Pambano la soka la watani wa jadi, Simba na Yanga limeinufaisha Bodi ya Ligi (TPLB) kuvuna maokoto ya maana kutokana na makosa yaliyofanywa na klabu hizo kupitia wachezaji na maofisa wao kwenye mchezo huo uliopigwa Novemba 5 mwaka huu na Yanga kushinda kwa mabao 5-1.
Bodi ya Ligi imezitoza faini klabu hizo mbili Sh 8 Milioni kwa makosa yaliyofanyika kwenye mchezo huo wa Ligi Kuu Bara uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, mbali na kujizolea kiasi kingine kama hicho kwa adhabu mbalimbali ilizotoa kwa klabu nyingine kuanzia za Ligi Kuu, Ligi ya Champioship hadi First League.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyotelewa leo Ijumaa mchana, Yanga imelimwa faini ya Sh 5 Milioni kwa kosa la kuingia uwanjani kupitia mlango usio rasmi kwenye mchezo huo, adhabu hiyo imetolewa sawa na kanuni ya 17:(21,60) ya Ligi Kuu kuhusu taratibu za mchezo.
Kwa upande wa Simba imetozwa faini ya Sh 1 Milioni kwa kosa la wachezaji wake kuchelewa kutoka katika vyumba vya kubadilishia nguo na kuufanya mchezo kuchelewa dakika nne, hivyo kuharibu utaratibu wa mrusha matangazo, adhabu hiyo imetolewa kuzingatia kanuni 17:60 ya Ligi Kuu.
Kwa hesabu hizo ni kama vile bodi imetoa adhabu kulingana na idadi ya mabao iliyofunga timu hizo kwenye pambano hilo, kwani Yanga ilishinda mabao matano wakati watani wao wa Simba ilifunga moja.
Mbali na faini hizo kwa klabu hizo kongwe, lakini nyota wao nao walikumbana na rungu hilo la bodi akiwamo Kibu Denis aliyelimwa faini ya Sh. 500,000 baada ya kushangilia mbele ya mashabiki wa Yanga na kuonyesha ishara ya kuwafunga mdomo mara baada ya kufunga bao pekee katika mchezo huo kitendo kilichokinyume na taratibu za kimchezo, sawa na ilivyokuwa kwa beki wa timu hiyo ya Simba, Henock Inonga aliyelimwa pia kiwango hicho kwa kushangilia kama mwenzake.
Naye Kipa wa Yanga na Djigui Diarra, alikumbana na adhabu ya kulimwa Sh 500,000 kwa kwenda kushangilia mbele ya benchi la ufundi la Simba katika mchezo huo, huku kocha msaidizi wa timu hiyo, Moussa Ndao akalimwa pia Sh 500,000 kwa kuwatolea lugha ya matusi benchi la ufundi la klabu ya Simba.
Klabu nyingine zilizokumbana rungu la Bodi ni Lipuli iliyopimwa Sh 3 Milioni kwa kushindwa kwenda uwanjani kwenye mchezo wa First League dhidi ya Dar City, sawia na kupokwa pointi 15, huku KMC na Coastal Union kila moja ikitozwa faini ya Sh 1 Milioni kutokana kuvunja kanuni za ligi kwenye mechi dhidi ya Dodoma Jiji na Yanga mtawalia, huku kiungo wa Yanga Khalid Aucho akifungiwa mechi tatu na kulimwa Sh 500,000 na Mkurugenzi wa Ufundi wa Singida FG, Ramadhan Mswazurwimo akilimwa Sh 1 Milioni, makocha wa Mbeya City iliyopo Championship Salum Manyanga na Paul Nonga kila mmoja amelimwa Sh 500,000 kwenye mchezo wao na Biashara United, huku Stand United nayo ilimwa Sh 500,000 kwa kosa ililofanya kwenye mechi dhidi ya Mbeya Kwanza.
Mwamuzi Emmanuel Mwandembwa aliyecheza mechi ya Coastal Union na Yanga amefungiwa miezi sita, huku klabu ya Dar City ikipewa onyo.