Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba, Yanga kulipa kisasi leo

Simba Queens 2023 Kikosi cha Simba Queens

Wed, 14 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara (SWPL), inaendelea leo kwa mechi za raundi ya pili kupigwa katika viwanja mbalimbali huku mtihani mkubwa ukiwa kwa vigogo, Simba Queens na Yanga Princess ambao waliangusha pointi katika mechi zao za kwanza.

Raundi ya kwanza ya ligi hiyo ilipigwa Desemba 6 na 7, mwaka huu na bingwa mtetezi, Simba Queens alianza kwa kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa JKT Queens huku Yanga Princess nao wakichapwa bao 1-0 na Fountain Gate Princess, wakati Alliance Girls ya Mwanza ikiichapa Ceassia Queens ya Iringa bao 1-0.

The Tigers Queens ya Arusha ililazimishwa sare ya 1-1 na Mkwawa Queens ya Iringa huku Amani ya Lindi ikiambulia sare ya 1-1 nyumbani dhidi ya Baobab Queens ya Dodoma.

Michezo yote mitano ya raundi ya pili itapigwa leo saa 10 jioni na Simba Queens itakuwa ugenini Uwanja wa Black Rhino, Arusha dhidi ya The Tigers Queens inayoingia kwenye mchezo huo ikiwa na benchi jipya la ufundi baada ya Sebastian Nkoma kutimkia Yanga Princess, huku uongozi wa timu hiyo ukigoma kutaja kocha mpya na wasaidizi wake ambao watatambulishwa siku chache zijazo.

Afisa Habari wa The Tigers, Ibrahim Sikon alisema wanafahamu Simba Queens itakuja na presha kubwa ya kuhitaji matokeo lakini wameshawaandaa kisaikolojia wachezaji wao na wanajua nini cha kufanya ili kuondoka na ushindi huku akitamba baadhi ya wachezaji wao muhimu walioukosa mchezo uliopita akiwemo kipa wa timu ya taifa ya Kenya, Samantha Akinyi, wamerejea.

“Tumejiandaa vizuri dhidi ya Simba Queens imani yetu ni kubwa kuelekea mchezo huu kwa hiyo hakuna ugumu wowote na tutaondoka na pointi tatu, tumeshawaeleza wachezaji nini kinatakiwa kufanyika tunajua Simba itakuja kwa presha kubwa lakini tumejiandaa vyema tutawapiga na kitu kizito,” alisema Sikoni.

Yanga Princess itakuwa nyumbani Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam kuikaribisha Mkwawa Queens ya Iringa ambao ni msimu wao wa kwanza kwenye ligi hiyo, na Yanga watakuwa chini ya kocha mpya, Nkoma aliyechukua mikoba ya Edna Lema aliyetimuliwa baada ya kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Fountain Gate Princess.

Akizungumzia mchezo huo, Meneja wa Mkwawa Queens, Said Chitalula alisema “Japokuwa ni wageni na Yanga princess ni wakongwe lakini tumejiandaa vizuri na tuko tayari kushindana na kupata matokeo mazuri.”

Mtanange mwingine ni kati ya Alliance Girls ya Mwanza dhidi ya JKT Queens ya Dar es Salaam, Uwanja wa Nyamagana na Kocha msaidizi wa JKT Queens, Greyson Haule alisema, “Tahadhari kwa kila mechi lazima iwepo, Alliance Girls ni timu nzuri lazima tuhakikishe tunapata matokeo na tuko tayari kwa mchezo huu kwa sababu tunahitaji kuwa na mwendelezo wa kile tulichokipata mchezo uliopita.”

Fountain Gate Princess ya Dodoma leo itakuwa ugenini kuvaana na Amani Queens ya Lindi, Uwanja wa shule ya sekondari Nyangao, huku Kocha mkuu wa Fountain Gate, Alex Alumirah akitamba amewaandaa wachezaji wake kuwa na mwendelezo mzuri na kuacha kujiamini kupitiliza.

“Tulishinda mchezo wa awali tunaamini imetuongezea ugumu wa michezo inayofuata hivyo wachezaji wangu nimewaandaa kuhakikisha tunapata matokeo na siyo kujiamini zaidi kwa sababu mchezo wa soka hauna matokeo ya historia,” alisema Alumirah.

Michezo mwingine itakayochezwa leo ni Baobab Queens ya Dodoma itaikaribisha Ceassia Queens ya Iringa katika Uwanja wa Jamhuri, Dodoma kuanzia saa 10 jioni.

Chanzo: Mwanaspoti