Huwezi kuamini, lakini ndio ukweli kwamba, Simba imetimiza dakika 630 bila kupata ushindi kwenye michuano ya kimataifa, kitu ambacho hakijawahi kutokea kwa timu hiyo.
Juzi usiku Simba ilipasuka bao 1-0 mbele ya Wydad Casablanca katika mechi ya raundi ya tatu ya Ligi ya Mabingwa Afrika mjini Marrakech, Morocco na kuifanya itimize jumla ya siku 232 tangu iliposhinda mara ya mwisho kwenye michuano ya kimataifa.
Simba ilishinda mara ya mwisho kwenye michuano ya kimataifa Aprili 22, mwaka huu kwenye mchezo wa robo fainali ilipoitungua Wydad kwa bao 1-0 mchezo uliopigwa Kwa Mkapa, Dar es Salaam kabla ya kwenda kurudiana nao ugenini na kufungwa 1-0 kisha kutolewa michuanoni kwa njia ya mikwaju ya penalti.
Hata hivyo msimu mpya wa michuano ya CAF ilipoanza Simba imeshacheza jumla ya mechi saba, ikiwamo mitano ya Ligi ya Mabingwa na mingine miwili ya African Football League (AFL) bila kuibuka na ushindi.
Ilianza mechi mbili za raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Power Dynamos ya Zambia ambazo zote ziliisha kwa sare, ikianza 2-2 ya ugenini kisha kutoka 1-1 ziliporudiana Dar es Salaam na kutinga makundi kwa kanuni ya faida ya bao la ugenini.
Baada ya hapo ikahamia kwenye AFL ikapangiwa kukutana na Ah Ahly ya Misri, ikatoka nao sare ya 2-2 katika mechi kali iliyopigwa Kwa Mkapa kabla ya kurudiana nao siku chache baadae na kuambulia sare ya 1-1 na kuwavusha Wamisri hadi nusu fainali kwa kanuni ya mabao ya ugenini.
Mwezi uliopita, Simba ikarudi kwenye mechi za makundi ikikakutana na Asec Mimosas ya Ivory Coast na kutoka sare ya 1-1, kutokana na bao la penalti la Saido Ntibazonkiza, likiwa ndilo bao pekee lililofungwa na timu hiyo hadi sasa kwenye hatua hiyo, licha ya kucheza mechi tatu ikiwa Kundi B.
Mapema wiki iliyopita ililazimishwa suluhu ugenini na Jwaneng Galaxy ya Botswana kabla ya juzi kulala kwa Wydad na kuifanya timu hiyo kuandika rekodi mbaya kwenye anga la kimataifa ambayo haijawahi kutoka kwao licha ya kuupiga mwingi mjini Marrakech.
Kwa sasa timu hiyo inayonolewa na Kocha Abdelhak Benchikha ina dakika 270 za kurekebisha dosari hiyo, wakati ikimalizia mechi za makundi ikiwamo ile ya marudiano dhidi ya Wydad itakayopigwa Desemba 19 kabla ya kumalizia mechi mbili za kundi hilo mapema mwakani.
Simba itaanza kwa kuifuata Asec jijini Abidjan, Ivory Coast Februari 23 mwakani kisha wiki moja baadae itaialika Jwaneng Galaxy kumalizana nao Kwa Mkapa mechi zitakazoamua safari ya Mnyama kwenda robo fainali au kung’oka kuwapisha wapinzani alioanao kundini kusonga mbele.
Kwa misimu mitano mfululizo iliyopita, Simba imefanikiwa kutinga hatua ya robo fainali nne tofauti zikiwamo tatu za Ligi ya Mabingwa 2018-2019, 2020-2021 na 2022-2023 pamoja na ile ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2021-2022.
Mapema kocha wa timu hiyo, Benchikha aliyetwaa Kombe la Shirikisho na CAF Super Cup kwa msimu uliopita akiwa na USM Alger ya Algeria, alikaririwa na Mwanaspoti, akisema akili yake ni kuvuka makundi kwa sasa ili kukuipa mafanikio, kabla ya kugeukia vita ya Ligi na ASFC.