Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba, Yanga ni kucheka au kulia

Onana X Pacome Simba, Yanga ni kucheka au kulia

Sat, 23 Dec 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Vigogo wa Ligi Kuu Bara, Simba na Yanga leo zinashuka katika michezo miwili tofauti ya mashindano hayo kusaka alama tatu baada ya kumalizana na wapinzani wao kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika katikati ya wiki hii.

Katika michezo ya katikati ya wiki, Simba iliikaribisha wydad Casablanca ya Morocco, Jumanne kwenye Uwanja wa Mkapa na kuichapa mabao 2-0, huku Yanga ikiikaribisha Medeama FC ya Ghana katika uwanja ambapo iliiadhibu mabao 3-0.

Baada ya kumaliza kibarua cha mechi hizo za kimataifa, vigogo hao wanarejea katika ligi ambapo Simba itakuwa mgeni wa KMC katika mchezo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Saalam kuanzia saa 10:00 jioni, huku Yanga ikikaribishwa na Tabora United katika Uwanja wa Jamhuri, Dodoma kuanzia saa 1:00 usiku.

Tabora United vs Yanga

Tabora United ambayo imepanda Ligi Kuu Bara msimu huu itakuwa na dakika 90 za kwanza dhidi ya Yanga inayopambana kutetea taji la ubingwa wa ligi hiyo kwa msimu wa tatu mfululizo.

Timu hiyo ililazimika kuhamia Dodoma kwa muda baada ya awali Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi kufungiwa ikitakiwa kuufanyia marekebisho na kamati inayosimamia ubora wa viwanja vinavyotumika kwenye ligi.

Hata hivyo siku chache kabla ya mchezo wa leo Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB) iliufungulia uwanja huo kuendelea kutumika, ingawa mechi ya leo itapigwa Dodoma badala ya Tabora na baada ya mchezo Tabora United watarejea katika uwanja wao.

Katika msimu huu wa kwanza kwa Tabora United imeonyesha haikuja kujaribu kucheza ligi ikiwa haijapoteza mechi ilizocheza nyumbani chini ya Kocha Mserbia Goran Kopunovic.

Timu hiyo inashika nafasi ya 11 ikiwa na alama 15 baada ya ushindi mara tatu na sare sita, ikichapwa mechi tatu zote za ugenini.

Ikitandaza soka la chini lenye pasi nyingi, Tabora United imekuwa na mwendo mzuri, lakini sasa inaanza safari ya kukutana na vigogo ikianza na Yanga baada ya awali kufungua ligi kwa kuchapwa na Azam FC mabao 4-0. Ukiacha ubora wa kipa John Noble golini, timu hiyo itakuwa mabegani mwa mfungaji wake kinara Eric Okutu ambaye ameshatupia nyavuni mabao manne huku kwenye kiungo ikiwategemea John Ben, Najim Ibrahim na Jackson Mbombo kusukuma mashambulizi.

Tabora United inarudi nyumbani ikitaka kubadilisha upepo wa matokeo baada ya kupoteza mechi ya mwisho ugenini ilipochapwa na Ihefu kwa mabao 2-1.

Akizungumzia mchezo huo, Kocha Goran alisema wanakutana na timu bora, lakini maandalizi waliyofanya yanawapa ujasiri wa kuzibakisha alama tatu nyumbani.

Goran ambaye amewahi kuifunga Yanga akiwa na Simba, alisema wageni wao wana mwendelezo mzuri wa kupata matokeo, lakini watahakikisha wanawafungia njia za kuzalisha mabao.

"Hii ni mechi kubwa na sote tunafahamu ubora wa Yanga. Ni timu ambayo inaundwa na wachezaji bora, lakini tumejipanga kupambana nao. Kwenye maandalizi nimewaambia wachezaji wanatakiwa kuiheshimu Yanga, lakini sio kuiogopa. Tuna wachezaji wenye kiu ya mafanikio na kwao mechi kama hizi ni daraja la mafanikio endapo watacheza kwa nidhamu kubwa haitakuwa rahisi kwa pande zote," alisema.

Kwa upande wake Yanga itaendelea kukosa huduma ya kiungo Khalid Aucho anayetumikia adhabu ya kusimamishwa mechi tatu sambamba na beki Lomalisa Mutambala ambaye bado hajapona vizuri.

Kwenye mechi tano zilizopita Yanga ilikuwa na ubora wa kufunga mabao nyumbani na ugenini ikifunga 14 na pia ukuta wake ukiruhusu matatu.

Akili ya Yanga ni kusaka alama tatu zitakazoiwezesha kukimbizana na Azama FC ambayo imekusanya alama 31, ilhali yenyewe ikiwa nazo 27 katika michezo 10 iliyocheza. Azam imecheza mechi 12.

Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi amewataka wachezaji wake kusahau kwa muda kila kitu kuhusu Ligi ya Mabingwa ili kujikita kusaka ushindi katika Ligi Kuu.

Gamondi alisema wameifuatilia kwa kina Tabora United na kugundua ni timu ambayo inacheza soka safi la chinichini, lakini anaamini ubora wa wachezaji wake na mazoezi waliyofanya utawabeba.

"Tumepata muda mfupi wa kurudisha miili yetu sawa baada ya mechi dhidi ya Medeama, lakini nimewaambia wachezaji wangu wasahau kabisa kwa muda mambo ya Ligi ya Mabingwa. Sasa tunarudi kwenye mechi ambazo sote tunajuana vizuri," alisema.

"Tabora sio timu rahisi ukiwaangalia wanavyocheza utagundua hilo. Wanacheza soka la ufundi na kuweka mpira chini. Unatakiwa kuwa makini na timu za aina hii ili uweze kufanikiwa."

KMC vs Simba Katika mchezo baina ya timu hizo, KMC iliyokuwa inatumia Uwanja wa Uhuru uliofungiwa na Bodi ya Ligi kutokana na kutokidhi vigezo kuanzia sasa inatumia ule Azam Complex.

KMC haijawahi kuifunga Simba na katika michezo minane iliyopita matokeo mazuri dhidi ya Simba ilikuwa ni sare ya mabao 2-2 mechi iliyopigwa Septemba 7,2022, lakini nje ya hapo imeziacha alama zote kwa Wekundu wa Msimbazi.

Kikosi hicho Cha Manispaa ya Kinondoni kitaingia kwenye mchezo kikitambua kuwa kimeruhusu mabao 19 katika Ligi Kuu msimu huu, kikifunga mabao 13 katika mechi 13. Na dhidi Simba KMC imefunga mabao matano katika mechi nane walizokutana. Katika mechi tano zilizopita KMC imeshinda moja na kupoteza mbili, huku ikitoka sare mara mbili, lakini kwa sasa inajua inakwenda kukutana na Simba ambayo imeanza kujipata baada ya kujitafuta kwa muda mrefu.

Ndani ya kikosi cha KMC mshambuliaji Waziri Junior mwenye mabao matano ndiye mchezaji hatari na tegemeo na ni wazi kwamba Simba inapaswa kumchunga, huku kando yake akiwepo kiungo Awesu Awesu mwenye mabao matatu.

Akizungumzia mchezo huo, Kocha Abdihamid Moalin wa KMC alisema itakuwa mechi ngumu, lakini wamejipanga kupata ushindi.

"Haiwezi kuwa mechi rahisi. Sote tumeona Simba imebadilika hivi karibuni. Wamerudi kuanza kucheza kama timu kubwa. Timu yao ina wachezaji wengi wenye uzoefu, tunatakiwa kucheza kwa akili kubwa," alisema Moalin.

"Ni kweli hatujawahi kushinda dhidi ya Simba, nafikiri hii ni changamoto nyingine kubwa kwetu kwenye mchezo huo. Tutatafuta namna ya kubadilisha historia kulingana na maandalizi tuliyofanya. Naamimi tunaweza kuwa na mechi tofauti."

Simba chini ya kocha Abdelhak Benchikha imeanza ligi kwa kishindo ikishinda mabao 3-0 dhidi ya Kagera Sugar kabla ya kuifumua Wydad kwa mabao 2-0 katika Ligi ya Mabingwa Afrika.

Chanzo: Mwanaspoti