali mrefu ndani ya uwanja kusaka mpira pindi ulipokuwa kwa Simba na kushambulia kwa haraka kila walipoupata.Safu yao ya ulinzi ilicheza kwa utulivu na umakini wa hali ya juu na iliweza kukabiliana na presha ya mashambulizi ya mara kwa mara yaliyolekezwa kwao a kipindi cha pili na nyota wa Simba

KADI NYEKUNDU

Mwamuzi Rafael Ikambi alifanya uamuzi sahihi kuwatoa nje kwa kadi nyekundu wachezaji Benedictor Mwamlangala wa Coastal Union na Enock Inonga wa Simba.

Zilikuwa ni kadi nyekundu halali ambazo kila mchezaji alijitakia kutokana na mazingira na uhalisia wa makosa.

Akifahamu wazi kuwa tayari ana kadi ya njano, Mwamlangala alifanya kosa la kuchelewesha muda kwa kupiga mpira nje wakati tayari Inonga akiwa ameshautenga kuuanzisha.

Lakini Inonga baadaye alifanya kosa la kipuuzi kumpiga kichwa Issah Abushehe tukio ambalo lilimfanya aonyeshwe nye-kundu ya moja kwa moja.

SIMBA HAWAKUNUFAIKA

Mara kadhaa wachezaji wa Simba walitoa nje mpira pindi wachezaji wa Coastal Union walipoumia au refa alisimamisha mchezo wakati mpira ulipomilikiwa na Simba ili kuwezesha wachezaji wa Coastal walioumia kutibiwa.

Katika hali ya kushangaza, refa Ikambi alianzisha mpira kwa kuwapa Coastal ambao nao hawakuucheza kwa kuwapa Simba ambao awali unasimamishwa ndio walikuwa wanaumiliki.

Haikuwa sawa na jambo la kushangaza, mwamuzi ambaye ndiye alitakiwa awe mfano bora wa dhana ya uungwana ndiye alikuwa wa kwanza kuivunja.

COASTAL WAANDAE MRITHI WA AKPANI

Kiungo Victor Akpani alikuwa mhimili imara wa Coastal Union katikati mwa uwanja kutokana na jinsi alivyohaha kuziba mianya kwa Simba kupenyeza mpira kuingia eneo lao, kuichezesha timu na kuituliza. Alionyesha hali ya kujiamini na ni wazi kwamba anaweza kuwa lulu dirisha lijalo la usajili.

MAKOCHA WAFUNGUKA

Kocha wa Coastal Union, Melis Medo alisema: “Unapocheza na Simba unatakiwa uwe umeandaliwa vyema kimwili, kiakili na kimbinu hivyo tulijipanga kwa hilo na nafurahi kuona wachezaji wangu wamefanyia vyema na tumepata ponti.”

Upande wa Simba, kocha wa Simba, Selemani Matola alisema: “Mechi haikuwa mbaya, ilikuwa nzuri. Hatukucheza vizuri kipindi cha kwanza, lakini cha pili tumetengenza nafasi ila mwisho wa siku tumepata pointi moja, siku nyingine tunakosa bahati tu. Tumepata nafasi lakini hatukuzitumia. Umaliziaji wetu haukuwa mzuri,”

Chanzo: www.tanzaniaweb.live