Kikosi cha Simba SC baadae leo Ijumaa (Januari 13) kitacheza mchezo wa Kimataifa wa Kirafiki mjini Abu Dhabi dhidi ya Dhafra FC inayoshiriki Ligi Kuu ya Falme za Kirabu ‘UAE Pro League’.
Simba SC itautumia mchezo huo kama sehemu ya maandalizi ya kuendelea na Mshike Mshike wa Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na Ligi ya Mabingwa Barani Afrika Hatua ya Makundi.
Meneja wa Habari na Mawasilino wa Simba SC Ahmed Ally amesema kikosi chao kipo tayari kwa mchezo huo, ambao utakua wa kwanza kwa Kocha wao kutoka nchini Brazil Robertinho.
Ahmed amesema lengo la mchezo huo sio kupata matokeo mazuri ama mabaya, zaidi ya Kocha Mkuu Robertinho na wasaidizi wake kupima uwezo wa wachezaji waliopo Kambini kwa sasa.
Amekiri kuwa timu ya Dhafra FC haina uzito mkubwa katika Ligi Kuu ya UAE, lakini hilo haliwapi tatizo kwani wanajua wanachohitaji kupitia mchezo huo, ambao utaanza saa kumi na moja kwa saa za Tanzania.
“Leo Januari 13 2023 tutakuwa na Mchezo wa kirafiki dhidi ya klab ya Al Dhafroah ianyoshirki ligi kuu (Falme za kiarabu),”
“Tunafahamu Sio klabu kubwa sana na yenye Ubora mzuri na hata matokeo bora kwa maana ukiangalia kwenye msimamo wa ligi yao (nafasi ya 11) Ila lengo lengo ni Mwalimu aone Wachezaji wake na apate kikosi chake” amesema Ahmed Ally
Simba SC inatarajia kucheza mchezo mwingine wa Kimataifa wa Kirafiki dhidi ya Mabingwa wa zamani wa UEFA Europa League CSKA Moscow ya Urusi, Jumapili (Januari 15).