Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba, Yanga zateka Ligi Kuu Bara

Yanga Vs Simba FT Simba, Yanga zateka Ligi Kuu Bara

Thu, 12 Jan 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Ligi Kuu Bara kwa sasa imesimama kupisha michuano ya Kombe la Mapinduzi, lakini namba zinaonyesha hadi kusimama kwake ikiwa katika mzunguko wa 19, Simba na Yanga hazishikiki kwenye vipengele mbali mbali.

Timu hizo kongwe na zenye mashabiki wengi Tanzania ndiyo zinaongoza Ligi Kuu ambapo kileleni ipo Yanga yenye pointi 50, ikifuatiwa Simba yenye alama 44, huku Azam FC ikiwa ya tatu na pointi 40.

MABAO

Simba ndiyo inaongoza kwa kufunga mabao mengi zaidi hadi sasa kwenye ligi ikiwa imepachika 47, ikifuatiwa na Yanga yenye 37, Azam 33, Mbeya City 24 na Mtibwa Sugar yenye 23, huku Ruvu Shooting ikiwa ndiyo yenye mabao machache 10, ikifuatiwa na Dodoma Jiji na Polisi Tanzania zenye 14.

Vinara wa kufunga mabao pia wametokea katika timu hizo mbili, akiongoza Fiston Mayele wa Yanga mwenye 14 akifuatiwa na Moses Phiri mwenye 10, na John Bocco aliye na tisa wote wakiwa Simba. Wengine ni Said Ntibanzokiza 'Saido' wa Simba, Sixstus Sabilo wa Mbeya na Idriss Mbombo wa Azam wote wakiwa na saba kila mmoja.

ASISTI

Wekundu wa Msimbazi wameendelea kutawala namba kwani kwenye pasi za mabao 'asisti', wameongoza wao pia ambapo kati ya sita wa juu, wanne wametoka Simba.

Anayeongoza ni Clatous Chama mwenye 11, akifuatiwa na Saido ana saba, lakini sita alienda nazo Msimbazi akizitoa akiwa Geita, Sabilo wa Mbeya City anafuata akiwa na sita huku Mzamiru Yassin na Mohamed Hussein kila mmoja akiwa nazo tano.

USHINDI

Yanga ndio imeshinda mechi nyingi zaidi 16, ikifuatiwa na Simba iliyoshinda 13 na Azam 12, huku Ruvu Shooting ikiwa ndiyo imepoteza mechi nyingi zaidi 12.

Polisi Tanzania ndiyo imeshinda mechi chache zaidi, mbili, ikifuatiwa na Ruvu iliyoshinda tatu huku Coastal Union na Mbeya zikiwa zimeshinda nne nne.

CLEAN SHEETS

Yanga ndiyo imecheza mechi nyingi zaidi bila kuruhusu bao, ikifanya hivyo mara 12 ikifuatiwa na Simba iliyocheza mechi 10, Singida nane, Namungo na Azam kila moja ikiwa na 'Clean Sheets' saba.

Makipa Aishi Manula (Simba) na Djigui Diarra (Yanga) ndio vinara wa cleensheet 10 kila mmoja, wakifuatiwa na Ali Ahmada (Azam FC) mwenye saba kisha Metacha Mnata (Singida Big Stars) na Said Kipao (Kagera Sugar) wenye sita sita.

UMEME

Kadi nyekundu zimetoka 19 hadi sasa, huku Polisi Tanzania na Mtibwa zikiongoza kila moja imepata nne, Geita, Namungo na Prisons mara mbili, huku nyingine tano zikipata mara moja moja.

Mohamed Mmanga wa Polisi Tanzania ndiye anaongoza kwa kadi nyekundu akiwa na mbili na wanaofuata wote wana moja moja.

Kadi za njano zimetoka 316, Namungo ikiongoza ikiwa nazo 42, ikifuatiwa na Dodoma yenye 38, Singida 33, Prisons 31 na Ihefu 30.

Charles Ilamfya wa Mtibwa, George Sangija wa Mbeya na Sadio Kanoute wa Simba wanaongoza kwa kupata kadi za njano saba kila mmoja, wakifuatiwa na Hashim Manyanya, Emmanuel Asante wa Namungo wenye sitasita.

WENYEWE WAFUNGUKA

Kocha Msaidizi wa Simba aliyeiongoza hadi kufika mechi ya 19 akiwa Mkuu, Juma Mgunda ameeleza ligi ya msimu huu kuwa ngumu, lakini bado wana matumaini ya kufanya vizuri zaidi na kutwaa ubingwa.

"Kiuhalisia msimu huu ligi ni ngumu na timu zimejipanga kweli kweli, lakini pamoja na hayo bado hatujatoka kwenye malengo, Simba tunaamini tuna nafasi ya kutwaa ubingwa na tunaendelea kuandaa mikakati ya kuhakikisha tunafikia malengo," anasema Mgunda.

Kinara wa mabao hadi sasa, Mayele alisema licha ya changamoto anayokutana nayo kutoka kwa mabeki lakini kutwaa tuzo ya mfungaji bora ni miongoni mwa malengo yake kwa msimu huu.

"Kila mmoja anatimiza wajibu wake, mabeki wa timu pinzani kazi yao ni kukaba na mimi kazi yangu ni kufunga hivyo siyo rahisi lakini nadhani nimejipanga kuwa mfungaji bora msimu huu na kuiongoza Yanga kutetea ubingwa," alisema Mayele.

Kocha mkuu wa Ruvu Shooting, inayoshika nafasi ya pili kutoka mkiani, Mbwana Makata amefunguka kuwa na wakati mgumu lakini anautumia muda huu wa mapumziko kukisuka kikosi chake upya kwa ungwe ya mwisho.

"Hatuko sehemu salama, tunahitaji nguvu ya ziada kutoka huku chini, muda huu ambao ligi imesimama tunaendelea kujifua zaidi ili mikikimikiki ikirejea angalau tuwe imara na kufanya vizuri katika mechi zijazo," anasema Makata.

Chanzo: Mwanaspoti