Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba, Yanga zapewa mbinu 8 Dar

Yanga Vs Simba Kirumba Simba, Yanga zapewa mbinu 8 Dar

Wed, 15 Feb 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Historia ya nyuma inazipa jeuri Simba na Yanga kutinga hatua ya robo fainali ya mashindano ya Klabu Afrika licha ya kuanza vibaya mechi za makundi mwishoni mwa wiki iliyoisha na jambo linalozipa matumaini zaidi ni kupata dondoo muhimu za kimbinu na kiufundi za wapinzani wao katika mechi zinazofuata, Raja Casablanca na TP Mazembe ambazo zimeanza kijeuri kwa kupata ushindi mnono katika mechi zao za mwanzo.

Simba ilianza kwa kupoteza kwa bao 1-0 ugenini dhidi ya Horoya, Jumamosi iliyopita kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na kesho yake, Yanga ikafungwa mabao 2-0 ugenini kwa Monastir ya Tunisia kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.

Matokeo hayo yanaweza kuwapa presha na hofu mashabiki wa timu hizo lakini kumbukumbu ya mashindano ya klabu Afrika zinaonyesha kuwa zipo timu ambazo zilianza vibaya kama ilivyo kwa Simba na Yanga lakini mwisho wa siku zilifanya vyema katika mechi zilizofuata na kisha zikatinga robo fainali na zingine hadi nusu fainali na fainali.

Msimu uliopita, CR Belouizdad ya Algeria ilianza kwa kupata sare mbili kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Etoile du Sahel na Esperance za Tunisia lakini ikafanya vyema katika mechi zinazofuata za kundi hilo na ikatinga robo fainali.

Katika msimu wa 2020/2021, haohao Belouizdad walipata pointi moja katika mechi mbili za mwanzo ambazo walifungwa moja na kutoka sare moja lakini wakatinga robo fainali kama ilivyotokea kwa Kaizer Chiefs ambao wlaifika hadi fainali wakati MC Alger wenyewe walipata pointi mbili katika mechi za mwanzo na wakatinga hatua inayofuata.

Hata hivyo, wakati kumbukumbu ya nyuma ikiwashusha presha mashabiki wa Simba na Yanga, mabenchi ya ufundi ya timu hizo yamepewa dondoo za namna wapinzani wao Raja Casablanca na TP Mazembe walivyo kwa maana ya ubora na udhaifu wao pamoja na nini wakifanye ili wapate ushindi ambao utasaidia kuziweka katika nafasi nzuri kwenye makundi yao.

SIMBA

Kuna mambo sita ambayo Simba inapaswa kuyafanyia kazi katika kuhakikisha wanaichapa Raja Casablanca watakapokutana siku ya Jumamosi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa na tayari benchi la ufundi la timu hiyo limeshanasa dondoo hizo na limeshaanza kulifanyia kazi.

Kwanza Raja ni timu ambayo imekuwa na hulka ya kucheza soka la kushambulia katika uwanja wowote ule pasipo kujali ipo nyumbani au ugenini na ina tabia ya kulazimisha kutafuta bao katika dakika 15 za mwanzo na jambo la pili wachezaji wake ni wajanja mno katika kuwapa presha mabeki wa timu pinzani kufanya makosa ndani ya eneo la hatari ili kupata penalti ama faulo.

Jambo la tatu ni uwezo wao mkubwa wa kushambulia kwa mipira ya juu na krosi ikitumia uwezo wa wachezaji kufunga mabao kwa kutumia aina hiyo ya mashambulizi na jambo la nne ni ubora wa kucheza kitimu ambao wamekuwa nao unaozipa wakati mgumu timu pinzani kujua hasa nani wa kumdhibiti pindi wanapokabiliana nao.

Mbali na hayo pia ni wajanja wa kuwapanikisha wachezaji wa timu pinzani na kupoteza muda hasa wanapokuwa wanaongoza na jambo la sita ni safu imara ya kiungo na wachezaji wa pembeni ambao wanao, wanaowategemea katika kuhakikisha timu hiyo inapata matokeo mazuri.

Kutokana na uimara huo wa Raja Casablanca, suluhisho linaloonekana linaweza kuisaidia Simba ni kutumia mawinga wenye kasi lengo la kuhakikisha inadhibiti mashambulizi ya wapinzani wao hasa kwenye krosi na mipira ya juu kutokea pembeni lakini pia kuhakikisha wanakuwa na namba kubwa katika safu ya kiungo.

Kocha Robertinho anaweza kutumia mfumo wa 3-4-3 akiwa na Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein, Joash Onyango, Enock Inonga, Saido Ntibazonkiza, Clatous Chama, Mzamiru Yassin, Ismail Sawadogo, Pape Sakho na John Bocco.

Kocha msaidizi wa Simba, Juma Mgunda alisema wameshafanya tathimini juu ya ubora na udhaifu wa Raja Casablanca na wameanza kuufanyia kazi ili wapate matokeo mazuri.

"Kwanza ni kujiandaa na kujipanga vizuri na hata wachezaji wanajua wanahitajika kufanya nini pale Benjamin Mkapa.Sisi kama benchi la ufundi tutajitahidi kuhakikisha tunafanya vizrui kwenye mechi hiyo inayofuata. Tunajua ni mechi ngumu lakini kwa maandalizi na ari tuliyonayo tuna imani kubwa ya kufanya vyema," alisema Mgunda.

YANGA

Yanga itakuwa na kibarua kigumu mbele ya vinara wa kundi lao, TP Mazembe ambao mchezo wa kwanza waliibuka na ushindi wa mabao 3-1 nyumbani dhidi ya Real Bamako.

Alisema jambo la kwanza, Mazembe wamekuwa na ujanja wa kufunga mabao ya mbali na pili wana uzoefu mkubwa wa kutumia mipira ya kutenga na krosi kufunga mabao, huku akisema jambo la tatu Wanapocheza ugenini wamekuwa hawamiliki sana mpira na huwa wanashambulia kwa kushtukiza ingawa wamekuwa wakitumia nafasi chache ambazo wamekuwa wakitengeneza.

Yanga inaweza kunufaika na kasi ndogo ya walinzi wa kati wa TP Mazembe ikiwa washambuliaji wake wa kati Fiston Mayele na Kennedy Musonda watakuwa makini katika kutumia nafasi ambazo watakuwa wanatengeneza.

Eneo la kiungo la Yanga linapaswa kufanya kazi ya ziada kuivunja TP Mazembe katikati mwa uwanja kwani ndilo eneo ambalo timu hiyo kutoka DR Congo limekuwa likitegemea katika ujenzi wa mashambulizi na hata kuipa ulinzi timu.

Kuendelea kutumia viungo watano katika mfumo wa 4-2-3-1 kunaweza kuendelea kuwa tegemeo kwa kocha Nasreddine Nabi na benchi lake la ufundi.

Kikosi cha Yanga ambacho kinaonekana kinaweza kuwa silaha ya kuimaliza Mazembe kinaweza kuundwa na Djigui Diarra, Djuma Shaban, Lomalisa Mutambara, Dickson Job, Yannick Bangala, Khalid Aucho, Aziz KI, Mudathir Yahya, Fiston Mayele, Salum Abubakar na Jesus Moloko.

WADAU WAZIPA SOMO

Kocha wa timu ya taifa ya ufukweni , Boniface Pawasa alisema kiufundi Raja Casablanca ni hatari dakika ya 1-20 na dakika 20 za mwisho, hivyo aliwashauri mastaa wa timu na benchi la ufundi kufanya mazoezi yanayoendana na uhalisia wa mechi husika.

"Mbinu za Waarabu wengi ni dakika za mwanzo na mwisho, wanapokuwa wanaongoza utawaona wakipoteza muda, hivyo Simba ni vizuri wakafuatilia sana mechi zao, jambo lingine ugenini wanajilinda zaidi," alisema.

Kwa upande wa Yanga wanaocheza na TP Mazembe ambayo aliielezea kwamba "Inacheza soka la wazi na mpira wa moja kwa moja na asilimia kubwa ya wachezaji wa Yanga wanaijua zaidi Mazembe, kinachotakiwa ni umakini kupata matokeo;

Aliongeza;"Kiujumla Simba na Yanga zimepoteza ugenini kutokana na mapungufu ya safu za ulinzi na washambuliaji walikosa umakini wa umaliziaji."

Kaimu Mkurugenzi wa michezo Tanzania, Ally Mayay alisema kama Simba na Yanga zikifanya marekebisho ya udhaifu wao wa mechi zilizopita, watazishangaza TP Mazembe na Raja Casablanca.

"Ni kupanga mpango wa kuhakikisha timu zinapokuja kucheza hapa ni lazima kupata pointi tatu. Hatua hii ni ngumu lakini huu ni wakati wa klabu zetu kuthibitisha ubora wa ligi yetu. Katika kudhibiti mipira ya juu kuna kazi inatakiwa kufanyika ili udhaifu huo usiweze kujirudia," alisema Mayay.

Chanzo: Mwanaspoti