Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba, Yanga tatu tu wanasonga CAF

Azizi Ki Simba, Yanga tatu tu wanasonga CAF

Sat, 11 Mar 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Simba na Yanga zinahitaji pointi tatu kila moja kufuzu hatua ya robo fainali ya michuano ya Shirikisho la Soka Afrika (Caf) na nafasi ya dhahabu kupenya ni kushinda mechi zao zijazo ambazo zote zinachezwa nyumbani kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Wekundu wa Msimbazi wataikaribisha Horoya ya Guinea Jumamosi ya Machi 18 katika mechi yao ya marudiano ya Kundi C la Ligi ya Mabingwa Afrika na siku itakayofuata Yanga itakuwa mwenyeji wa US Monastir ya Tunisia katika mechi ya Kundi D la Kombe la Shirikisho Afrika.

Takwimu za mechi za kwanza baina ya timu hizo ugenini, zinaleta matumaini makubwa kwa Simba na Yanga kushinda Kwa Mkapa na kutinga robo fainali.

Kule Guinea, Simba ilipoteza kwa bao 1-0 na kule Tunisia Yanga ililala 2-0, lakini hizi ni mechi ambazo matokeo hayafanani na kile kilichotokea uwanjani. Mabao yote hayo matatu waliyofungwa wawakilishi hao wa Tanzania yalitokana na mipira iliyokufa - Simba ilifungwa kutokana na mpira wa kona, wakati Yanga ilifungwa kwa mpira wa kona moja na frii-kiki moja.

Ndiyo, kipa Aishi Manula wa Simba aliokoa penalti ambayo ingeweza kuwapa Horoya mabao mawili na pia Horoya waligongesha nguzo, lakini Simba pia iligongesha nguzo na ilitawala kwa karibu kila kitu.

John Bocco alipaswa kufunga hat-trick, Jean Baleke alipaswa kufunga, Clatous Chama alikaribia kufunga na timu kiujumla iliupiga mwingi katika mechi ile. Hizi ni ishara njema kwamba Simba ina kila sababu ya kuifunga Horoya hapa nyumbani kama wachezaji watakuwa katika ubora wao, watatumia nafasi na kufanyia kazi udhaifu wa wapinzani.

SIMBA IKINOA KISU

Mashabiki wanaona kama Simba haina safu kali ya ushambuliaji msimu huu, lakini wanasahau Simba ndiyo timu iliyofunga mabao mengi zaidi kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu ikifunga mara 55 ikiwazidi vinara Yanga kwa mabao 13, kwani Wanajangwani wamefunga mabao 42 hadi sasa baada ya mechi 23.

Takwimu hizi za mabao zimetokana na timu hiyo kutengeneza nafasi nyingi za kufunga, kazi kubwa ikifanywa na Clatous Chama, Said Ntibazonkiza na wengineo wakiwamo Moses Phiri, Jean Baleke, Kibu Denis na Pape Sakho wanaocheza nafasi za ushambuliaji huku krosi za mabeki wa pembeni Shomary Kapombe na Mohammed Hussein 'Tshabalala' daima zikiwanyima usingizi mabeki wa upinzani.

Magoli ya kwenye Ligi Kuu hayakupatikana kwa bahati mbaya na nafasi nyingi walizotengeneza Simba kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa msimu huu hazikuja kwa kubahatisha bali ni mipango inayofanyika kuanzia kwenye viwanja vya mazoezi. Kama wachezaji wa Simba watatulia pale mbele kwa hizi nafasi nyingi zinazotengenezwa, Horoya itaoga mvua ya mabao.

MIPIRA ILIYOKUFA

Katika mechi zote ambazo Simba na Yanga zimecheza, zimeonekana kusumbuliwa na mipira ya kutengwa, iwe kona ama frii-kiki, ambazo wapinzani mara kwa mara walikuwa wakiiwahi mipira ya juu.

Katika kuwakabili wapinzani ambao mipira ya juu ni kati ya maeneo yao ubora, Simba na Yanga zinatakiwa kufanyia kazi jambo hilo ili kupunguza kutoa kona, kucheza faulo jirani na boksi la penalti na kuboresha 'taimingi' zao za kurukia mipira ya juu.

Simba na Yanga wakati ziliposhinda mechi zilizopita za Caf Kwa Mkapa, zilipunguza makosa ya aina hizo na hivyo kupunguza hatari za kujiweka kwenye hatari ya kuruhusu mabao.

Simba iliruhusu bao la kichwa dhidi ya Horoya kule Guinea hivyo inapaswa kujichunga, wakati wapinzani wa Yanga, Monastir licha ya kwamba watakuja Dar wakiwa tayari wamefuzu baada ya kufikisha pointi 10, wanaweza kuwa hatari zaidi kwa sababu watacheza wakiwa hawana presha ya matokeo hivyo wanaweza kufunguka na kuisumbua Yanga.

Monastir licha ya kuongoza la Yanga, lakini si timu ya kutisha sana kwa sababu katika mechi zake imekuwa ikiongoza kwa kuruhusu kushambuliwa na kupigiwa mashuti mengi, ikiokolewa na ushujaa wa kipa wao, ambaye pia ndiye nahodha. Walipigiwa mashuti 17 kule DR Congo wao wakipiga mashuti manne tu, lakini wakaibuka na ushindi wa 2-0 dhidi ya TP Mazembe.

Na hata katika mechi yao dhidi ya Mazembe ya kule Tunisia juzi, walifunga bao moja kwa mpira wa kutengwa na kushinda 1-0, huku kipa wao akiibuka shujaa wa mchezo kwa kuokoa hatari nyingi zilizoelekezwa langoni mwao. Kiufupi, Mazembe wanapaswa kujilaumu wenyewe kwa kukosa ushindi katika mechi zote mbili ambazo walitawala mchezo na kupiga mashuti mengi ambayo yaliokolewa na kipa ama kwenda nje ya lango.

Monastir, ambayo haijawahi kutwaa ubingwa wa Tunisia, inacheza soka la kujilinda zaidi ikizidiwa umiliki wa mpira na kupigiwa mashuti katika karibu kila mechi. Jambo hili ni faida kwa Yanga kwasababu timu bora zinazocheza soka la kujilinda ni zile ambazo mpinzani haruhusiwi kupiga shuti, lakini kwa inavyocheza kwa kumpa kipa wao kazi nzito ya kuokoa kila dakika ni wao tu Yanga washindwe wenyewe.

MAYELE AKIAMUA

Mayele akiamua kuongeza kitu kwa kuwashirikisha zaidi wenzake, Yanga itakuwa nafasi kubwa ya kufuzu kwa sababu uwepo wake pale katika eneo la ushambuliaji ni tatizo kubwa kwa wapinzani.

Katika mechi za siku za hivi karibuni, straika huyo Mkongomani amekuwa akifika mara nyingi jirani na lango la wapinzani, lakini amekuwa akipoteza nafasi nyingi ikiwamo kuwanyima wenzake nafasi za kufunga.

Pamoja na kuwa na mchango mkubwa kutokana na mabao yake na pia kutoa asisti kwa wenzake, lakini bado Mayele anaweza kuisaidia timu yake kufunga mabao mengi zaidi kama atapunguza kulazimisha kufunga katika nafasi ambazo ni ngumu kwake na badala yake akiamua kupasia wenzake walio katika nafasi bora zaidi.

Katika mechi iliyopita dhidi ya Real Bamako ambayo Yanga ilishinda 2-0 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Mayele angeweza kufunga 'hat-trick' (kama angefunga mpira wa krosi ya Djuma Shabani aliodundiza kichwa chini badala ya kulenga lango na kama asingepaisha krosi ya Jesus Moloko aliyopokea akiwa ndani ya boksi).

MIKONO SALAMA

Manula aliokoa penalti katika mechi ya kule Guinea dhidi ya Horoya na licha ya kufungwa bao moja la kona kule alikuwa nguzo muhimu ya kuokoa hatari kadhaa na kuipanga timu huku akiwapa mabeki wa Simba kujiamini katika mechi zote walizocheza hadi sasa kutokana na kuwafanya nyota wa timu hiyo waamini kwamba lango lao liko katika mikono salama, kama ilivyo kwa Djigui Diarra wa Yanga ambaye kiwango chake katika mechi zote alizocheza ameonyesha utulivu mkubwa na hata mara moja kuingia katika kikosi cha wiki cha Kombe la Shirikisho kutokana na kazi yake anayoifanya pale langoni.

Historia yake Diarra kwamba alianza kama mchezaji wa kiungo kabla ya kuwa kipa, inampa kujiamini kuutuliza mchezo na kuanza kujenga mashambulizi ya timu yake kuanzia nyuma au kupiga pasi ndefu sahihi za kwenda mbele, habutui mpira, hii ni faida kubwa kwa Yanga katika mechi za kusaka kuingia robo fainali.

VIKOSI BORA/ MFUMO

Baada ya Simba na Yanga kutawala takwimu muhimu katika mechi zao zote za nyumbani na hata ugenini (bila ya kujali matokeo), moja ya vitu muhimu vya kupenya robo fainali ni utulivu wa akili kwa wachezaji na kupanga vikosi bora katika mechi ya kila mmoja wao ya hapa Dar ili zile mechi zao za mwisho ugenini dhidi Raja Casablanca na TP Mazembe ziwe ni za kukamilisha ratiba tu.

Kikosi bora cha Simba kinachoweza kuumaliza mchezo mapema na kufuzu kibabe robo fainali huku wakiwa na mechi moja mkononi kinaweza kuwa: Manula, Kapombe, Mohammed Hussein, Onyango, Kanoute, Mzamiru, Saido, Chama, Phiri, Bocco. Mfumo: 4-2-3-1

Kikosi bora cha Yanga kinaweza kuwa: Diarra, Kibwana, Lomalisa, Mwanyeto, Job, Aucho, Mudathir, Moloko, Musonda, Mayele. Mfumo: 4-2-3-1

Chanzo: www.tanzaniaweb.live