Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba, Yanga zawekeana mitego hii, dabi ya kesho

Kibu Fgh Simba, Yanga zawekeana mitego hii, dabi ya kesho

Wed, 7 Aug 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kwa maandalizi ambayo yamefanywa na watani wa jadi. Kazi ipo kesho Kwa Mkapa. Simba na Yanga zitakutana kesho kufungua pazia la msimu ujao wa Ligi Kuu Bara 2024/25.

Mashabiki wa Simba walifurahia kikosi chao kipya kwenye Simba Day  chini kocha,Fadlu Davids raia wa Afrika Kusini kutokana na kandanda safi la kushambulia kwa kasi ambalo walitandaza dhidi ya APR ya Rwanda hasa katika kipindi cha pili huku wachezaji Joshua Mutale, Debora Fernandes Mavambo, Awesu Awesu na Edwin Balua wakiwa gumzo wakati timu hiyo ikiibuka na ushindi wa mabao 2-0.

Wananchi waliona vile ambavyo kocha wao, Miguel Gamondi anaweza kuwatumia wachezaji tofauti katika mipango yake ya kusaka matokeo na ndio maana katika mchezo dhidi ya Red Arrows ya Zambia aligawa vikosi viwili vilivyotumika kwenye vipindi tofauti wakati wakiibuka na ushindi wa mabao 2-1.

Hesabu zilizopo kwa sasa ni kwa namna gani timu hizo zitakabiliana kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii kulingana na maboresho ambavyo yamefanywa, Fadlu anavimbia kuwa na wachezaji vijana wenye njaa ya mafanikio huku Gamondi akifurahia upana wa kikosi chake hivyo amekuwa na machaguo zaidi ambayo yameonyesha kitu katika michezo yao ya kirafiki.

Mfano mzuri ni Duke Abuya na Prince Dube ambao wamenogesha eneo la kiungo na safu ya ushambuliaji ya timu hiyo. Kwa kuvitazama vikosi vya timu zote mbili, Yanga na Simba hizi ni bato ambazo zitakuwa na nafasi kubwa ya kuuamua mchezo huo kwenye uwanja wa Benjamini Mkapa.

Mtego wa Simba

Katika michezo minne ambayo Simba imecheza ya kirafiki tangu ilipoweka kambi ya wiki tatu huko Ismailia, Misri dhidi ya Al-Adalah (2-1), Telecom FC (2-1) na El Qanah FC (3-0) na mmoja wa Simba Day dhidi ya APR (2-1) imefunga jumla ya mabao tisa, mawili yamefungwa na Jean Charles Ahoua huku Augustine Okejepha, Valentino Mashaka, Ladack Chasambi, Steven Mukwala, Joshua Mutale, Edwin Balua na Fernandes wakifunga moja kila mmoja.

Katika michezo hiyo, Fadlu alikuwa akifanya machaguo tofauti ili kupata kikosi chake cha maangamizi jambo ambalo limemfanya kuwa na wachezaji tofauti hasa katika maeneo ya ushambuliaji wenye uwezo wa kutengeneza nafasi na kufunga.

Ubora ambao Simba wameonyesha eneo la ushambuliaji, kuanzia eneo la kiungo mchezeshaji hadi pembeni kwa mawinga ni wazi kwamba kutakuwa na vita dhidi ya ukuta wa Yanga ambao umeboreshwa kwa kusajiliwa kwa Chadrack Boka upande wa beki ya kushoto.

Katika namna ambavyo Fadlu ameonekana kukisuka kikosi chake  kuwa na staili tofauti za kushambulia, mfano mzuri ni namna walivyocheza katika mchezo wa Simba Day dhidi ya APR, ndani ya dakika 45 za kipindi cha kwanza, Mutale na Awesu walikuwa wakiongeza idadi ya viungo washambuliaji, walisogea eneo la wapinzani kwa kuingia ndani, Shomary Kapombe na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ ndio waliokuwa huru kushambulia maeneo ya pembeni.

Ukuta wa Yanga ambao unaongozwa na kipa, Djigui Diarra umeruhusu mabao matatu katika michezo minne iliyocheza ya kirafiki mawili dhidi ya FC Augsburg ya Ligi Kuu Ujerumani ‘Bundesliga’ na moja dhidi ya Red Arrows F.C.

Udhaifu ambao Yanga imeonakana kuwa nao katika ukuta wake, ni kuruhusu bao la kichwa dhidi ya Red Arrows huo ni ugonjwa ambao wamekuwa nao tangu msimu uliopita, huku mabao dhidi ya Augsburg ikiwa ni uzembe wa kushindwa kwa mabeki wake kukaa katika maeneo sahihi kiasi cha kuacha mianya wazi.

ni dhahiri kuwa eneo la Simba la ushambuliaji litakuwa na mawinga, Joshua Mutale, Awesu Awesu, viungo wa kati,Debora Fernandes,Jean Charles Ahoua na huku Steve Mukwala akisimama kama mshambuliaji wa mwisho. Moto wa Yanga

Hii ni vita nyingine kali kati ya safu ya ushambuliaji ya Yanga yenye mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita, Stephane Aziz Ki dhidi ya ukuta wa Simba wenye maboresho mawili yaliyofanywa katika dirisha hili la usajili, kipa kutoka Horoya ya Guinea, Moussa Camara na beki wa kati, Chamou Karaboue.

Ni wazi kuwa ukuta wa Simba ambao umeruhusu mabao mawili katika michezo yake ya kirafiki utakuwa na kazi kubwa ya kufanya kutokana na Yanga kuimarisha eneo lake la ushambuliaji kwa kuwaongeza kundini, Duke Abuya, Prince Dube, Jean Baleke na Clatous Chama ambaye anajitafuta.

Abuya na Dube wanaonekana tayari kuwaka na wanaweza kuiweka Simba katika wakati mgumu kutokana na kile walichokifanya katika michezo ya kirafiki kwa kushirikiana na Aziz Ki, Maxi Nzengeli, Pacome Zouzoua na Clement Mzize.

Safu ya ushambuliaji ya Yanga ilishtua Afrika Kusini kwa kuitandika Kaizer Chiefs  mabao 4-0 kwenye michuano ya Toyota, Aziz KI alifunga mara mbili, Dube na Mzize kila mmoja alicheka na nyavu.

Namna ambavyo Yanga imekuwa ikisaka matokeo imekuwa haitabiriki, inaweza kushambulia kupitia maeneo yake ya pembeni (winga ya kushoto na kulia) na hata kati ambako amekuwa akicheza Aziz Ki na wakati mwingine Mudathir Yahya.

Hivyo inaonekana safu yake ya ushambuliaji kesho itakuwa na mawinga, Max Nzengeli,Prince Dube, viungo wa kati, Duke Abuya, Aziz KI huku mshambuliaji wa kati akiwa Clement Mzize.

Wasikie wadau Nyota wa zamani wa Yanga, Sekilojo Chambua anaamini itakuwa mechi nzuri ambayo itaamuliwa na ubora wa safu kali zaidi ya ushambuliaji kutokana na timu zote mbili kufanya usajili ambao unaonekana kuwa tija.

Muda mwingine ni ngumu kuongelea dabi kwa sababu kile ambacho kipo vichwani mwetu huwa tofauti, lakini naona itakuwa mechi nzuri na ya kuvutia, Yanga na Simba zote zimekuwa na wakati mzuri katika maandalizi yao,” alisema na kuongeza;

“Yanga inaweza kuwa na wakati mzuri zaidi kwasababu imefanya maboresho madogo sana tofauti na Simba iliyosajili wachezaji wengi lakini hiyo sio sababu yao wakushindwa kupambania matokeo, wameonyesha wanakitu.”

Kwa upande wake, nyota wa zamani wa Simba, Zamoyoni Mogella alisema; “Hii ni mechi ambayo itatoa picha ya kile ambacho wamekifanya kwenye maandalizi yao, binafsi naamini itakuwa mechi nzuri ambayo ni ngumu kuitabiri.”

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: