Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba, Yanga zaamsha mzuka

Mzuka Pioc Data Simba, Yanga zaamsha mzuka

Mon, 24 May 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

BAADA ya kufanikiwa kupata timu ya Ligi Kuu Bara, Chama cha Soka Mkoa wa Geita (Gerefa) kimeanza mikakati ya kuandaa uwanja ambao utatumika msimu ujao ili kuwapa burudani wadau na mashabiki wa soka mkoani humo.

Mkoa huo ambao uliundwa mwaka 2012 ukimegwa kutoka Mwanza, msimu ujao utazishuhudia Simba na Yanga kufuatia Geita Gold kufanikiwa kupanda Ligi Kuu baada ya kusota kwa misimu minne.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mwenyekiti wa chama hicho, Salum Kulunge alisema kwa sasa wameanza mikakati ya ukarabati wa viwanja ambavyo vitatumika kwa ajili ya mechi za ligi kuu.

Alisema kwa kuanzia, Gerefa na wadau wa soka mkoani humo watafanyia maboresho uwanja wa Nyankumbu Sekondari kwa kuweka ukuta ambao utatenganisha shule ili kuondoa usumbufu unaoweza kujitokeza.

“Tutajenga ukuta ambao utatenganisha sehemu ya mashabiki na shule lakini kuuweka sawa ili ukidhi viwango na lengo ni kuhakikisha mashabiki hawakosi burudani kwa timu yao, tumejipanga kimkakati,” alisema Kulunge.

Mwenyekiti huyo ambaye pia ni muasisi wa timu hiyo, aliongeza kuwa kutokana na klabu hiyo kuwa chini ya Halmashauri, wanaendelea kuweka mipango ya kukamilisha uwanja wa kisasa uliopo Magogo mjini humo.

Alisema mipango yao ni kuwa mzunguko wa kwanza Geita Gold itatumia uwanja wa Nyankumbu Sekondari na raundi ya pili wahamie rasmi katika dimba hilo la kisasa.

“Kuanzia Jumatatu (leo) Mkandarasi ataanza kazi na hii ni kutaka kutekeleza mpango kazi wetu kwamba mzunguko wa kwanza tutumie uwanja huo na raundi ya pili tuhamie sehemu mpya na rasmi, ni dimba la kisasa kabisa,” alisema.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz