Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba, Yanga waombeana dua mbaya

43563 Pic+kagere Simba, Yanga waombeana dua mbaya

Mon, 25 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Baada ya Simba kuinyuka Azam FC mabao 3-1 juzi, vita ya kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Bara na ufungaji bora imezidi kupamba moto huku timu hasimu, Simba na Yanga zikitazamana kwa jicho baya.

Simba yenye pointi 45 ikiwa nafasi ya tatu, imekoleza kasi ya kutaka kutetea ubingwa wake wakati Yanga iliyo nafasi ya kwanza kwa pointi 61 nayo haikubali kwani inataka kurejesha ubingwa Jangwani.

Mashabiki wa Yanga ni kama wanawaombea Simba dua mbaya wakiamini kuwa Simba haina ubavu wa kushinda michezo yao yote saba ya viporo huku Simba wakiwajibu kuwa kila mtu ashinde mechi zake na mwisho watapiga hesabu.

Simba imebakiwa na michezo 20 na kama itashinda yote itafikisha pointi 105 wakati Yanga ikishinda mechi zote itafikisha pointi 100.

Kama Yanga inautaka ubingwa msimu huu, itabidi ishinde mechi zote na iiombee Simba ipoteze mechi mbili tu kwani wao watakuwa wamefikisha pointi 100 na Simba itakuwa na pointi 99.

Hata hivyo licha ya Simba kuonekana imebaki na mechi nyingi pia ina kazi kubwa ya kupambana kushinda mechi 10 za mikoani wakati Yanga inakabiliwa na michezo mitano tu mikoani.

Simba ina mechi 11 za ugenini lakini moja ni kama watakuwa nyumbani kwani watacheza na KMC kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam wakati nyingine watazikabili Lipuli ya Iringa keshokutwa, Stand United ya Shinyanga, Coastal Union (Tanga), Alliance (Mwanza), Biashara United (Mara), Singida United (Singida), Mbeya City na Prisons za Mbeya na Mtibwa Sugar ya Morogoro.

Yanga yenyewe ina mechi saba za ugenini lakini mbili dhidi ya Azam na Ruvu Shooting watakuwa kama wako nyumbani Uwanja wa Taifa. Miamba hiyo ina kazi kwa Alliance, Lipuli, Biashara United na Ndanda ya Mtwara.

Simba, Yanga zatikisa mikoani

Bado Simba inaonekana ina mwenendo mzuri kwenye ligi kwani ina uwiano mzuri wa kushinda katika mechi za nyumbani na ugenini sawa na watani zao Yanga ingawa inatakiwa kuwa makini na mechi zake za viporo.

Hadi sasa, Simba imeshacheza mechi 10 nyumbani na imeshinda nane, imetoa sare mechi mbili na haijapoteza wakati katika mechi za ugenini imecheza michezo minane,imeshinda sita,imetoa sare mchezo mmoja na imepoteza mmoja.

Yanga imecheza michezo 12 nyumbani, imeshinda 10 na kutoa sare mmoja wakati ugenini imecheza michezo 13, imeshinda tisa, sare tatu na kupoteza moja .

Katika hiyo michezo nane ya ugenini ya Simba, kwenye viwanja vya mikoani imecheza michezo mitano na imeshinda mitatu dhidi ya African Lyon 3-0, Mwadui 3-1 na JKT Tanzani 2-0, imetoka sare mchezo mmoja dhidi ya Ndanda 0-0 na imepoteza mmoja dhidi ya Mbao 1-0.

Simba ina kibarua kigumu dhidi ya Lipuli watakayokutana nayo keshokutwa Jumanne kwani katika misimu miwili timu hizo zimekutana mara tatu nyumbani na ugenini na hakuna aliyeibuka mbabe wa mwenzake zaidi ya sare.

Wekundu wa Msimbazi wanaweza kupata mteremko kwa Stand United ambayo kwa miaka ya karibuni katika michezo minne waliyokutana kwenye Uwanja wa Kambarage Shinyanga Simba ilishinda mara tatu na mara moja ilipoteza kwa bao 1-0 Februari 21 mwaka 2015.

Kagera Sugar nayo huwa haifurukuti kwa Simba kwani katika michezo minne ya karibuni imeshinda mechi moja tu April 2,2017 ilipoichapa Simba mabao 2-1. Timu nyingine ambazo zimekuwa zikiambuliwa vipigo kwao mara kwa mara zinapokutana na Simba ni Kagera Sugar, Coastal Union, Mbeya City,Prisons, wakati Mtibwa Sugar imekuwa haitabiriki kwani katika michezo mitano ya miaka ya karibuni timu hizo zilipokutana kwenye Uwanja wa Jamhuri Morogoro, Mtibwa ilipoteza mechi mbili sare mbii na ilishinda mechi moja.

Kocha wa Simba Patrick Aussems amekiri mechi zilizobaki ni ngumu zaidi kwani kila mmoja aliye juu anautaka ubingwa.

“Siku 10 za mwisho zilikuwa nzuri. Matokeo mazuri, kiwango bora na mashabiki walifurahi.Jambo muhimu timu inakua kiakili na kua na mtazamo sahihi hili ni jambo zuri ukilinganisha na ratiba ngumu tuliyonayo katika wiki zijazo. Tunahitaji kujitoa na kupambana kama tunataka ubingwa”alisema Aussems.



Chanzo: mwananchi.co.tz