Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba, Yanga ijayo sasa ni Aprili 9

Simba Vs Yanga Simba, Yanga ijayo sasa ni Aprili 9

Sun, 1 Jan 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Habari ndio hiyo. Baada ya sare ya 1-1 katika mechi ya kwanza ya Kariakoo Derby kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu, miamba Simba na Yanga itarudiana tena ili kumaliza ubishi baina yao katika pambano litakalopigwa Aprili 9 mwakani kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Awali, pambano hilo lilikuwa limepangwa kupigwa Februari, lakini limesogezwa mbele baada ya mabadiliko madogo yaliyofanywa na Bodi ya Ligi (TPLB) kutokana na mechi za ligi hiyo kuingiliana na michuano ya Kombe la ASFC, Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika na michuano ya Chan kwa timu ya taifa.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mtendaji Mkuu wa TPLB, Almas Kasongo alisema ratiba ya awali mchezo huo wa duru la pili haukupangwa rasmi japo ulionekana ungepigwa Februari mwakani na sasa utachezwa Aprili 9 kuanzia saa 11:00 jioni.

Hapa Mapinduzi kuna vita nzito

Katika mechi yao ya kwanza, Simba ilitangulia kwa bao la Augustine Okrah kabla ya Stephane Aziz KI kusawazisha sekunde chache kabla ya mapumziko ya mechi hiyo iliyopigwa Oktoba 23.

Alisema wamefanya mabadiliko kulingana na sababu mbalimbali ikiwemo ushiriki wa timu tano za Bara katika michuano ya Kombe la Mapinduzi linalotajiwa kuanza kesho Jmapili.

“Kuna sababu saba zilizotulazimisha kufanya mabadiliko ya ratiba ya Ligi Kuu, ikiwemo Kombe la Mapinduzi, imekuwa ikiendelea kwa miaka mingi, tunatambua mchango wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika michezo na tumeamua kufanya mabadiliko kwa sababu ya timu tano kutoka Bara kwenda kucheza michuano hiyo,” alisema Kasongo na kuongeza;

“Sababu ya pili ni kuhusu timu yetu ya Taifa Stars na michuano ya CHAN itakayofanyika nchini Algeria, katika ratiba yetu ya awali tuliweka makadirio ya timu yetu kufika mbali, lakini imeondolewa hivyo ikatulazimu kuiboresha ratiba.”

Alieleza sababu nyingine ni michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika na Ligi ya Mabingwa Afrika, kwa Yanga na Simba. kwa kuzipa nafasi klabu hizo kujiandaa na michuano hiyo inayotarajiwa kuanza Febuari.

Alisema wamewaondolea mechi za karibuni ambazo wanatakiwa kucheza mwezi huo na kuzipa muda wa timu hizo kujiandaa vizuri kuelekea michuano hiyo ya Kimataifa kwa sababu ni wawakilishi pekee Tanzania.

“Mabadiliko haya pia yamezingatia Taifa Stars kuelekea michuano ya AFCON, tukiwa na mechi mbili za nyumbani na ugenini dhidi ya Uganda zitakazopigwa kati ya Machi 20-28, 2023,” alisema Kasongo.

Alisema kuelekea michuano hiyo Taifa Stars inatakiwa kuingia kambini mapema kwa ajili ya michezo hiyo lakini pia ratiba huyo imezingatia uwapo wa Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) na sababu nyingine za mikataba hasa kwa Azam TV.

“Febuari 12 na Mei 19 hadi 25, itakuwa ni Wiki ya Kombe la ASFC kwa kuchezwa mechi za Mzunguko wa 32, 16-Bora, robo na nusu fainali.

“Sababu ya mwisho ni ya kikanuni, kabla ya Corona kushamiri, ligi ilichezwa kuanzia Agosti hadi Mei lakini baada ya Corona mambo yakabadilika na sasa tunahitaji kurejea katika utaratibu wa awali ambao mechi za mwisho zitachezwa tarehe moja (Mei 28, 2023), kwa timu zote kucheza muda mmoja,” alisema.

Chanzo: Mwanaspoti