Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba, Yanga SC freshi zikijipanga zinatoboa

Simba Vs Yanga Kibu DD.jpeg Simba, Yanga SC freshi zikijipanga zinatoboa

Mon, 4 Dec 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kimahesabu, Simba na Yanga bado zina nafasi ya kutoboa kwenda robo fainali kupitia mechi nne zilizosalia katika makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kila mmoja, licha ya kwamba zimeanza vibaya kwa kutopata ushindi kwenye michezo miwili iliyocheza hadi sasa ikiwamo ya juzi Jumamosi.

Simba iliyopo Kundi B, ikiwa Botswana ikicheza na Jwaneng Galaxy ililazimishwa suluhu jijini Francistown, huku Yanga ikiwa nyumbani Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam ilitoka sare ya 1-1 na watetezi wa taji la michuano hiyo, Al Ahly ya Misri kwenye mchezo wa Kundi D.

Awali, Yanga ilianza kwa kukandikwa mabao 3-0 ugenini na CR Belouizdad ya Algeria, wakati Simba ikiwa nyumbani Kwa Mkapa ilitoka sare ya 1-1 na vinara wa kundi lao, ASEC Mimosas ya Ivory Coast na kuziweka pabaya kwenye misimamo ya makundi hayo.

Pointi mbili ilizovuna Simba kundini zimeifanya ishike nafasi ya tatu nyuma ya Asec na Jwaneng, kisha Wydad Casablanca iliyopoteza michezo miwili mfululizo ikiburuza mkiani bila ya pointi, wakati Yanga yenyewe ndio inayozibeba timu za Kundi D ikiwa na pointi moja, huku Al Ahly ikiongoza msimamo.

Wawakilishi hao wa Tanzania wote watakuwa ugenini wikiendi hii, kwa Yanga kuvaana na Medeama wakati Simba itakuwa wageni wa Wydad na mechi hizo ndizo zinazoweza kutoa dira kwa wababe hao wa soka nchini kabla ya kurudi nyumbani wiki ijayo kurudiana na wapinzani wao hao na kusubiri tena hadi mwakani.

Makocha wa vikosi vyote viwili, Miguel Gamondi kwa Yanga na Abdelhak Benchikha kwa Simba, vichwa vitakuwa vinawauma wakitafuta mbinu bora zaidi ambazo zitawasaidia katika hekaheka ya kusaka pointi 12 kwa mechi zilizopo mbele yao, zikiwa mbili za kufungia mwaka na zile za mwishoni za mwakani.

Kimahesabu ni kwamba timu hizo zina nafasi ya kupenya kama itazichanga karata zao vyema, kwa kurejea kilichojiri msimu uliopita Simba ilivyovuka kwenda robo fainali katika Ligi ya Mabingwa Afrika licha ya kuanza kwa kupoteza mechi mbili mfululizo mbele ya Raja Casablanca iliyoitungua nyumbani mabao 3-0 kuisha kwenda kupoteza ugenini mbele ya AC Horoya ya Guinea.

Yanga yenyewe katika makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita ilianza kwa kichapo cha 2-0 kutoka kwa US Monastir ya Tunisia, lakini ilijikaza msuli na kuifunga TP Mazembe 3-1 licha ya kuja kulazimishwa sare ya 1-1 na Real Bamako ya Mali, mwishowe ilisonga hadi fainali ya michuano hiyo.

SIMBA UTULIVU TU

Katika mechi ya juzi Simba ikiwa chini ya kocha mpya, Abdelhak Benchikha ilicheza vizuri kwa kutengeneza nafasi nyingi tofauti na mechi iliyopita dhidi ya Asec, lakini washambuliaji wake walikosa utulivu na kujinyima mabao mbele ya Jwaneng.

Takwimu zinaonyesha Simba ilipiga mashuti 16, huku matatu tu ndio yaliyolenga lango, mbali na kufanya mashambulizi mengi ya hatari langoni mwa Jwaneng ilipata ugumu mbele ya Wekundu hao kiasi cha kupiga mashuti matano tu huku moja likilenga lango.

Simba iliumiliki mchezo huo kwa asilimia 65 na kupiga jumla ya pasi 461 ambazo asilimia 80 zilikuwa sahihi, tatizo lilikuwa utulivu kwenye eneo la mwisho ambalo lilikuwa likiongozwa na Jean Baleke aliyekuwa akisaidiana na Sadio Ntibazonkiza, Kibu Denis na Willy Essomba Onana ambaye alionekana kuchemka.

Baada ya hesabu kuwa tofauti katika kipindi cha pili, Simba ilifanya mabadiliko kadhaa yaliyoonekana kuipa timu uhai hasa alipoingia Clatous Chama ambaye hata hivyo naye alipoteza nafasi katika dakika za mwisho cha mchezo baada ya kuwahadaa mabeki wa Jwaneng na kupiga shuti lililoishia kugonga nguzo ya chini.

Ni ngumu kumlaumu Benchikha kutokana na ukweli hana muda mrefu tangu aanze kuinoa timu hiyo, lakini namna timu ilivyocheza Botswana ni wazi, kuna kitu na sasa ana kibarua cha kukaa na wachezaji wake na kufanyia kazi upungufu uliojitokeza kwenye mchezo huo wa kwanza kwake ili mambo yawe mepesi.

Matokeo ya Wydad kwenye michezo miwili iliyopita yanatoa tumaini kwa Simba kuweza kuambulia japo pointi ugenini kama Benchikha ataimarisha utulivu kwa washambuliaji wa timu hiyo na kutumia nafasi inazotengeneza kuwa mabao ili kujitengenezea nafasi ya kuvuka kundini kwenda robo fainali.

Kitu cha muhimu ni mabeki wa Simba hasa wa pembeni kuwa makini kutokana na ukweli Wydad inatumia sana mipira ya pembeni na wachezaji wao wana kasi, hivyo ni vyema Benchikha kukomaa eneo hilo zaidi.

YANGA HAINA STRAIKA

Kwa kuwaheshimu Al Ahly, Gamondi aliingia na mpango wa kucheza na mabeki wa kati watatu ambao ni Dickson Job, Bakari Mwamnyeto na Ibrahim Abdallah Hamad ‘Bacca’ ili kuwa imara zaidi katika eneo lake la kujilinda kutokana na ubora wa wapinzani wake.

Licha ya Yanga kuruhusu bao katika dakika ya 86 walilofungwa na Percy Tau, Wananchi walikuwa bora katika kujilinda na timu ilikuwa na uwiano mzuri hata katika kushambulia ambapo Zouzoua Pacoume, Maxi Nzengeli na Stephane Aziz Ki nao walifanya kazi kubwa katika maeneo tofauti ya ushambuliaji, wakifanya kile ambacho kiliwezekana na hatimaye likapatikana bao la kusawazisha lililofungwa na Pacoume katika dakika 90+1.

Namna ambavyo Yanga ilikuwa ikipambana kusaka matokeo ni wazi kuwa ilionyesha ina kitu ambacho kinaweza kuwasaidia katika michezo yao ijayo ikiwa itachanga vizuri karata zake katika kituo kinachofuata ambacho ni Ghana kucheza dhidi ya Medeama baada ya hapo itarejea Dar kumalizana nayo hiyo hiyo kwenye mchezo wa pili.

Kwenye mechi ya juzi Yanga ingeweza kupata ushindi kama ingetumia nafasi ilizotengeneza ambao zilikosa mshambuliaji wa kutupia nyavuni kama ilivyotokea kwenye mchezo wa kwanza dhidi ya CR Belouizdad. Licha ya Clement Mzize, Kennedy Musonda na Hafiz Konkoni kuwa mastraika, lakini bado wameshindwa kuifanya kazi kwa ufanisi kitu ambacho Gamondi ana kazi ya kufanya kwa ajili ya mechi nne zilizosalia.

Upande wa takwimu dhidi ya Al Ahly, Yanga ilikuwa na umiliki wa mchezo kwa asilimia 47 huku ikipiga mshuti 11 ni mawili tu ambayo yalilenga lango, wapinzani wao walipiga mshuti 15 huku saba yakilenga lango.

KAZI IPO HUKU

Kati ya makundi ambayo yanaonekana kuwa msisimko wa aina yake kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ni pamoja na kundi A, unajua kwanini? Hakuna mababe hadi sasa, unaambiwa kila mmoja ameonja ushindi na kipigo kwenye kundi.

Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini ambayeo mechi yake ya kwanza ilishinda ilitandikwa bao 1-0 na TP Mazembe ambao wanautumia Uwanja wa Mkapa kama machinjio yao, Nouadhibou ya Mauritania ilionyesha kuwa wao sio wanyonge kama ambavyo wengi walikuwa wakiwatazama kwa kuitandika Pyramids ya Fiston Mayele kwa mabao 2-0.

Hadi sasa baada ya raundi mbili kila kundi mbabe ni Petro de Luanda ya Angola tu aliyevuna pointi zote (6)

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: