Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba, Yanga zagawana mabao

Simba Vs Yanga Chama Yulee.jpeg Simba, Yanga zagawana mabao

Mon, 8 Apr 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Wakati tarehe ya pambano la marudiano la Kariakoo Derby ikitangazwa rasmi jana kuwa sasa litapigwa Aprili 20, rekodi zinaonyesha hadi sasa vigogo hao wa soka nchini wamegawana idadi ya mabao, Simba ikiwa kinara ugenini ilihali watani wao Yanga wakikamua zaidi nyumbani.

Watani hao wataumana wiki mbili zijazo baada ya awali ratiba kuonyesha mechi yao ingechezwa Aprili 16 likiwa ni pambano la marudiano kwani zilishakutana mara ya kwanza msimu huu katika Ligi Kuu Novemba 5 mwaka jana na Simba kunyooshwa mabao 5-1.

Kwa sasa Yanga inaongoza msimamo ikiwa na pointi 52 baada ya mechi 20 na kufunga mabao 49, wakati Simba ikiwa ya tatu na alama 45 kupitia mechi 19 na mabao 39, huku Azam FC ikishika nafasi ya pili kwa pointi 47 baada ya mechi 21 ikifunga mabao 47.

Hata hivyo, rekodi zinaonyesha kuwa katika mechi 19 Simba imevuna mabao 20 ugenini, huku nyumbani ikiwa na 19, pia imeruhusu mabao manane nyumbani na ugenini imefungwa 10 kuonyesha kwa mechi za nyumbani Wekundu hao wapo imara zaidi kulinganisha na timu nyingine, japo imepitwa mechi moja za ushindi ikiwa na 14 kama Azam, ilihali Yanga imeshinda mechi 17 kati ya 19.

Kwa upande wa Yanga, katika mechi 20 ilizocheza na kuvuna mabao 49, mabao 29 imeyafunga nyumbani na 20 iliyapata ugenini na yenyewe imefungwa manne nyumbani na sita ugenini, yakiwamo matano iliyofungwa na Ihefu na Azam zilizowachapa 2-1 kila timu na jingine la watani wao Simba ilipoinyoa 5-1.

Yanga imepoteza mechi mbili tu na kutoka sare moja, huku ikishinda 17 katika mechi 20 ilizocheza hadi sasa.

REKODI ZILIVYO SIMBA

Mtibwa Sugar 2-4 Simba (Ago 17), Simba 2-0 Dodoma (Ago 20), Simba 3-0 Coastal Union (Sept 21), Prisons 1-3 Simba (Okt 5), Singida BS 1-2 Simba (Oktoba 8), Mashujaa 0-1 Simba (Feb 3), Simba 2-1 Ihefu (Okt 28), Simba 1-5 Yanga (Nov 5), Simba 1-1 Namungo (Nov 9), Tabora United 0-4 Simba (Feb 6).

Nyingine Simba 1-1 Azam FC (Feb 9), Simba 3-0 Kagera Sugar (Des 15), Geita Gold 0-1 Simba(Feb 12), KMC 2-2 Simba (Dec 23), JKT Tanzania 0-1 Simba (Feb 15), Coastal Union 1-2 Simba (Mar 9), Simba 1-2 TZ Prisons (Mar 6), Simba 3-1 Singida BS (Mar 12) na Simba 2-0 Mashujaa (Mar 15).

YANGA

Yanga 5-0 KMC (Ago 23), Yanga 5-0 JKT Tanzania (Ago 29), Yanga 1-0 Namungo (Sep 20), Ihefu 2-1 Yanga (Okt 4), Geita Gold 0-3 Yanga (Okt 7), Yanga 3-2 Azam (Okt 23), Yanga 2-0 Singida BS (Okt 27), Simba 1-5 Yanga (Nov 5), Coastal Union 0-1 Yanga (Nov 8) na Yanga 2-1 Mashujaa (Feb 8).

Nyingine ni; Kagera Sugar 0-0 Yanga (Feb 2), Yanga 4-1 Mtibwa Sugar (Des 16), Yanga 1-0 Dodoma (Feb 5), Tabora United 0-1 Yanga (Des 23), TZ Prisons 1-2 Yanga (Feb 11), KMC 0-3 Yanga (Feb 17), Namungo 1-3 Yanga (Mar 8), Yanga 5-0 Ihefu (Mar 11), Yanga 1-0 Geita Gold (Mar 14) na Azam 2-1 Yanga (Mar 17).

MTAZAMO WA WADAU

Licha ya Simba kuongoza kuvuna mabao mengi ugenini (20), aliyekuwa beki wa timu hiyo, Joash Onyango anayecheza Ihefu (Singida Black Stars) kwa sasa, anaona timu hiyo inahitaji mshambuliaji wa kuamua mechi: "Inatakiwa isajili straika ambaye hawezi kukosa nafasi zinazotengenezwa."

Mtazamo wa staa wa zamani wa Yanga, Mohammed Hussein 'Mmachinga' mwenye rekodi ya mabao 26 Ligi Kuu Bara, aliyofunga 1996 alisema; "Kwa ushindani wa Ligi Kuu ulivyo mgumu, klabu kongwe zinaonyesha ukomavu.

"Ligi ni ngumu kutokana na udhamini, hivyo si kitu rahisi kupata mabao na pointi nyingi ugenini, pia mastaa wa timu hizo wanalipwa vizuri, hivyo lazima waonyeshe utofauti wa thamani zao."

Chanzo: Mwanaspoti