Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba, Yanga watawala Ubingwa Shirikisho

Yanga Shirikishoz Yanga ndio Bingwa Mtetezi wa Kombe la Shirikisho

Wed, 8 Mar 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Mchezo wa juzi usiku kati ya Azam FC na Mapinduzi FC ulikamilisha wababe nane watakaomenyana katika hatua ya robo fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports (ASFC), ambalo katika misimu saba iliyopita Simba na Yanga zimelitwaa mara tano.

Tangu michuano hiyo iliporejeshwa mwaka 2015, Simba imebeba ubingwa mara tatu, 2016/17, 2019/20 na msimu wa mwaka 2020/21 wakati Yanga ikibeba mara mbili 2015/16, na 2021/22, Mtibwa 2017/18 na Azam msimu wa mwaka 2018/19.

Katika misimu hii saba, Yanga 2015/16 ndio ilikuwa bingwa wa kwanza kwa kuichapa Azam mabao 3-1 wakati Simba iliishia hatua ya robo fainali ilipofungwa na Coastal Union 2-1 ambayo nayo ilifungwa na Yanga katika nusu fainali.

Msimu wa mwaka 2016/17, Simba ikitwaa ubingwa kwa kuichapa Mbao FC, Yanga iliishia hatua ya nusu fainali ikifungwa na Mbao FC bao 1-0 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba bao lililofungwa na Pius Buswita.

Simba mambo yakawaendea ovyo msimu wa 2017/18, ilipoondolewa na Green Warriors kwa penalti hatua ya 32 baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya bao 1-1.

Yanga nayo haikufika mbali kwani ilichapwa na Singida United kwa penalti baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya bao 1-1 na kuifanya Singida kwenda hadi fainali na kupoteza kwa mabao 3-2 mbele ya Mtibwa Sugar.

Simba ikaendelea kufanya vibaya msimu uliofuata (2018/19), ilipoondolewa hatua ya 32 kwa kuchapwa na Mashujaa FC mabao 3-2 wakati Yanga ilichapwa nusu fainali mabao 2-0 na Lipuli iliyotinga fainali ambapo Azam alitwaa kombe.

Msimu wa mwaka 2019/20, Simba ikitwaa ubingwa kwa kuichapa Namungo 2-1, Yanga iliishia hatua ya nusu fainali ikifungwa 4-1 na Simba.

Simba ikatetea ubingwa msimu wa 2020/21 ilipoichapa Yanga bao la Taddeo Lwanga kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma.

Msimu uliopita (2021/22), Yanga ikaisambaratisha Simba nusu fainali pale Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza kwa bao la Feisal Salum ‘Fei Toto’.

Tayari timu zote zimetinga hatua ya robo fainali, Simba ikiichapa African Sports mabao 4-0 huku Yanga ikiichapa Tanzania Prisons mabao 4-1.

Michezo ya hatua ya robo fainali inatarajiwa kuchezwa kuanzia Machi 31 hadi Aprili 2, wakati nusu fainali ikichezwa Aprili 29 na 30 na fainali ikipigwa baada ya Ligi Kuu kumalizika Mei 28.

Ulimboka Mwakingwe ambaye kwa sasa yupo Tanga kwenye kozi ya ukocha anasema michuano ya ASFC imekuwa chachu kubwa kwa timu katika kuongeza uimara.

“Timu inaposhiriki michuano mingi inasaidia kuwafanya wachezaji kuwa imara zaidi na kuwapa nafasi hata wale wachezaji ambao hawapati nafasi ya kucheza huwa wanacheza inapokuwa michuano mingi,” alisema.

Wababe waliopenya robo fainali ni Yanga, Simba, Azam, Singida BS, Geita Gold, Ihefu na Mtibwa Sugar.

Chanzo: Mwanaspoti