Pengine katika michuano inayomilikiwa na Shirikisho la mpira wa miguu barani Afrika CAF kwa ngazi ya klabu ni nadra sana kutokea kwa vigogo wa soka Tanzania, Simba na Yanga kuondoka ndani ya siku moja kisha kugawana anga lakini kwa sasa ndivyo ilivyo.
Ipo hivi Klabu za Simba na Yanga zote zinatarajiwa kuondoka nchini Septemba 14, kuelekea katika michezo yao ya kuwania kufuzu hatua ya makundi ya ligi ya mabingwa Afrika.
Simba na Yanga zote zimeweka malengo ya kuhakikisha kuwa msimu huu wanavuka hatua ya makundi na kwenda mbali zaidi katika Ligi ya Mabingwa Afrika.
Vigogo hao kwa upande wa Yanga wao watasafiri kuelekea Rwanda kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wao dhidi ya Al Merreikh unaotarajiwa kufanyika Septemba 16, huku Simba wao wakielekea Zambia kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wao dhidi ya Power Dynamos ambao pia utapigwa Septemba 16, mwaka huu.
Meneja wa Habari na Mawasiliano Simba Ahmedy Ally alisema kuwa; “Tunatarajia kuanza safari rasmi Septemba 14 kuelekea nchini Zambia tayari kwa ajili ya mchezo wetu wa ugenini, malengo yetu ni kwenda kushinda mchezo huo naamini pia tunaweza kufanya hivyo,”.
Kwa upande wa Yanga Ofisa Habari, Ally Kamwe pia alisema kuwa: “Yanga tunatarajia kuondoka Septemba 14, kuelekea Rwanda na misafara yetu itakuwa miwili angani na ardhini, ambapo tutaondoka na msafara mkubwa wa mashabiki wa Yanga, tunakwenda kutoa burudani nje ndani kwa maana ya kupata matokeo nje ndani,” alisema kiongozi huyo.