MATOKEO ya ushindi ilizopata Simba na Yanga katika mechi za kimataifa yamemuamsha nyota wa zamani wa timu hizo, Willy Martin ‘Gari Kubwa’ aliyesema timu hizo sasa zina dakika 90 za kibabe ambazo ni kama fainali katika mechi za nyumbani zitakazoamua hatma ya kufuzu robo fainali.
Simba iliifunga Vipers ya Uganda kwa bao 1-0 katika mechi ya Kundi C ya Ligi ya Mabingwa Afrika wakati Yanga iliinyoosha Real Bamako ya Mali kwa mabao 2-0 kwenye mchezo wa Kundi D wa Kombe la Shirikisho na kujiweka pazuri kwenye makundi hayo.
Ushindi wa juzi umeifanya Simba ifikishe pointi sita ikiwa nafasi ya pili katika msimamo, ikisaliwa na mechi mbili ikiwamo moja ya nyumbani dhidi ya Horoya itakayopigwa Machi 18 na kama itapata ushindi itajihakikisha kwenda robo fainali kuungana na Raja Casablanca ya Morocco iliyotangulia.
Kwa upande wa Yanga, ushindi wa juzi umeifanya ifikishe pointi saba ikiganda nafasi ya pili kwenye Kundi D na itakuwa nyumbani kuikaribisha US Monastir ya Tunisia katika mechi itakayopigwa Machi 19 na kama itashinda itaungana na Watunisia waliotangulia mapema kwenda robo fainali.
Akizungumza na Mwanaspoti, Gari Kubwa aliyezichezea timu hizo kwa nyakati tofauti na kuzipa mafanikio makubwa, alisema kwa sasa ni dakika 90 za kibabe za za kufa au kupona kwa watani hao kuhakikisha wanashinda.
Gari Kubwa alisema kwa mwenendo waliozionyesha Simba na Yanga haswa katika mechi za nyumbani umewapa nguvu Watanzania katika kuzitabiria makubwa msimu huu kuendelea kuwakilisha nchi vyema kimataifa.
“Kikubwa wasibweteke, hizi mechi zinazofuata ndizo zinaenda kuamua hatma yao, niwaombe wachezaji, viongozi, wadau na mashabiki huu ndio muda wa kuzisapoti zaidi timu zetu ili ziendelee kuwakilisha nchi,” alisema Gari Kubwa na kuongeza;
“Tumekuwa na rekodi nzuri ya kuwakilishwa na timu nne kimataifa, hivyo lazima tuendelee kutetea nafasi hii mataifa mengi yanatamani fursa hii hivyo tuziombee sana timu zetu.”
Simba na Yanga zimekuwa na matokeo mazuri nyumbani ambapo katika michezo miwili ilizocheza Uwanja wa Taifa zimeshinda zote na kujiweka mazingira mazuri ya kufuzu hatua inayofuata.