Kitendo cha klabu za Simba na Yanga kufanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa kimeelezwa kuwa kinaongeza umaarufu wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Hilo limeelezwa na Ofisa Habari wa Bodi ya Ligi, Karim Boimanda kwenye mjadala wa Simba, Yanga kufuzu robo fainali ya michuano ya kimataifa nini maana yake kwa soka la Tanzania na ukanda wa Afrika Mashariki ambao umejadiliwa kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter ya Mwananchi 'Twitter Space'.
Boimanda ambaye alijikita kuongelea zaidi ligi, alisema, "Tumekuwa tukikusanya watu wengi viwanjani hawasikilizani lakini hapa watu wanasikilizana kwa hiyo niwapongeze sana...., timu zinapofuzu kwenda robo kwanza tunaongeza umaarufu wa ligi yetu, inavutia madhamini kutoka ndani na nje ya nchi,"
"Wadhamini wanaleta fedha ambazo zinasaidia timu kuwa sawa kiasi cha kuweza kusajili wachezaji bora kutoka ndani na nje ya nchi. Baada ya klabu kupata nguvu zinaenda kufanya vizuri kwenye mashindano, klabu ikiwa sawa ndio inapata nguvu pia ya hata kuendesha soka la vijana," alisema.
Boimanda anatamani kuona timu za Ligi Kuu Bara zikiendelea kufanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa ili kuendelea kuipa umaarufu ligi yetu na isiwe kwa klabu za Simba na Yanga pekee.