Ukisikia mshindwe wenyewe ndiyo hii sasa, pengine hiki ndiyo kipindi bora zaidi katika soka la Tanzania tangu lilipozaliwa kwa zaidi ya miaka 80 iliyopita.
Yaani kuwa na timu mbili na kongwe kwenye mashindano mawili makubwa tofauti ya ngazi ya klabu Afrika kwenye hatua kubwa mbili tofauti pia.
Nchi na soka letu limefikia hapa sasa, Yanga wanacheza robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika wakiwa wametanguliza mguu mmoja kwenye hatua ya nusu fainali.
Wakati Simba wao kama Yanga kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, wapo mguu mmoja kwenye nusu fainali. Simba waliwafunga Wydad Casablanca bao 1-0 kwa Mkapa kwenye mechi ya duru ya kwanza.
Huku Yanga wakiwaburuza Rivers United wakiwa kwao Nigeria kwa mabao 2-0 kwenye mechi ya kwanza. Timu zote wiki hii watacheza mechi za marudiano za kuamua nani anakwenda nusu fainali na nani anaondoka.
Hii ni maana ya kuwa wameshakula ng’ombe mzima na wamebakiza mkia tu. Yaani hapa washindwe wenyewe tu. Sasa kwenye hatua kama hizi umakini unahitajika zaidi kwani unaweza ukaharibu ndoto kubwa kwa muda mfupi tu.
Simba wao watakuwa wa kwanza kucheza mechi yao Ijumaa hii na Yanga itamaliza kazi Jumapili. Kila la heri wawakilishi wetu ki mataifa, mikfanikiwa ninyi tumefanikiwa taifa zima. Tunaamini nyie wote mna silaha zenye kufanikiwa kuwashinda wapinzani wenu.