BAADA ya mchezo wao dhidi ya Yanga kushindwa kufanyika, Kocha Msaidizi wa Simba, Suleiman Matola amesema hasira zote wanazihamishia kwenye mchezo ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Coastal Union kesho saa 1:00 jioni kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Simba itaingia katika mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya kuondoka na ushindi wa mabao 7-0 dhidi ya timu hiyo mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo.
Akizungumza na gazeti hili jana, Matola alisema hasira zote wanazihamishia kwenye michezo ya Ligi Kuu na hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini mwishoni mwa wiki hii.
“Mipango yetu na Yanga imeishia hapa, sasa tunaangalia mchezo wetu dhidi ya Coastal Union ambao tutakuwa nyumbani, kila kitu tulichopanga kimeenda kama tulivyopanga sasa ni wakati wa kuangalia Ligi Kuu pamoja na michuano mingine, malengo yetu ni kutetea mataji yetu.”
“Hesabu zetu zimeharibika tulitaka kuongeza wingi wa pointi baina yetu na anayetufuatia, tunarudi nyumbani tena kuwakabili Coastal Union, kikubwa mashabiki waendelee kujitokeza kwa wingi uwanjani kutupa sapoti ili tufanikishe malengo yetu,” alisema Matola.
Simba ipo kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 61, imeshuka uwanjani mara 25 na kushinda michezo 19, sare nne, huku ikiwa imepoteza michezo miwili na kufunga mabao 58 na kufungwa 10 katika ligi hiyo inayoshirikisha timu 18.