Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba hapo sawa

36b15f9bb733bacd32fae6b783a0fd36.jpeg Simba hapo sawa

Wed, 17 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

VINARA wa kundi A katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika Simba wameendeleza wimbi la ushindi na kutanua wigo kileleni mwa msimamo kwa kujikusanyia pointi 10 baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Al Merrikh ya Sudan kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa jana.

Mchezo huo wa nne wa mzunguko wa pili Simba ilianza kupata mabao yao katika dakika ya 17 kupitia kwa Luis Miquissone ambaye alitumia vyema pasi ya Clatous Chama na kuwapa uongozi.

Bao hilo liliendelea kuwapa presha Merrikh ambapo katika dakika ya 29 nahodha wake Monged alioneshwa kadi ya njano baada ya kumtolea lugha mbaya mwamuzi. Simba iliendelea kuliandama kama nyuki lango la Merrikh ambapo katika dakika ya 30 nusura waandike bao la pili baada ya Chris Mugalu kushindwa kutumia vyema pasi ya Benard Morrison.

Simba iliendelea kuliandama lango la Merrikh, ambapo iliwachukua dakika 21 kuandika bao la pili kupitia kwa nahodha Mohamed Hussein ambaye alifunga kwa shuti kali akimalizia kazi nzuri ya Morrison.

Wekundu wa Msimbazi walipata pigo katika dakika ya 42 kwa mlinzi wake kisiki Joash Onyango, kushindwa kuendelea na mchezo baada ya kupata majeraha hivyo nafasi yake kuchukuliwa na Erasto Nyoni.

Licha ya kuongoza kwa mabao hayo Simba iliendelea kuliandama lango la Merrikh lakini hadi dakika 45 zina tamatika Simba walikuwa mbele kwa mabao 2-0. Kipindi cha pili kilianza kwa kila timu kufanya mabadiliko Simba wakimtoa Muzamiru Yassin na kumuingiza Rally Bwalya nao Merrikh walimtoa Al Basheed Mohamed na kumuingiza Yousif Mohammed.

Mabadiliko hayo yaliongeza chachu katika safu ya kiungo ya Simba ambapo katika dakika ya 48 Simba iliongeza bao la tatu kupitia kwa Chris Mugalu aliyemalizia kwa shuti kali krosi ya Luis Miquissone.

Baada ya bao hilo Simba iliendelea kuliandama lango la Merrikh na kuwafanya wageni kupata wakati mgumu na kujikuta wakifanya makosa kwa kufanya madhambi ambapo dakika ya 64 Wagdi alijikuta akioneshwa kadi ya njano baada ya kumfanyia madhambi Thadeo Lwanga.

Licha ya kuandamwa kama nyuki Merrikh, walijibu mapigo katika lango la Simba katika dakika ya 81 kupitia kwa Mattocks ambaye alikuwa yeye na Aishi Manula lakini shuti lake liliishia katika mikono ya kipa huyo.

Baada ya kukosa bao hilo Merrikh wakaongeza nguvu ambapo katika dakika ya 84 mshambuliaji Terry alishindwa kuipatia bao la kufutia machozi timu yake baada ya mpira wake kwenda nje. Simba walirejea tena katika lango la Merrikh kwa nguvu lakini ukosefu wa umakini uliwanyima bao la nne baada ya Chama kukosa bao la wazi baada ya kumpiga chenga mlinda mlango wa Merrikh, Monged.

Hadi mwamuzi anapuliza kipyenga cha kumaliza pambano Simba inaendeleza wimbi la ushindi katika uwanja wa Benjamin Mkapa, kwa matokeo hayo Simba anaendelea kusalia kileleni huku akifuatiwa na Al Ahly mwenye alama saba. Ahly iliifunga AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo mabao 3-0.

Vikosi vilivyoanza Simba, Aishi Manula, Shomary Kapombe, Mohamed Hussein, Kennedy Juma, Joash Onyango/ Erasto Nyoni dk 42, Thadeo Lwanga, Benard Morrison/ Jonas Mkude dk 71, Mzamiru Yassin/ Rally Bwalya dk 46, Chris Mugalu/ Meddie Kagere dk 71, Clatous Chama na Luis Miquessone/ Francis Kahata dk 82.

Chanzo: www.habarileo.co.tz