Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba, Yanga zapewa vibonde tena ASFC

Droo Azam Leo Simba, Yanga zapewa vibonde tena ASFC

Fri, 2 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Droo ya hatua ya 32 Bora ya michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) imefanyika mapema leo, huku vigogo Simba na Yanga zikipewa tena timu mchekea kwenye hatua hiyo baada ya awali kuzing'oa timu za Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL), Hausung ya Njombe na Tembo ya Tabora katika mechi za 64 Bora.

Simba iliyoifumua Tembo kwa mabao 4-0 imepangwa kukutana na TRA ya Kilimanjaro inayoshiriki First League (zamani Ligi Daraja la Pili, SDL), wakati watetezi wa taji hilo, Yanga iliyoitupa nje Hausung kwa mabao 5-1 ikipewa Polisi Tanzania inayoshiriki Ligi ya Championship (zamani Ligi Daraja la Kwanza (FDL).

Katika droo hiyo iliyofanyika leo jijini Dar es Salaam pia ilihusisha mechi za hatua ya 16 Bora kwa zile timu zitakazovuka salama hatua inayofuta ya 32 Bora, ambapo mshindi wa mechi ya Yanga na Polisi atacheza na mshindi wa mchezo kati ya Dodoma Jiji na Biashara United.

Aidha mshindi wa mechi ya Simba na TRA atavaana na mshindi wa mchezo kati ya Mashujaa Kigoma na Mkwajuni FC, huku ratiba nyingine zikionyesha Azam FC itacheza hatua ya 32 dhidi ya Green Warriors na mshindi wa mechi hiyo ataumana na kati ya Mtibwa Sugar au Stand United.

Mechi nyingine za 32 zitazikutanisha Singida Fountain Gate dhidi ya ndugu zao za FGA Talents, huku Coastal Union itaumana na Mbeya Kwanza, Tabora United dhidi ya Nyamongo, KMC itaumana na Gunners na Ihefu itaimana na Mbuni FC.

Maafande wa JKT Tanzania itaumana na TMA, Namungo itavaana na Transit Camp, Kagera Sugar dhidi ya Pamba Jiji , Geita itaumana na Mbeya City na Rhino Rangers itakwaruzana na Mabao FC na kwa mujibu wa Meneja wa Mashindano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Baraka Kizuguto, mechi za raundi hiyo zitapigwa kati ya Februari 19-20 na washindi wataenda hatua ya 16 Bora ili kusaka timu nane za kucheza robo fainali ya michuano hiyo kwa msimu huu ambapo fainali ya kupata bingwa itapigwa Juni 2.

Kizuguto amesema katika raundi hiyuo ya 32 timu zinazoshiriki Ligi Kuu zitakuwa nyumbani na kwamba kwa mechi za raundi ya 16 bado haijulikani zitachezwa lini, ila umma utatangaziwa.

"Timu zijiandae zimebakiza siku 17 tu ili kuanza kwa mashindano hayo ambayo mara nyingi huwa na maajabu kwa timu zinazoonekana ndogo huwa zinashangaza wengi," amesema Kizuguto, wakati wawakilishi mbaloimbali wa timu kwenye droo hiyo nao walitoa maoni yao juu ya kilichofanyika kila upande ukipongeza.

Mwakilishi wa klabu ya Simba, Ally Shantri 'Chico' amesema; "Kikosi chao kinahitaji ushindi tu nasio kitu kingine, kwani wanataka kurudisha heshima ambayo wameikosa kwa muda kidogo katika michuano hiyo."

Kwa upande wa Ofisa Habari wa KMC, Khalid Chukuchuku amesema; "Mchezo uliopita ulikuwa mgumu hadi tukafikia hatua ya mikwaju ya penalti, hiyo ni dhahiri kuwa hakuna timu ndogo nasi tunakwenda kujipanga zaidi bila kujali tumepangwa na nani kwani haya ni mashindano."

Michuano hiyo ya ASFC ambayo zamani ilifahamika kama Kombe la FA ilianza msimu wa 2015-2016 baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) chini ya Jamal Malinzi kurejesha upya baada ya kusimama tangu mwaka 2002 wakati JKT Stars (sasa JKT Tanzania ilipokuwa bingwa wa michuano ya awali.

Tangu iliporejea Simba na Yanga kila mmoja imetwaa ubingwa mara tatu zikiwa ndio vinara, huku Mtibwa Sugar na Azam FC, kila moja ikitwaa mara moja na kwa sasa Yanga ndio watetezi wakilishikilia kwa msimu wa pili mfululizo.

Msimu uliopita Yanga ilicheza fainali na Azam kwenye Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga na kushinda bao 1-0 baada ya awali kutwaa taji kwa kuifunga Coastal Union ya Tanga katika fainali kali iliyopigwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha iliyoamuliwa kwa penalti 4-1 baada ya dakika 120 kuisha kwa sare ya 3-3.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live