Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba, Yanga zikafungue silaha CAF

Simba, Yanga Waanza Kuweka Viporo Mechi Za NBC Simba, Yanga zikafungue silaha CAF

Wed, 6 Dec 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Ukitazama mechi mbili za awali za Ligi ya Mabingwa Afrika, unagundua aliyekuwa mzima amekuwa mbovu na aliyekuwa mbovu amekuwa mbovu!

Ni muda wa mashabiki wa soka nchini kuwa na presha na kuishi kwa matumaini. Simba hata iwe mbovu vipi, linapokuja suala la michuano ya kimataifa huwa wanabadilika. Wanakuwa watu wengine tofauti.

Yanga pamoja na kutokuwa na historia nzuri sana kimataifa, lakini kwa sasa wana timu bora. Kitendo cha kuburuza mkia baada ya mechi mbili za awali kwenye makundi, ni aibu. Ni fedhea! hakuna shabiki yeyote wa soka aliliona hili mapema.

Ukitazama kundi alilopangwa Simba, uhakika wa nafasi mbili za juu ulikuwa mkubwa sana. Safari ya Mnyama kwenda kileleni inaonekana ilikuwa haina misukosuko.

Lakini ukitazama wanavyocheza, unaweza kusema wachezaji wamefungwa mawe! Ubabe wote wa Yanga kwenye Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita, huuoni msimu huu.

Ubabe wote wa Yanga kwenye ligi ya ndani, huwaoni wakifurukuta kimataifa. Je, unalielewa chama lako?

Ukiitazama Simba, kuna muda unaona ni vituko vitupu! Kwa Mkapa siku hizi watu wanatoka vizuri tu. Huu sio utamaduni wa Simba tuliouzoea.

Watu wangu wa Simba, mnaiona kweli timu ikitoboa msimu huu kwenda Robo Fainali?

Simba haijashinda hata mechi moja msimu huu za kimataifa. Hii sio Simba ninayoifahamu. Mnyama kimataifa ni uwanja wake wa nyumbani.

Amemfunga sana Al Ahly, As Vita. Mnyama ni wa kimataifa.

Kwenda sare dhidi ya Asec Mimosas na Jwaneng Galaxy, kuna namna inafikirisha! Simba wamekuwa Swala sasa!

Ule Ufalme wa Nyika ni kama umepotea msimu huu. Hawajiamini tena. Ukitazama matokeo yao ya mwisho dhidi ya Jwaneng Galaxy ndiyo utachoka kabisa! Simba alitawala kila kitu lakini siyo magoli. Alifanikiwa kwenye kila kitu lakini hakufunga.

Ukitazama mechi ya Asec Mimosas kwa Mkapa, utachoka kabisa. Wanaokuambia Simba ni mbovu, wanakudanganya! Simba wanaupiga mwingi lakini ushindi haupatikani!

Maisha ya Simba siku hizi ni sare utadhani wana sherehe! Hakuna timu imewahi kufika nusu fainali kwa kupata sare kila siku.

Sare dhidi ya Jwaneng Galaxy ni kama sare ya sita kwa Simba Kimataifa msimu huu. Walifuzu hatua ya makundi kwa sare mbili dhidi ya Power Dynamos. Wametolewa kwenye African Football League (AFL), dhidi ya Al Ahly kwa kupata sare zote na sasa, wako mechi ya pili Ligi ya Mabingwa Afrika na sare zote!

Sijawahi kuiona timu yoyote kutoka Tanzania kuifikia Yanga kwa kushinda mechi sita mfululizo za kimataifa ugenini.

Hao ni Yanga kabla ya kufungwa na CR Belouizdad Algeria. Nadhani Yanga walijiamini kupitiliza na washakuwa jeuri.

Kwa sasa wanaamini watamfunga yoyote, popote. Wamecheza mechi mbili mfululizo bila ushindi. Ni tofauti sana na matokeo yao ya msimu uliopita.

Pamoja na ubora mkubwa wa wachezaji wao, ni beki Yao kouassi, kiungo Khalid Aucho na mshambuliaji Pacome Zouzou ndio wamekuwa na mfululizo wa uchezaji mzuri. Aziz KI na Maxi Nzengeli sio mechi zote wanakupa kiwango kile kile.

Haya siyo aina ya matokeo ambayo Wanayanga waliyatarajia. Tayari presha imeanza kupanda kuelekea mzunguko wa tatu wa mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika.

Ni mechi ambayo Yanga anatakiwa kushinda. Matokeo tofauti na ushindi, itakuwa taratibu inajiaondoa kwenye mbio za robo fainali.

Yanga inakwama wapi kwenye mechi mbili zilizopita?

Kila mchezaji tegemezi ndani ya Yanga, yupo. Hakuna mchezaji anayeumwa na asiyepangwa. Staili walioingia nayo Yanga kwenye mchezo dhidi ya Al Ahly, ndiyo walipaswa kuitumia kwenye mchezo wao dhidi ya CR Belouizdad ugenini.

Yanga walipaswa kufunga njia zote na kulazimisha sare ugenini. Kuna namna matumaini yameanza kuyumba kwa wana Yanga.

Kila nikitazama msimamo wa Kundi la Yanga, nawaona wakiwa wa mwisho na pointi moja. Kila nikitazama msimu wa kundi la Simba, nawaona wako wa tatu na pointi mbili!

Haya siyo aina ya matokeo ambayo wapenzi wa timu hizi walitarajia! Ni mshangao mkubwa! Wale Jwaneng Galaxy walikuwa wanafungika kabisa!

Simba hana cha kujitetea katika hili. Unapotaka sare kwenye mechi ya kushinda unajiweka pabaya wewe mwenyewe! Walau Asec Memosas kwa mkapa walileta ushindani kidogo ingawa hata wao walitakiwa kuacha alama tatu kwa Mkapa.

Wamekutana tu na Simba aliyevurugwa! Wamekutana na Simba aliyechanganyikiwa! Kama wangecheza na Simba ‘yenyewe’, wangekufa mapema kwa Mkapa.

Bado naiona Yanga ikiwa timu bora Tanzania. Sasa ni muda wa kwenda kufungua kila silaha na kuanza kushinda.

Maxi, Aziz KI, Pacome na Mzize ni muda wa kwenda kuibebe timu.

Kwenye makaratasi timu zetu zote bado zina nafasi ya kusonga mbele, lakini ni lazima zishinde mechi zao mbili zinazofuata.

Hapa Kidogo matumaini yataimarishwa. Kwa Matokeo ya mechi mbili za kwanza, safari ya kutolewa wote ndiyo picha kubwa inayobaki kwa mashabiki.

Analiona chama lako likitoboa kwenda Robo Fainali? Niandikie ujumbe mfupi wa maandishi kupitia namba yangu ya simu hapo juu.

Chanzo: Mwanaspoti