Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba, Yanga zaliza wengi Zenji

Yanga Ngushi Simba, Yanga zaliza wengi Zenji

Mon, 9 Jan 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Simba na Yanga zote zimeaga michuano ya Kombe la Mapinduzi 2023, baada ya kuchemsha kwenye hatua ya makundi na kitendo hicho, kimewaumiza wengi wakiwamo waandaaji wa michuano hiyo ambao wameweka bayana walivyovurugwa na vigogo hao.

Mwenyekiti wa Mashindano ya Mapinduzi, Khamis Abdallah Said amesema wameumizwa na wababe wa soka la nchini kushindwa kuyaheshimu michuano hiyo kwa kutoyapa kipaumbele.

Said aliyasema hayo muda mchache baada ya Yanga kuifuata Simba kwa kuondolewa katika michuano hiyo hatua ya makundi huku akikiri kuwa wamepata somo kama waandaaji.

Alisema timu hizo zina mashabiki wengi visiwani na zimekuwa zikipendwa zaidi tofauti na timu za hapa, hivyo amewaomba viongozi wa timu hizo kusoma alama za nyakati hata kama hawataki kombe basi walete wachezaji wao wote ili kuwapa burudani wapenzi wa timu hizo.

“Simba na Yanga msimu huu hawajayapa uzito mashindano haya kutokana na aina ya vikosi walivyokuja navyo, sio jambo zuri walilolifanya hatujajua sababu ni nini tutawasiliana nao,” alisema Said na kuongeza;

“Wametupa funzo tunaamini itafika wakati wao ndio watakuwa wanaomba kushiriki michuano hii, tunapambana kuzipandisha viwango timu zetu ili nazo ziweze kuwa na ukubwa unaostahiki kuwa na mashabiki wengi.”

Said alisema wao kama waandaaji wa mashindano hawajaumizwa kuondolewa kwa timu hizo, ila kitendo cha kuleta vikosi ambavyo sio sawa na kama wangeamua kuwarudisha wasishiriki ingekuwa sawa kisheria.

“Tangu mwanzo wa mashindano walionyesha kutokuwa na uwakilishi mzuri kutokana na vikosi walivyoleta huku wengine wakija na wachezaji ambao waliwaweka majukwaani.”

Akizungumzia ubora wa timu za Zanzibar, Said alisema anaishukuru serikali kuzisaidia timu hizo kupata udhamini ameona matunda yake na anatarajia kuona ubora huo ukiongezeka msimu hadi msimu.

“Udhamini uliopatikana umeongeza chachu kwa timu zetu ambazo zimeonyesha ushindani kwenye mashindano haya tunatarajia wadhamini wengine wengi kuongezeka na kuifanya ligi yetu inakuwa bora.”alisema.

Wakati huohuo alizingumzia makundi kupangwa manne na timu tatu tatu kuwa wamefuata maoni ya wadau kuwa timu zinatoka kwenye mashindano mengi hivyo kucheza mechi nyingi wanachoka.

“Timu kucheza mechi nne hadi fainali ni maoni ya wadau na sisi kama waandaaji tulichukulia uzito ili kupunguza mzigo kwa wachezaji ambao wanatoka kucheza ligi na kuja Mapinduzi ili wasicheze mechi nyingi.”

Chanzo: Mwanaspoti