Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba, Yanga mpaka kieleweke CAF

Simba, Yanga Waanza Kuweka Viporo Mechi Za NBC Simba, Yanga mpaka kieleweke CAF

Mon, 27 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Michuano ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, imeanza wikiendi iliyopita kwa wawakilishi wa Tanzania, Yanga na Simba wakitupa karata zao za kwanza kwenye viwanja viwili tofauti.

Yanga ilikuwa ugenini kule Algeria kuvaana na CR Belouizdad na kulala kwa mabao 3-0, huku watani wao wakisalia nyumbani na kuikaribisha Asec Mimosas ya Ivory Coast na kulazimishwa sare ya 1-1.

Matokeo hayo yanapaswa kutumiwa na timu hizo kama chachu kwa ajili ya kujipanga vyema kwa mechi zijazo za raundi ya pili, wakati Yanga itarudi nyumbani wikiendi hii kuikaribisha Al Ahly ya Misri, ilihali Simba itasafiri hadi Gaborone, Botswana kuvaana na Jwaneng Galaxy.

Ni wazi Yanga haitataka kupoteza mchezo wa pili wa Kundi lake la D tena ikiwa nyumbani, huku Simba ikitaka kusahihisha makosa yake ya kushindwa kulinda bao nyumbani na kulazimishwa sare ya 1-1 na Asec, ili kulipa kisasi kwa wapinzani wao wa Jwaneng waliowakwamisha misimu miwili iliyopita kucheza makundi ya Ligi ya Mabingwa kwa kuing’oa kwa kanuni ya bao la ugenini.

Mwanaspoti, kama wadau wa michezo tunaamini matokeo ya mechi hizo za kwanza hayawezi kuzikatisha tamaa timu hizo zinazocheza kwa mara ya kwanza pamoja katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kwani matokeo hayo kwa timu zote ni sehemu ya mchezo na sasa wanatakiwa kujipanga kwelikweli ili mambo yawe mepesi kwao kabla hatua ya makundi haijachanganya zaidi huko mbele.

Kwa aina ya wachezaji ilizonazo timu hizo hasa wale wenye uzoefu mkubwa anga la kimataifa ni wazi, matokeo ya mechi hizo yamewafanya wazinduke na kujipanga zaidi kwa michezo ijayo ili kuzibeba timu hizo kwenye harakati za kusaka tiketi ya kutinga robo fainali.

Tunaamini mechi hizo zijazo za wikiendi hii, Simba na Yanga zitashuka viwanjani kuwakabili wapinzani wao wakiwa na mzuka mwingi na kusahau kila kitu kilichotokea kwenye michezo iliyopita kwani kuteleza sio kuanguka.

Tunalisema hili kwa kurejea msimu uliopita kwenye mechi zao za makundi, Simba ikicheza Ligi ya Mabingwa ilicharazwa bao 1-0 na Horoya ya Guinea, huku Yanga ikiwa makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika ilinyukwa mabao 2-0 na US Monastir ya Tunisia.

Hata hivyo, kila mmoja anajua licha ya kuanza vibaya, timu hizo zilijipanga upya na kufanikiwa kuvuka hatua ya makundi, Simba ikiishia robo fainali na Yanga kufika fainali ya michuano iliyoshiriki na kukosa taji kwa kanuni ya bao la ugenini tu kwani matokeo ya mwisho na USM Alger ilikuwa ni sare ya mabao 2-2.

Ndio maana tunazitaka timu hizo kutokata tamaa kwa sasa ama kupaniki kwa kile ilichovuna kwenye mechi zao za kwanza.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live