Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imekutana na Wakurugenzi Watendaji wa klabu nne zilizopata nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa ya CAF ili kupanga mikakati ya namna gani zijipange kuelekea msimu mpya wa mashindano yao.
Timu hizo ambazo ni Yanga, Simba zitakazoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika, Azam FC na Singida Fountain Gate kwenye Kombe la Shirikisho Afrika pamoja na Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC).
Hata hivyo, kati ya timu hizo nne, Simba pekee itakuwa na michuano minne msimu ujao pamoja na ile ya Super League itakayoanza Novemba mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Timu hizo zitaanza na Ligi Kuu Bara na michuano ya CAF ambayo yote itaanza Agosti na baadaye Simba itashiriki Super League iliyotangazwa kuanza rasmi Oktoba mwaka huu.
Habari za ndani zinaeleza kuwa mabosi hao walikutana kuona namna gani ratiba yao ilivyo na kuwashauri jinsi ya kusajili vikosi vipana na kujiandaa vyema kutokana na namna miundombinu ilivyo nchini wanapokwenda kucheza mechi za ugenini.
"Ni kweli tumekutana na wenzetu wa Bodi ya Ligi kujadili namna msimu ujao ulivyo kwetu, hivyo kazi iliyobaki ni kwetu kuwa na vikosi imara ili tufanye vizuri, kwetu ni kuhakikisha tunafanya usajili mzuri ili kuwa na timu ambayo itamudu kucheza mashindano yote," alisema mmoja wa mabosi wa timu hizo.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa TPLB, Almasi Kasongo alisema timu hizo zinatakiwa kujiandaa vizuri kwa mambo mawili, kiuchumi na usajili.
"Miundombinu yetu sio rafiki sana, hivyo hawa wawakilishi wetu wanapaswa kujaandaa vizuri sana kuanzia uchumi hadi usajili wao, wawe na vikosi vipana maana ratiba inaweza kuwabana, wakatoka kucheza nje ya nchi halafu wakifika hapa wanakuwa na mechi za nje ya mikoa yao.
"Hivyo kuna kila sababu ya kujipanga vizuri kwao kwneye mambo hayo mawili na tutajitahidi kutengeneza ratiba ambayo itakuwa rafiki kwa timu zote ili pia kuepukana na mechi za viporo," alisema Kasongo