Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba, Yanga zaandaa sapraizi

Simba, Yanga Warejea Ligi Kuu Wikiendi Hii Simba, Yanga zaandaa sapraizi

Thu, 28 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati dirisha dogo la usajili likiwa limeshafunguliwa, Yanga imesema kama mambo yakienda vyema, itawatambulisha baadhi ya wachezaji wake wapya katika mashindano ya Kombe la Mapinduzi, kauli hiyo pia ikitolewa na watani zao, Simba.

Yanga itaanza kampeni ya michuano hiyo Desemba 31, mwaka huu kwa kuwavaa  Jamhuri wakati Januari Mosi, mwakani JKU itawakaribisha Simba na keshokutwa mechi za ufunguzi itakuwa ni kati ya Mlandege dhidi ya Azam FC na Vital'O itawaalika Chipukizi.

Meneja wa Yanga, Walter Harrison, alisema wanataka kufanya sapraizi kwa mashabiki wa soka Zanzibar kwa kuwatambulisha wachezaji wapya ambao wamesajiliwa katika kipindi cha dirisha dogo la usajili.

Alisema wanatarajia kuwatambulisha wachezaji ambao wamewasajili kuisaidia timu hiyo kufanya vizuri katika michuano mbalimbali ikiwamo Ligi ya Mabingwa Afrika.

"Nawaambia wananchi wajiandae kwa sababu tunaenda Zanzibar kuhakikisha tunakuwa na ushiriki mzuri, tunachukua kombe, safari hii tunakuja tofauti kabisa tukiwa na malengo ya kuwapa burudani mashabiki wetu, tumedhamiria kutwaa ubingwa na wajue tu Zanzibar safari hii tunakuja na 'sapraizi' ya wachezaji wapya," alisema Harrison.

Tayari Yanga imeshatangaza kumsajili,   Shekhan Hamisi Ibrahim, kutoka JKU ya Zanzibar.

Naye Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi, alisema ni kweli anahitaji straika, lakini ni ngumu sana kwa kipindi hiki cha dirisha dogo kupata mshambuliaji mwenye ubora mkubwa.

"Sio sisi tu Yanga bali dunia nzima mahitaji wa mastraika asilia ni makubwa sana na hata Real Madrid wanahitaji pia. Ni kweli tunahitaji, lakini kwa kipindi hiki cha dirisha dogo ni ngumu sana, wachezaji wazuri wengi wako kwenye vikosi vinavyocheza Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho, nyingine zinaendelea na nyingine zimetolewa.

Lakini kwa sasa ni lazima utumie pesa nyingi sana na anaweza kuja kupindi hiki pia asifanye chochote kwa sababu hajui mazingira, nchi, mfumo na vitu vingine, ila tutajitahidi," alisema kocha huyo.

Baadhi ya washambuliaji wanaotajwa kuwindwa na Yanga ni Sankara Karamo wa Asec Mimosas ya Ivory Coast na Emmanuel Bola anayecheza FC Lupopo ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) na Jonathan Sowah wa Medeama ya Ghana.

Taarifa zinasema ada ya uhamisho ya Bola kujiunga na Yanga inatajwa kuwa ni Dola za Marekani 100,000 lakini kumekuwa na sintofahamu kuhusu nyota huyo kuridhia kujiunga na mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

“Tayari Gamondi alishawaambia aina ya mshambuliaji anayemhitaji na kilichobakia ni kukamilisha masuala machache, baada ya hapo watamtambulisha ili kujiunga mazoezini mapema kwa ajili ya kujiandaa na michuano mbalimbali inayowakabili," kilisema chanzo chetu.

Naye Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema kikosi chao kinakwenda Zanzibar kikiwa kimesahau matokeo ya mechi zilizopita kwa sababu wanahitaji 'kuzaliwa' upya.

Ahmed alisema watatumia mashindano hayo kuongeza ubora wa wachezaji wao lakini kupambana kuwania taji la michuano hiyo yenye historia kubwa nchini.

"Tutashiriki katika mashindano ya Kombe la Mapinduzi tukiwa kamili, ukiondoa nyota ambao wanakwenda kutumikia mataifa yao, tunahitaji heshima," Ahmed alisema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live