Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba, Yanga zatabiriwa ugumu mzunguko wa pili

950f4002a33417c8fe4012a18feaf3cb.png Simba, Yanga zatabiriwa ugumu mzunguko wa pili

Wed, 20 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

WADAU mbalimbali wa soka nchini wamesema mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara hautakuwa rahisi kwa vinara Yanga na Simba kwa kuwa timu nyingi zimesajili kuboresha vikosi vyao.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, baadhi ya wadau hao Ismail Aden Rage, Ally Mayay na Bakari Malima walisema kutakuwa na ushindani mkubwa ambao unaweza kuleta changamoto kwa wakongwe hao wa soka nchini.

Mchezaji wa zamani wa Yanga na mchambuzi wa soka, Mayay alisema anategemea ushindani utakuwa mara mbili kutokana na aina ya usajili wa kila timu ila atakayechukua taji safari hii huenda ni kwa tofauti ndogo ya pointi moja au mbili tu.

“Kila timu imesajili kuonesha umakini na umuhimu wa kupigania taji ila Simba na Yanga zisitegemee mteremko licha ya kuwa na vikosi vizuri, changamoto na upinzani ni lazima utakuwapo,” alisema.

Mayay alisema timu kama Ruvu isipotizamwa vizuri inaweza kuwa tishio katika nafasi za juu kwani usajili wake ni mzuri na kwa sababu ilionesha mafanikio tangu mzunguko wa kwanza huenda pia ikaendeleza ubora huo.

Kwa upande wa Simba, alisema haikuwa na haja kuongeza mtu katika nafasi ya ushambuliaji kwa kuwa ipo vizuri ila inaweza kufanya vizuri zaidi au kuwa katika kiwango kile kile.

Kwa Yanga alisema usajili wake utaongeza changamoto kwa wapinzani wake. Mwenyekiti wa zamani wa Simba, Rage alisema mambo hayatakuwa mepesi kwani anachokiona kulingana na usajili wa kila timu, ushindani utaongezeka kwa kuwa timu zitakuwa zinapigania ushindi ma nyingine kubaki Ligi Kuu na wengine kubeba taji.

Alisema alichokiona Yanga ni nzuri na imeanza kuchangamka hivyo itaendeleza ubora na Simba inazidi kuwasha moto kwa hiyo kazi itakuwa kubwa. Mchezaji wa zamani wa Simba na Yanga, Malima alisema mzunguko wa pili utakuwa mgumu kwa sababu baadhi ya timu zimejiimarisha hivyo nyingine zijiandae kisaikolojia na sio kwenda na matokeo uwanjani.

Alisema kuna timu kama Coastal Union na Ihefu zimeboresha vikosi vyao hivyo anategemea taji halitakuwa rahisi kwa Simba au Yanga bali zinaweza kuibuka tim nyingine zisizotarajiwa.

“Watanzania tumekuwa tukiweka matumaini kwa Simba au Yanga kuwa ndizo zenye uwezo wa kuchukua taji au kushinda mechi zote kitu ambacho hakiwezekani, kulingana na ushindani utakavyokuwa mambo yanaweza kuwa magumu,” alisema.

Timu zinazopewa nafasi kunyakuwa taji ni Yanga, Simba, Azam FC, Namungo na Ruvu ambazo zitaendelea kutawala katika nafasi nne za juu.

Chanzo: habarileo.co.tz