Simba inakiwasha leo dhidi ya Raja Casablanca kabla ya kesho Yanga kutupa karata katika Kombe la Shirikisho Afrika kwa kuvaana na TP Mazembe na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo (Taswa) kimetoa baraka zao.
Taswa imewatakia kila la heri wawakilishi hao wa nchini, sambamba na wanariadha waliopo Australia kwenye Mbio za Nyika za Dunia zinazofanyika leo, huku kikiwapongeza Dk Pindi Chana kwa kuteuliwa Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo na Saidi Othman kuwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na kusainiwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Alfred Lucas, Taswa imezitakia Simba na Yanga mechi zenye mafanikio mbele ya wapinzani wao kwa kusahau matokeo ya michezo ya kwanza iliyopigwa ugenini nchini Tunisia na Guinea.
“Taswa inaamini Simba na Yanga zitafanya kile ambacho Watanzania wengi tunakitaka wakifanye, nacho ni kutupatia ushindi, hasa kwa vile watakuwa nyumbani Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam,” taarifa hiyo ya Taswa ilisomeka hivyo na kuongeza;
“Taswa inaamini zimejiandaa vya kutosha, zina kila sababu ya kupeperusha vyema bendera ya nchi, tunawasihi mashabiki wote tuziombee timu zetu, kila mmoja kwa imani yake, bila shaka mambo yatakuwa mazuri na hazitatuangusha.
“Pia tunaitakia mafanikio mazuri timu ya Taifa ya Riadha ambayo Jumamosi hii itapeperusha bendera ya taifa kwenye mashindano ya Dunia ya Mbio za Nyika (World Cross Country Championship) yanayofanyika nchini Australia.”
Timu hiyo ya Tanzania ya riadha iliyoagwa mapema wiki hii, inawakilishwa na wanariadha wanne, akiwamo nahodha Fabian Sulle, Josephat Joshua, Inyasui Sulley na Mathayo Sombi sambamba na kocha Dennis Malle