Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba baba lao miaka 5 ya Magufuli

JPMSIMBAA Simba baba lao miaka 5 ya Magufuli

Sat, 20 Mar 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

KUNA mengi yaliyotokea katika michezo hasa soka katika kipindi cha miaka madarakani cha Rais John Magufuli aliyefariki dunia Machi 17, mwaka huu.

Huku taifa likiwa katika siku 14 za maombolezo, tunakuletea klabu iliyofanikiwa zaidi katika kipindi hicho.

Simba ndiyo iliyokuwa na mafanikio makubwa zaidi ukilinganisha na klabu nyingine za soka nchini ikitwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara tatu mfululizo na kufikia hatua ya robo-fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

UBINGWA WA FA

Simba baada ya kukaa muda mrefu bila ya kuchukua taji lolote la Ligi Kuu Bara na mashindano mengine walikuja kuibuka katika mwaka wa pili tangu Magufuli aingine madarakani akichukua nafasi hiyo kutoka kwa Rais mstaafu, Jakaya Kikwete.

Simba wakati huo walikuwa wakiitwa majina mengi ya utani kwa kushindwa kuchukua mataji kama ‘Wa Mchangani’, ‘Wa Matopeni’ na kadhalika, walianza utawala wao wa sasa wa soka nchini kwa kutwaa Kombe la Shirikisho (FA) Mei 27, 2017.

Waliifunga Mbao FC mabao 2-1 katika fainali kwenye Uwanja wa Jamhuri Dodoma.

Kombe hilo lenye thamani ya Sh50 milioni liliwapa nafasi ya kwenda kucheza Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kutoshiriki mashindano ya kimataifa kwa muda mrefu.

MAKOMBE MATATU

Katika kipindi cha Magufuli, Simba wameonekana kuwa na mafanikio makubwa zaidi katika Ligi Kuu Bara baada ya kutwaa taji hilo mara tatu mfululizo.

Simba ndani ya utawala wa Magufuli walitwaa ubingwa wa ligi msimu wa 2017-18, wakifikisha pointi pointi 69, msimu wa 2018-19 pointi 93 na msimu uliopita 2019-20, walimaliza na pointi 88. Hadi anafariki dunia, Simba inaonekana kuwa na nafasi kubwa zaidi ya kutwaa ubingwa huo wa Bara kwa msimu wa nne mfululizo.

Katika kipindi hicho cha Magufuli, Yanga imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara mbili 2015-16 na 2016-17.

NGAO YA JAMII

Ndani ya miaka sita ya Magufuli, Simba wametwaa Ngao ya Jamii kwa miaka minne mfululizo.

Simba wametwaa kombe hilo katika miaka ya 2017, 2018, 2019 na msimu uliopita 2020, ambao waliwafunga Namungo FC mabao 2-0 katika mechi iliyochezwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Arusha. Katika kipindi cha Magufuli, Yanga wametwaa Ngao ya Jamii mara moja 2015 na Azam moja 2016.

KOMBE LA MAPINDUZI

Katika utawala wa Magufuli, Simba wamecheza fainali tatu katika Kombe la Mapinduzi ambalo hufanyika huko visiwani Zanzibar lakini hawajatwaa hata mara moja.

Fainali hizo tatu ambazo Simba wamecheza zilikuwa 2017, 2019 na msimu huu 2021 dhidi ya Yanga ambazo zote walipoteza na kuwa washindi wa pili. Azam FC wametawala katika kipindi hicho wakilitwaa mara tatu, Mtibwa mara moja na Yanga mara moja.

KOMBE LA CECAFA

Katika utawala wa Magufuli Simba waliingia fainali michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kagame Cup) mwaka 2018 na kumaliza katika nafasi ya pili baada ya kupoteza 2-1 dhidi ya Azam FC katika fainali. Azam imetawala pia ikilitwaa taji hilo mara mbili 2015 na 2018.

SPORTPESA

Juni 10, 2018 Simba walimaliza nafasi ya pili katika Kombe la SportPesa baada ya kufungwa mechi ya fainali mabao 2-0, dhidi ya Gor Mahia kutokea Kenya.

Katika mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa Afraha Nakuru mabao ya Gor Mahia yalifungwa na Meddie Kagere (dakika 6) ambaye Simba mara baada ya mashindano hayo kumaliza walimsajili, huku bao jingine likifungwa na Jacques Tuyisenge dakika 55.

LIGI YA MABINGWA AFRIKA

Katika Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba kwenye utawala wa Magufuli mafanikio makubwa ambayo waliyafikia ni kufika robo fainali ya mashindano hayo makubwa katika ngazi ya klabu.

Msimu wa 2018–19, Simba walifika robo fainali na waliondolewa na miamba ya soka la Afrika TP Mazembe kwa idadi ya mabao 4-1. Msimu uliopita mambo kwa Simba hayakuwa mazuri ila awamu hii kwa sasa wanakaribia mafanikio yao ya msimu 2018-19, kwani wapo katika hatua ya makundi na wana nafasi ya kufuzu robo fainali.

Kikosi hicho cha Simba katika utawala huu wa Magufuli wamevuna pointi katika uwanja wake wa nyumbani dhidi ya timu ngumu za Afrika kama Al Ahly ambao wamewafunga mara mbili, AS Vita, JS Saoura na nyingine.

UONGOZI SIMBA

Uongozi wa Simba kupitia katika ukurasa wake wa mitandao ya kijamii uliandika ujumbe wenye salamu za pole.

Taarifa hiyo ilieleza: “Uongozi wa klabu ya Simba umepokea kwa mshtuko mkubwa taarifa za kifo cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli ambacho kimetokea jana (juzi) Jumatano Machi17, kwenye Hospitali ya Mzena iliyopo jijini Dar es Salaam”.

“Katika kipindi hiki ambacho Watanzania bado tupo kwenye huzuni kubwa ya kumpoteza kiongozi wetu kitaifa, tunawaomba watu wote tuendelee kumuombea kwa Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahala pema peponi”.

Taarifa hiyo iliongeza kwa kusema “Tunatoa pole kwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu, Familia, Ndugu, jamaa na watu wote ambao wameguswa na msiba huu mzito.

MANAHODHA SIMBA WAMLILIA

Nahodha Mkuu wa Simba, John Bocco aliandika katika ukurasa wake wa Instagram: “Kweli kizuri hakidumu. RIP mzalendo wa kweli, Mtanzania uliyeiweka Tanzania mbele na sio ubinafsi, naamini wa kujifunza tumejifunza mengi sana kutoka kwako na wa kuona tumeona mengi sana mazuri kutoka kwako. R.I.P Mr President wewe ni zaidi ya somo kwa Watanzania”.

Naye Nahodha msaidizi wa timu hiyo, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ aliandika: “Rais wangu, Rais wetu, Ahsante kwa kulipenda Taifa letu, Ahsante kwa kuwatetea maskini na wanyonge. Legends dont die, they sleep. R.I.P President.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz