Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba, Yanga kimataifa: Kila mtu shinde zake

Yanga X Simba Moyo Mayeler na Phiri

Fri, 17 Feb 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kila mtu ashinde mechi zake ndivyo hesabu zinavyosoma kwa wawakilishi wetu wa kimataifa katika ngazi ya klabu, yaani Simba na Yanga ambao wanatarajiwa kushuka uwanjani wikiendi hii kujiuliza kwa mara ya pili katika michezo ya mashindano wanayoshiriki.

Hii ni baada ya wote wawili wikiendi iliyopita kujikuta wakiangukia pua kwenye karata yao ya kwanza ugenini ambapo Simba walipoteza kwa bao 1-0 mbele ya Horoya AC nchini Guinea, huku Yanga wao wakikubali kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa US Monastir ya Tunisia.

Ikumbukwe kuwa katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika Simba ndiyo wawakilishi pekee wa Tanzania katika mashindano hayo ambapo wamepangwa kundi C pamoja na timu za Vipers ya Uganda, Raja Casablanca ya Morocco na Horoya AC ya Guinea.

Watani zao wa jadi Yanga wao wanaibeba bendera ya Tanzania katika mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika ambapo mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara wamepangwa kwenye kundi D, pamoja na timu za TP Mazembe ya DR Congo, US Monastir ya Tunisia na Real Bamako ya Mali.

Timu hizi zilirejea nchini mwanzoni mwa wiki hii na tayari kila moja imeendelea na maandalizi ya michezo ya wikiendi hii.

TanzaniaWeb inakuletea baadhi ya dondoo muhimu kuhusu shoo hizi kali za kimataifa wikiendi hii.

KWA MARA YA KWANZA BAADA YA MIAKA MITANO

Hii inatarajiwa kuwa mara ya kwanza ndani ya kipindi cha misimu minne kuziona Simba na Yanga zikicheza michezo ya hatua ya makundi ya mashindano ya kimataifa ambapo mara ya mwisho tulishuhudia haya msimu wa 2018.

Simba wao wanajivunia kuwa na nyakati nzuri kimataifa ambapo katika kipindi cha misimu minne iliyopita yaani tangu msimu wa 2018/19 mpaka 2021/22 wamefanikiwa kucheza hatua ya robo fainali ya mashindano ya Afrika mara tatu, mbili za Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya TP Mazembe na Kaizer Chiefs huku robo fainali moja ni ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2021/22 dhidi ya Orlando Pirates.

Mara ya mwisho Yanga kushiriki makundi ya mashindano ni mwaka 2018.

MARA YA MWISHO KWA MKAPA

Simba mara ya mwisho kukipiga kwenye Uwanja wa Mkapa kwenye mashindano ya kimataifa ilikuwa ni Oktoba 16, mwaka jana ambapo waliibuka na ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na kiungo mshambuliaji Mzambia, Moses Phiri ulikuwa mchezo wa hatua ya mtoano.

Ushindi huu uliifanya Simba kuandikisha ushindi wa jumla wa mabao 4-1 kufuatia ushindi wa mabao 3-1 kwenye mchezo wa kwanza ugenini.

Yanga wao mara ya mwisho wakicheza katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kwenye mashindano ya kimataifa ilikuwa Novemba 2, mwaka jana ambapo walilazimishwa suluhu na Club Africain ya Tunisia kwenye mchezo wa hatua ya mtoano.

MORRISON, KANOUTE KUIKOSA SHOO

Simba watakuwa wanajivunia kurejea kwa kiungo wao wa kimataifa wa Burundi, Saido Ntibazonkiza ambaye alikosekana kwenye mchezo dhidi ya Horoya AC kutokana na changamoto ya majeraha ya misuli ambayo ilikuwa ikimsumbua, ambapo tayari staa huyo amefanya mazoezi na wenzake kuelekea mchezo huu.

Simba pia huenda wakaongezewa nguvu ya kiungo Mmalawi, Peter Banda ambaye naye hakwenda Guinea kutokana na majeraha na alitarajiwa kufanyiwa vipimo vya mwisho jana. Pamoja na hao Simba watapata pigo la kumkosa Sadio Kanoute anatumikia adhabu ya kadi tatu za njano.

Yanga wao Jumapili wataendelea kukosa huduma ya Bernard Morrison na Aboutwalib Mshery ambao wana majeraha ya muda mrefu huku sehemu kubwa ya kikosi ikiwa salama.

RAJA WATUA KIBABE BONGO, TP MAZEMBE MUDA WOWOTE

Baada ya safari ndefu kutoka nchini Morocco hadi Qatar, kikosi cha Raja Casablanca jana Alhamisi kilitarajiwa kutua jijini Dar es Salaam tayari kwa ajili ya maandalizi ya mwisho ya mchezo huo.

Kupitia kurasa zao za mitandao ya kijamii, Raja wameweka wazi wanajivunia kuja kucheza katika nchi yenye mapenzi makubwa na mpira wa miguu kama Tanzania na kutamba kuwa kikosi chao kina Morali ya kutosha, huku wapinzani wa Yanga TP Mazembe wakitarajiwa kuwasili muda wowote kuanzia jana Alhamisi jioni.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live